Na Eva Ngowi, Dar es Salaam
Serikali
kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imepanga kupitia upya matumizi ya
Mfumo wa Stempu za Kielektroniki (ETS) baada ya watumiaji wa mfumo huo
kulalamika kuwa unagharama kubwa na kuwasababishia hasara kubwa huku
kukiwa na mifumo mingine inayofanya kazi kama hiyo lakini kwa gharama
nafuu.
Hayo yalisemwa Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru aliyeongoza jopo la
Wataalamu wa Wizara hiyo walipofanya ziara ya kikazi kutembelea viwanda
vya kutengeneza bia vya Tanzania Breweries Ltd na Serengeti Breweries
Ltd.
Bw. Mafuru alisema kuwa wakati wa ziara hiyo wamebaini kuwa
kuna mifumo inayofanyakazi zinazofanana lakini mfumo unaotumiwa na
Serikali kuzalisha stempu hizo za kieletroniki unagharama kubwa
ukilinganishwa na mfumo mwingine unaotumia teknolojia ya Block Chain
ambao hauna gharama kubwa.
“Tutawasiliana na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) ili watuambie sababu za kutoona kile ambacho sekta
binafsi inayotumia mfumo huo inakiona ili tuje na utatuzi wa
kuwapunguzia gharama wazalishaji wanazotumia kuendesha mfumo huo, fedha
ambazo zingekuwa sehemu ya mapato ya Serikali, alisema Bw. Mafuru.
“Kuna
mahali tumeambiwa kuwa wawekezaji hawa wanalipia Mfumo huo hadi
shilingi bilioni 22 kwa mwaka, ukichukua asilimia 30 ya sh. Bilioni 22
kwa mwaka ni karibu sh. Bilioni 6.6 hiyo ingekuwa ni kodi ambayo hivi
sasa hatuipati kwa sababu ni sehemu ya gharama ya kulipia Mfumo huo”
Alisema Bw. Mafuru
Alisema kuwa kuna hoja zilizoibuliwa na
viwanda hivyo tangu mwaka 2016 na kwamba zilihitaji kujibiwa ama
kutatuliwa na taasisi za Serikali na Wizara nyingine za kisekta ili
kuchochea uwekezaji nchini.
Bw. Mafuru alisema nia hasa ya
kufanya ziara hiyo ni kutimiza wajibu wa Wizara ya Fedha na Mipango
katika eneo la kusimamia uchumi kwani maendeleo ya nchi pamoja na uchumi
wake unategemea ushiriki wa sekta binafsi katika uzalishaji na utoaji
wa ajira kwa wananchi.
“Ziara hii imelenga kutuwezesha sisi
kuelewa kwanza changamoto ambazo wenzetu kwenye sekta hii hasa sekta ya
utengenezaji wa vinywaji, wanazipitia na kupata mrejesho kutoka kwao
kuhusu sera za hivi karibuni za kibajeti ambazo tumezipitisha kupitia
bajeti ya Serikali, Sheria ya fedha lakini pia utekelezaji wa ile blue
print, ambayo mwaka huu Serikali imetekeleza kwa kiwango kikubwa kupitia
marekebisho yaliyofanywa na Sheria ya Fedha ya 2022” alisema Bw. Mafuru
Alisema
kuwa Wizara yake inafanya hivyo ikiwa ni jitihada ya kupata mrejesho na
hatimaye waweze kujua mahali panapohitajika kuongeza jitihada,
kurekebisha mapungufu yanayojitokeza na pia kuangalia mahali
panapofanyika vizuri ili kuifungua uchumi wa nchi.
Aidha Bw.
Mafuru alisema kuwa jambo muhimu ambalo ameliona ni kwamba taasisi
nyingi za Serikali zinafanyakazi kivyake na kwamba zinahitajika juhudi
za pamoja za kuunganisha mipango yao na kushirikiana kiutendaji ambako
kutaongeza tija katika nchi.
Bw. Mafuru aliongeza kuwa ili
kuongeza uwekezaji nchini inapaswa kuwawekea wawekezaji mazingira rafiki
ya kuwa na uhakika kama mitaji yao iliyopo hapa Tanzania italindwa ili
waweze kuleta mitaji mingine.
