Serikali imeamua kuyajenga
Masoko ya Mwanakwerekwe, Jumbi na Chuini kwa kupitia vikosi vya Idara
Maalum za SMZ ili kuwaondoshea usumbufu uliodumu kwa muda mrefu wananchi
wake.
Makamu wa pili wa Rasi wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman
Abulla ameyasema hayo wakati akiakhirisha mkutano wa Nane (8) wa baraza
la Kumi (10) la Wawakilishi Chukwani nje kidogo wa mji wa Zanzibar.
Amesema
kuwa Serikali imeamua kukabidhi Miradi ya ujenzi wa Masoko hayo kwa
Vikosi vya Idara Maalum za SMZ ambapo hapo awali walikabidhiwa
wakandarasi wazawa na kuonesha kusuasua kwa ujenzi huo kwa muda mrefu
jambo ambalo linawaletea usumbufu wananchi wake.
Mhe. Hemed
amesema kuwa Serikali imeamua kufanya hivyo ili kuboresha upatikanaji wa
huduma muhimu kwa wananchi wake ambapo Soko la Mwanakwerekwe litajengwa
na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU); Soko la Jumbi litajengwa na Chuo cha
Mafunzo na Soko la Chuini litajengwa na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi
(KZU).
Aidha, Mhe.Hemed amesema kuwa katika kuboresha sekta ya
miundombinu Serikali imeingia mkataba wa ujenzi wa barabara wa kilomita
Mia Moja nukta tisa (100.9) na kampuni ya China Civil Engineering
Corporation ( CCECC) ujenzi huo unaotarajiwa kuanza hivi karibuni
utachukua kipindi cha miezi Thelathini na sita (36) hadi kukamilika
kwake na utagharimu kiasi cha Dola za kimarekani Milioni Mia Moja na
kumi na sita (116).
Amesema, Ujenzi huo unahusisha Ujenzi wa
Barabara za Mjini kwa kiwango cha lami, zitakazokuwa na njia za waendao
kwa miguu, kuekwa taa za barabarani, misingi ya maji ya mvua pamoja na
bustani. Aidha, ujenzi huo utajumuisha na ujenzi wa barabara za juu
(fly over) katika eneo la makutano ya barabara za Amani na Mwanakwerekwe
kwa lengo la kuzifanya barabara hizo kuwa za kisasa na kuimarisha haiba
ya Mji wa Zanzibar, ili uendane na hadhi ya Miji ya Kitalii.
Mhe.
Hemed amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni miongoni mwa vipaumbele
vya Serikali ya Awamu ya Nane (8) inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt.
Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025 ibara ya 165, MKUZA III, Dira ya
Maendeleo ya Zanzibar (Vision 2050) pamoja na Mpango Kabambe wa
Usafirishaji wa Zanzibar (Zanzibar Transport Masterplan).
Sambamba
na hayo, Makamu wa Pili wa Rais amesema kuwa kupitia ripoti iliyotolewa
na Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonesha
kuwepo wa matumizi mabaya ya fedha za umma,Ufisadi, Rushwa, na Wizi kwa
baadhi ya watendaji hivyo, amewataka Viongozi wenye dhamana kuwasimamia
watendaji walio chini ya dhamana zao ili kuvidhibiti vitendo hivyo.
Mhe.
Hemed amesema kuwa Serikali haitakua na muhali wa aina yoyote kwa
mtendaji atakaebainika anafanya mambo kinyume na taratibu za nchi yetu,
hii itaambatana na hatua kali zitakazochukuliwa dhidi ya wale wote
watakaobainika kujihusisha na vitendo hivi na Serikali haitamuonea mtu
yeyote katika hili kwani uchunguzi wa kina utafanywa kuhakikisha haki
inatendeka.
