MKOA wa Ruvuma unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5.362 katika Halmashauri zote nane kupitia tozo ya miamala ya simu.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema kati ya fedha hizo shilingi bilioni tano zimejenga vituo vya afya kumi na zaidi ya shilingi milioni 360 zimejenga vyumba vya madarasa 29.
Amesema miradi hiyo inatekelezwa katika Halmashauri zote nane mkoani Ruvuma ambapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga miradi inayotekelezwa ina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja.
Ameitaja miradi inayotekelezwa katika Halmashauri Mbinga kuwa ni ujenzi wa kituo cha afya Mkumbi na kituo cha afya Kindimbachini vinavyogharimu shilingi bilioni moja na umaliziaji wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari Nyoni na Litumbandyosi unaogharimu shilingi milioni 50.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa,Katika Halmashauri ya Madaba serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 525 kutekeleza miradi ya Kituo cha Afya Matetereka ambacho kinagharimu shilingi milioni 500 na ujenzi wa madarasa mawili katika sekondari ya Lipupuma ambayo yanagharimu shilingi milioni 25.
RC Thomas ameitaja miradi inayotekelezwa kupitia tozo ya miamala ya simu katika Halmashauri ya Mbinga Mji inagharimu shilingi milioni 537 ambazo zinatumika kutekeleza miradi ya ujenzi wa kituo cha Afya Mbangamao ambacho kinatumia shilingi milioni 500 na umaliziaji wa vyumba viwili vya madarasa katika sekondari ya Kilimani na chumba kimoja sekondari ya Lamata ambavyo vinagharimu zaidi ya shilingi milioni 37.
Kanali Thmoas amesema katika Halmashauri ya Namtumbo serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 537 ambazo zinatumika kujenga kituo cha Afya Ligera ambacho kimetengewa shilingi milioni 500 na ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa sekondari ya Nasuli na vyumba viwili sekondari ya Mbunga ambavyo vinatumia zaidi ya shilingi milioni 37.
Kulingana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,miradi inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa inagharimu shilingi milioni 537 ambapo shilingi milioni 500 zinatumika kujenga jengo la upasuaji,wodi ya akinamama katika kituo cha afya Liparamba,ujenzi wa nyumba ya watumishi wa afya,jengo la mionzi na njia ya kutembea wagonjwa.
Ameitaja miradi mingine inayotekelezwa katika Halmashauri ya Nyasa kuwa ni umaliziaji wa vyumba vya madarasa vitatu katika shule za sekondari Luhangarasi na Kingerikiti.
Mkuu wa Mkoa ameitaja miradi inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea kuwa ina thamani ya shilingi bilioni moja ambapo miradi inayotekelezwa ni ujenzi wa Kituo cha Afya Kilagano na kituo cha afya Liganga kila kimoja kikiwa na thamani ya shilingi milioni 500.
Katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea ameitaja miradi inayotekelezwa kupitia tozo ya miamala ya simu kuwa ina thamani ya shilingi milioni 550.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni Kituo cha Afya Subira kinachogharimu shilingi milioni 500 na ukamilishaji wa vyumba vinne vya madarasa katika shule za sekondari Lizabon,Luwawasi na Lukala vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 37.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,miradi inayotekelezwa kupitia tozo ya miamala ya simu katika Halmashauri ya Tunduru inagharimu zaidi ya shilingi bilioni moja.
Hata hivyo amesema kati ya fedha hizo shilingi milioni 500 zinatekeleza ujenzi wa kituo cha afya Masonya na shilingi milioni 500 zinatekeleza mradi wa kituo cha afya Mchesi.
Miradi mingine inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo ni ukamilishaji wa maboma katika shule za sekondari Masonya na Mbesa kwa gharama ya shilingi milioni 25.
Imeandikwa na Albano Midelo,Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma Septemba 16,2022
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akiwa ofisini kwake mjini Songea
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...