“Makampuni yote mawili
tuliyoyatembelea leo yana mipango ya kuongeza uwekezaji wao nchini
lakini kuna kitu kinang’ang’ania kwenye mawazo ikiwemo kutokuwa na
uhakika kama mambo wanayoyalalamikia yamechukua miaka mitatu hadi minnne
kushughulikiwa na kutokuwa na uhakika wa kuongeza hatma yao” Aliongeza
Bw. Mafuru
Akizungumzia changamoto ya uhaba wa chupa za bia,
kunakochangia uzalishaji wa bia kuwa chini kutokana na kuwepo kwa
kiwanda kimoja pekee cha kuzalisha chupa hizo, Bw. Mafuru alisema Wizara
itaangalia masuala ya kisera ili kuongeza uzalishaji wa chupa hizo.
“Tutaongea
na Wenzetu wa Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji waweze kuangalia
namna ya kuongeza kasi ya kupata wawekezaji watakaoweza kuwekeza katika
eneo hilo kwa sababu kuna fursa na bahati nzuri fursa hii sio tu kwa
soko la Tanzania bali zitauzwa hata nchi Jirani na kutuwezesha kupata
fedha za kigeni. Alisema Bw. Mafuru
Kwa upande wake, Mkurugenzi
wa Masuala ya Ushirikiano wa Kampuni ya TBL Bi. Lucia Mwamboka, alisema
wana matumaini kwamba mazungumzo yaliyofanyika kati ya Timu ya Wizara ya
Fedha na Mipango yataleta tija na kwamba wako tayari kushirikiana na
Serikali ili kupanua wigo wa kodi.
Aliiomba Wizara kuyafanyiakazi
mapendekezo yao haraka iwezekanavyo na ikiwezekana ifikapo mwezi
Desemba Mwaka huu, majibu ya kupunguza gharama za uendeshaji wa Mfumo
huo wa Stempu za Kieletroniki unaosimamiwa na Serikali kupitia Mamlaka
ya Mapato Tanzania-TRA, yapatikane.
Naye Mkurugenzi wa Mahusiano
wa Kampuni ya Bia ya Serengeti, Bw. John Wanyancha alisema wamefarijika
kwa ujio wa viongozi kutoka Serikalini hususan Wizara ya Fedha na
Mipango kusikiliza malalamiko yao na kuona jinsi ya kuyafanyia kazi na
kuamini kuwa ziara ya Serikali kwenda kuwasilikiliza wawekezaji ni njia
nzuri ya kuleta mageuzi chanya katika maendeleo ya viwanda hapa nchini.
Alisema
kuwa Sekta hiyo ya uzalishaji wa vinywaji imekuwa kinara katika
uchangiaji kwenye eneo la kodi na Serikali itahakikisha inafanya
jitihada za kutatua changamoto zao ili waendelee kuchangia kwa sehemu
kubwa na waendelee kukua na kuongeza ajira na kuleta maendeleo ya
kiuchumi ambayo ndiyo matarajio ya Serikali.
Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru (katikati)
akimsikiliza Mkurugenzi wa Mahusiano Serengeti Breweries Ltd Bw. John
Wanyancha (kushoto), kulia ni Kamishna wa Sera Bw. Elijah Mwandumbya wa
Wizara ya Fedha na Mipango.
Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru (kulia )
Pamoja na timu ya Wizara ya Fedha na Mipango walipotembelea kiwanda cha
Tanzania Breweries Ltd. (TBL) kushoto ni Mkurugenzi wa Masuala ya
Ushirikiano TBL Bi. Lucia Mwamboka.
Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru akizungumza
na timu ya Tanzania Broweries Ltd. (hawamo pichani) wakati alipotembelea
kiwanda chao jijini Dar es Salaam
Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru akiwa kwenye
majadiliano na timu ya kiwanda cha bia cha Tanzania Breweries Ltd (TBL)
jijini Dar es Salaam. Kushoto ni timu ya Wizara ya Fedha na Mipango na
kulia ni timu ya TBL.
Kamishna
wa Madeni Bw. Japhet Justine asikiliza majadiliano kati ya Timu ya
Wizara ya Fedha na Timu Serengeti Breweries Ltd (hawamo pichani)
yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kiwanda cha bia cha Serengeti
Breweries jijini Dar es Salaam.
Kamishna
wa Sera Bw. Elijah Mwandumbya asikiliza majadiliano kati ya Timu ya
Wizara ya Fedha na Timu Tanzania Breweries Ltd (hawamo pichani)
yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kiwanda cha bia chaTBL jijini
Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...