Makamu wa Pili wa Rais amewataka watendaji wa
Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kuendelea
kufanya kazi zao kwa weledi ikiwemo kuipitia Ripoti ya Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) na kuangalia wale wote waliohusika na makosa
mbali mbali ya Rushwa na Uhujumu wa Uchumi ili kuweza kuchukuliwa hatua
kwa mujibu wa Sheria No. 1/2012 ya makosa ya uhujumu Uchumi Nchini kwani
makosa mengi ambayo yameripotiwa ni pamoja na kuomba na kupokea Rushwa
kinyume na Kifungu cha Thelathini na Sita (36), ubadhirifu wa mali na
mapato kinyume na Kifungu cha 42(1)(a), kutumia vibaya mali kinyume na
Kifungu cha 43, matumizi mabaya ya Ofisi kinyume na Kifungu cha 53,
kukwepa kulipa kodi kinyume na kifungu cha 44 na magendo kinyume na
Kifungu cha 45.
Pia Mhe. Hemed amewatoa hofu wananchi kwa kusema
kuwa ZAECA inafanyakazi zake kwa misingi ya Sheria, haki na uadilifu
na hakuna mtu yeyote atakaeonewa. “natoa wito kwa wananchi kuendelea
kutoa ushirikiano katika kuhakikisha ZAECA inatimiza majukumu yake
ipasavyo ili nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali iweze kurudi”
amesema
Sambamba na hayo, Makamu wa Pili wa Rais amesema kuwa
pato la nchi kwa kwa mwaka 2022 limeongezeka kwa asilimia (20.8%)
ukilinganisha 2020- 2021 ambapo nchi ilikubwa na janga la Uviko 19 hali
iliyosababisha uchumi wa dunia nzima kushuka, amesema kwa sasa Serikali
imeelekeza nguvu zake katika kuongeza makusanyo hususan kupitia vyanzo
vya mapato yasiyokua ya kodi sehemu ambayo Serikali ilikuwa haifanyi
vizuri kutokana na uvujaji mkubwa uliokuwa ukijitokeza kupitia
wafanyakazi wetu wasio waaminifu.
Amesema kuwa Serikali imeamua
kutumia mfumo wa makusanyo wa kielektroniki wa ZANMALIPO ili kupunguza
mianya ya uvujaji na kuongeza mapato ya nchi. Hivyo, Mhe. Hemed
amewaagiza watendaji wote wanaohusika na ukusanyaji wa mapato kutumia
mfumo huo na kuhakikisha unalindwa ipasavyo ili usiweze kuchezewa.
“Juhudi
maalum zitaelekezwa katika kuwabaini na kuwachukulia hatua kali za
kisheria wale wote watakaobainika kufanya vitendo vya wizi na ubadhirifu
wa mali za umma ikiwemo wataalamu wanaoichezea mifumo yetu, aidha, ni
jukumu letu sote kuhakikisha mapato yote yanakusanywa vizuri kwa
kushirikiana na mamlaka husika” amesema.
Akizungumzia kuongezeka
kwa watalii nchini Mhe. Hemed amesema kuwa kuna ongezeko la watalii
Laki Moja na Thelathini na Tatu, Mia Tano na Arobaini na Moja (133,541)
na kufikia watalii Laki Tatu Tisini na Nne, Mia Moja na Thamanini na
Tano (394,185) kwa mwaka 2021 kutoka watalii Laki Mbili na Sitini, Mia
Sita na Arobaini na Nne (260,644) kwa mwaka 2020. Amesema hii inatokana
na amani na utulivu iliopo nchini pamoja na utoaji wa huduma zilizo bora
na za haraka katika Viwanja vya Ndege, Bandari na Mahotelini.
Aidha,
ametoa wito kwa Uongozi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kusimamia
nidhamu, mila, silka, tamaduni na maadili ya nchi yetu kwa watalii wote
wanaoingia nchini. Sambamba na hilo, amewataka kuchukua hatua kali kwa
mtalii yeyote atakaekwenda kinyume na sheria na miongozo tuliyojiwekea
kwa maslahi mapana ya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar amesema kuwa serikali imeamua kuwaongezea mishahara wafanyakazi
wake ili kuimarisha utawala bora na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto
zote zilizojitokeza katika zoezi hilo na kusema kuwa kila mafanyakazi
atalipwa haki yake kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Mhe.Hemed
amesema kuwa baada ya Serikali kuongeza mishahara kumezuka
wafanyabiashara ambao si waaminifu na kuamua kuongeza bei za bidhaa kama
vile Mchele, Sukari na Unga wa ngano kinyume na sheria jambo ambalo
linaleta manung’uniko makubwa kwa wananchi hivyo ameiagiza Wizara ya
Biashara na Maendeleo ya Viwanda kuwachukulia hatua kali wafanyabiashara
hao kwa mujibu wa sheria.
