Raisa Said,Mkinga
Wanafunzi 28,000 wa shule za msingi katika Wilaya za Handeni na Mkinga Mkoani Tanga, wanatarajia kunufaika na mpango wa kusaidia chakula mashuleni unaoratibiwa na mashirika yasiyo ya Kiserikali ya World Vision na Save the Children kwa muda wa miezi mitatu.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Kanali Maulid Surumbu wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika katika Wilaya ya Mkinga mkoani humo jana.
Surumbu amesema mpango huo utasaidia kupunguza utoro, tatizo la kuanguka mashuleni na kuuinua kiwango cha taaluma katika wilaya hizo mbili ambazo zimebainika kuwa na uhaba wa chakula.
Kanali Surumbu amesema Wilaya ya Mkinga ina shule 83 za msingi na kati ya hizo shule tatu pekee ndiyo zenye mpango huo wa chakula mashuleni na kwamba shule nyingine 80 hazina mpango huo hivyo mradi huo utakwenda kuleta tija endapo utatekelezwa vizuri.
“Nitoe rai kwa wazazi na walezi mradi huu ni wa miezi mitatu hivyo tujitahidi baada ya kumalizika na sisi tukawajibike kuwapatia chakula watoto wetu ili waweze kukua vizuri na kufanya vizuri katika masomo yao,” amesema.
Aidha, amewataka wataalamu wa kilimo kusaidia kuwashauri wananchi ili waweze kulima mazao kulingana na ikolojia ya eneo husika ili kupunguza uhaba wa chakula.
Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Kaskazini taisis ya World vision, Gilbert Kamanga amesema mradi huo umegharimu Sh 597 milioni ambapo vyakula vitakavyogawiwa katika Wilaya ya Mkinga ni kilo 70,697 za mahindi, maharage kilo 39,276, chumvi kilo 2,357 na mafuta ya kupikia lita 393 ambavyo vina thamani ya shilingi 216.43 milioni.
“Kwa upande wa Wilaya ya Handeni chakula kitagawiwa katika shule 24 ambapo jumla ya watoto 14,689 watanufaika na upatikanaji huu wa chakula mashueni ambapo watapata mahindi kilo 129,000, maharage kilo 53,000, chumvi kilo 3,600 na mafuta ya kupikia lita 9,000,” amesema Kamanga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...