Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia upya Sheria za uwekezaji pamoja na biashara nchini ili kukabiliana na migogoro inayotokana na Sheria hizo.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati akizindua Chama cha Mawakili wa Serikali katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.

Aidha, Rais Samia amesema ni vyema Mawakili wa Serikali wawe makini na kuharakisha kusikiliza migogoro inayokinzana na Sheria za uwekezaji ili kupunguza kupelekana Mahakamani na wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa nchini.

Rais Samia amesema kufanya hivyo kutasaidia kupunguza kesi za uwekezaji, kulinda uwekezaji nchini na kupanua wigo wa kukuza uwekezaji, kukusanya mapato na hivyo kukuza uchumi kwa maslahi ya taifa.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka Mawakili wa Serikali kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu bila kukiuka haki za wananchi na kuwasaidia kutatua kero zao ambazo hazihitaji kufikishwa mahakamani.

Rais Samia pia ametoa wito kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu pamoja na Mawakili wote wa Serikali kuendelea kutoa elimu kwa umma hususan sheria zinazowagusa wananchi na kuwaelekeza taratibu za namna ya kupata haki zao.

Vile vile, Rais Samia amesema utoaji wa elimu utapunguza mrundikano wa mashauri ambayo hayana ulazima wa kufikishwa mahakamani kwa ajili ya utatuzi na hivyo pia kuchangia kupunguza mrundikano wa mahabusu.

Rais Samia amewataka Wakuu wa Mikoa kutumia Kamati za Ushauri wa Kisheria zilizoanzishwa katika ngazi zote za Mikoa na Wilaya nchini kupunguza malalamiko ya wananchi na mashauri dhidi ya Serikali.

Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kwenye laptop kuzindua mfumo rasmi wa Kieletroniki wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OAGMIS), nembo ya Ofisi hiyo pamoja na Chama cha Mawakili wa Serikali katika Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali uliofanyika leo Septemba 29,2022Jijini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi mbalimbali pamoja na Mawakili wa Serikali kabla ya kuzindua Chama cha Mawakili wa Serikali, nembo na Mfumo rasmi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika hafla iliyofanyika leo Septemba 29,2022 Jijini Dodoma.

 

Viongozi mbalimbali pamoja na Mawakili wa Serikali wakisikiliza hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (hayupo pichani) wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali pamoja na Mawakili wa Serikali kabla ya kuzindua Chama cha Mawakili wa Serikali, nembo na Mfumo rasmi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika hafla iliyofanyika leo Septemba 29,2022 Jijini Dodoma.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akitembelea mabanda mbalimbali likiwemo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kujionea shughuli mbalimbali pamoja na huduma zitolewazo na Ofisi hizo kabla ya kuhutubia na kuzindua Rasmi Chama cha Mawakili wa Serikali, nembo na Mfumo rasmi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...