Katika kuboresha upatikanaji wa
huduma ya Maji Safi na Salama Mhe. Hemed amesema kuwa Serikali
inatekeleza miradi mikubwa miwili ukiwemo mradi wa mkopo wa EXIM Bank wa
Milioni Tisiini na Mbili nukta Moja Nane (92.18) ambazo zimepangwa
kutumika kwa kumalizia uchimbaji wa Visima 64 matangi 15 na uungwaji wa
mabomba katika Shehia 36 kwa Mkoa wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Kusini
Unguja na hadi sasa ujenzi huo umeshafikia asilimia 62%.
Na
mradi mwengine ni ule wa ahuweni ya Uviko 19 ambapo ZAWA imetengewa
jumla ya shilingi Bilioni thelethini na Mbili nukta Mbili (32.2) ambazo
zinatumia kwa uchimbaji wa visima thelathini na Nane (38) kwa Unguja na
Pemba na kujumisha matengenezo ya visima 36 vya Ras el Khema na ujenzi
matangi 10 kwa Unguja na Pemba pamoja na matengenezo ya Mtangi matatu
(3) ya zamani.
Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema
kuwa miradi yote inayojengwa kwa kutumia fedha za Ahueni ya UVIKO 19
iko katika katua za mwisho kukamilika kwake pamoja na vifaa ambavyo
zinastahiki kuwemo kwenye miradi hio.
Akizungumzia huduma za
Afya Mhe. Hemed amesema Serikali imejipanga kuleta madaktari bingwa
kutoka pande mbali mbali za dunia kwa lengo la kuja kubadilishana uzoefu
na madaktari wetu ili wananchi wapate huduma bora na zinazokwenda na
wakati.
Amesema kuwa Serikali inaendelea kutoa huduma za afya
zilizo bora kwa wananchi wake na kukabiliana na maradhi mbali mbali ya
mripuko yanayojitokeza. “Nachukua fursa hii kuwaomba sana wananchi
wenzangu ambao bado hawajawapeleka watoto wao kupata chanjo kuhakikisha
wanawapeleka kupata huduma hiyo kwa kulinda Afya za watoto wao ambao
ndio taifa la kesho”.
Katika kuakhirisha kikao hicho jumla ya
Maswali ya Msingi Mia moja na Hamsini na Saba (157) na maswali ya
nyongeza Mia Tatu na Sitini (360) yaliulizwa na yalijibiwa na
Waheshimiwa Mawaziri. Pia katika mkutano huo jumla ya Miswada Miwili
(2) imejadiliwa na kupitishwa. Miswada yenyewe ni:-
I.
Mswada wa Kufuta Sheria ya Baraza la Wawakilishi (kinga, uwezo
na fursa), Namba 4 ya mwaka 2007 na kutungwa Sheria mpya ya Baraza la
Wawakilishi (kinga, uwezo na fursa) katika kutekeleza kazi na mambo
mengine yanayohusiana na hayo.
II. Mswada wa
Sheria ya Kuanzisha Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi wa
Kodi Zanzibar na mambo yanayohusiana na hayo. Kikao hicho cha Baraza la
wawakilishi kimehairishwa hadi Siku ya Jumatano tarehe 23 Novemba, 2022
saa 3.00 kamili asubuhi.
Makamu wa Pili wa RAis wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akikihairisha Mkutano wa 8 wa Baraza la 10 la Wawakilishi Chukwani jijini Zanzibar Leo tarehe 30.09.2022
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...