BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC,) limeeleza kutambua jitihada zinazofanya na mradi wa ‘Mwanamke Imara’ unaotekelezwa na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA,) na kulenga kupunguza ukatili wa kijinsia kwa wanawake na vijana pamoja na kuwajengea uelewa katika shughuli za ujasiriamali na uchumi kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa semina maalumu iliyolenga kujenga uelewa na kubainisha ushiriki wa watanzania katika miradi ya kimkakati kwa wajasiriamali, vijana na wanawake iliyoikutanisha Baraza hilo, mradi wa Mwanamke Imara, vijana na wajasiriamali na kufanyika kwa njia ya mtandao Kaimu Katibu Mtendaji wa NEEC Isaac Dirangw amesema,suala la ajira kwa wanawake na vijana ni mtambuka na ushiriki wao katika miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini inaweza kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto hiyo.
Amesema ushiriki wa watanzania katika miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na wawekekezajii kutoka nje hasa katika sekta ya uziduaji (madini, mafuta na gesi,) bado ni mdogo na elimu zaidi inahitajika ili kuinua kiwango cha ushiriki kwa watanzania katika miradi hiyo.’’
‘’Tunatambua jitihada za Mwanamke Imara katika kutetea wanawake na vijana katika katika masuala ya kijinsia na kuwapa elimu ju ya fursa za uchumi, tupo pamoja na tutaendeleza ushirikiano ikiwemo kutekeleza majukumu ya kuratibu matamsha, warsha na shughuli zitakazowaleta pamoja wadau na kujadili fursa za kiuchumi kwa manufaa ya watanzania.’’ Amesema.
Akieleza manufaa ya watanzania kupitia fursa za miradi ya uwekezaji nchini Dirawang amesema, hadi sasa watanzania wapatao elfu 55 wameajiriwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo huku kampuni 1500 za ndani zimeshiriki katika kutoa huduma katika miradi ya maendeleo na kuhimiza elimu zaidi kwa watanzania ili waweze kunufaika na miradi mikubwa inayotekelezwa nchini.
Aidha aliwataka wadau hao kutupia macho sababu zinazopelekea wawekezaji kuagiza bidhaa nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa ubunifu, ushirikiano finyu wa wajasiriamali, ubora finyu wa bidhaa, mitaji midogo kwa wajasiriamali na kutozingatiwa kwa muda mambo yanayokwamisha pia watanzania wengi kukosa fursa za kushiriki katika miradi ya maendeleo.
Pia ameeleza kuwa baraza hilo litaendelea kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuratibu, kufuatilia shughuli za uwezeshaji kiuchumi na kuwawezesha watanzania vikiwemo vikundi mbalimbali vya ujasiiriamali pamoja na kuishauri Serikali na taasisi za Umma juu ya shughuli za uwezeshaji kiuchumi.
‘’Tutaendelea kuratibu ushiriki wa watanzania katika miradi hii ya kimaendeleo ili kuhakikisha idadi ya watanzania wanaonufaika na miradi hii mikubwa inayotekelezwa nchini na wawekezaji kutoka nje inaongezeka na hiyo ni pamoja na kuhakikisha huduma na manunuzi yote yanafanywa ndani ya nchi kwa manufaa ya watanzania na Taifa kwa ujumla.’’ Amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mradi wa Mwanamke Imara Mary Richard amesema mradi huo umelenga kupinga ukatili wa kila aina kwa wanawake na vijana kuanzia ngazi ya familia na katika ngazi za uongozi, maamuzi, umiliki wa mali na ushiriki katika shughuli za kiuchumi.
‘’Kujitegemea na umiliki wa fedha huepusha sana ukatili wa kijinsia kwa kuwa ni nguvu ya kiuchumi, TAWLA na NEEC sasa tutakuwa na mahusiano rasmi ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa elimu kwa watanzania juu ya kuzitumia fursa za miradi ya kimkakati na kuweza kunufaika na fursa hizo.’’ Amesema.
Kwa upande wake Wakili wa kujitegemea na Mhadhiri wa Cho Kikuu Tumani (Makumira,) Dkt. Elifuraha Laltaika amesema ushiriki wa watanzania katika miradi ya kimkakati hasa ya uziduaji (madini, mafuta na gesi) bado ni mdogo kutokana na uelewa mdogo wa fursa hizo licha ya sheria kuelekeza watanzania ni lazima wanufaike na fursa hizo.
Amesema mchakato wa kisera na elimu utasaidia katika kuongeza ushiriki wa watanzania katika miradi hiyo kupitia utoaji huduma ambapo kundi la wajasiriamali litanufaika zaidi pamoja na ajira kwa watanzania ambapo Taifa litanufaika kwa kupata teknolojia mpya mara baada ya miradi kukamilika, kukua kwa viwanda vya ndani pamoja na ushiriki wa mashirika na kampuni za ndani katika kutoa huduma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...