TAASISI ya Nyumba ya Watumishi Housing Investment(WHI) imeshauriwa kujikita kwenye maeneo ya Wilaya na Halmahauri mpya kwa ajili ya kusaidia makazi kwa watumishi wa Umma.
Ushauri huo umetolewa Septemba 27, 2022 jijini Dar es Salaam na Waziri Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama alipotembelea mradi wa WHI ulipo Magomeni Usalama jijini Dar es Salaam.
Amesema Miji yetu inaendelea kukua ua na kadri inavyokua watumishi wa umma wanapelekwa kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za halmashauri na wilaya mpya na maeneo mengine ikiwamo zahanati na hospitali, lakini uhaba wa nyumba kwa watumishi hawa bado ni mkubwa.
Hivyo amesema pamoja na miradi mizuri ambayo inafanywa na Taasisi hiyo kwenye majiji mbalimbali amewataka sasa mfike kwenye maeneo ya pembezoni ambako imekuwa ni changamoto kwa watumishi wetu kupata makazi mazuri.
“Kule tunaweka kufanya mambo mawili la kwanza kwenye Faida Fund tunaweza kuwahamasisha mamlaka ya serikaki za mitaa kwenye hizo mhalmahauri mpya na wilaya kujiunga na mfuko huu ninauhakika tunaweza kupata nafasi ya kuanza kujenga nyumba kwenye maeneo hayo mapya ya utawala,” amesema Mhagama.
Pia Waziri Mhagama ameiagiza WHI kurejea mpango wa kushirikiana na mamlaka nyingine kwa ajili ya kupeleka huduma bora kwa watumishi waliko vijijini huku akihimiza kuongeza gawio serikalini.
“Hatua hiyo itakuwa ni motisha kubwa kwa watumishi wetu walioko vijijini. Jambo jingine mnapotoa gawio kwa wawekezaji msisahau kutoa gawio serikalini kwani kadri mnavyofanya hivyo ndio mnapata pia mikopo ya ya kuweza kuendeleza miradi.
Ametoa mwito kwa maofisa utumishi wanaoshughulika na utawala utumishi wa umma kuwaunganisha watumishi na WHI ili wajue fursa ya makazi bora inapatikana ndani ya taasisi hiyo.
Kuhusu mradi huo wa Magomeni, Waziri Mhagama ametoa kipindi cha miezi sita kwa WHI kubadilisha matumizi ya sakafu ya kwanza(Floor ya kwanza) kutoka kuwa eneo la biashara hadi makazi.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa WHI, Paskali Massawe akizungumzia mradi huo wa magomeni amesema nyumba zote 88 zimenunuliwa na watumishi wa umma huku akiahidi kufanya ukarabati nyumba nane za floor ya kwanza zitakazo fanya jumla ya nyumba katika jengo hilo kuwa 96.
“Changamoto yetu imekuwa ni mtaji ambapo tumekuwa tukiendelea kuzungumza na wawekezaji kwa ajili ya kuongeza mtaji. Kwasasa tuna kitengo chetu cha ujenzi ambacho kimefika daraja la kwanza hatua itakayopunguza gharama za ujenzi na uuzaji wa nyumba zetu kwa ujumla."
Ameongeza kuwa wana malengo ya kuendelea kujenga nyumba kwenye halmashauri mpya ambapo halmashauri za Mbeya na Songea zimeonyesha nia ya kutaka kufanya kazi na taasisi yao huku akifafanua utafiti unaonesha nyumba zinazojengwa na kuuzwa na WHI zimekuwa na unafuu wa bei zaidi ya asilimia 10 kulinganisha nyumba nyingine.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Jenista Mhagama akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye mradi wa nyumba Magomeni nawakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Watumishi Housing Investment(WHI) jijini Dar es Salaam.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama akiwa sehemu ya juu ya wazi katika mradi wa nyumba Magomeni na Watendaji wa WHI wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya nyumba za kuwapangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma eneo la Magomeni Usalama jijini Dar es Salaam. (Picha na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)
Baadhi ya Watumishi wa WHI wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama(hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya nyumba za kuwapangisha na kuwauzia Watumishi wa Umma katika eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam.
Mwonekano wa Mradi wa nyumba wa Magomeni House unaomilikiwa na Watumishi Housing Investment(WHI) eneo la Magomeni Usalama jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...