SHIRIKA la Umeme Tanzania ( TANESCO,) limeeleza kuwa hatua za kutumia vyanzo mbadala vya uzalishaji wa umeme vimepunguza makali ya upatikanaji wa umeme nchini yaliyosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na kubeba athari nyingi ikiwemo upungufu wa vipindi vya mvua na kusababisha ukame.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi, Huduma kwa wateja wa TANESCO Martin Mwambene amesema katika kukabiliana na mabadiliko hayo na kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa wananchi wote, kuanzia mwaka jana Shirika hilo lilianza mikakati ya kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mseto vya nishati.
"Mpaka sasa mradi wa kituo cha Ubungo namba tatu chenye uwezo wa megawati 112 kinachozalisha umeme kwa gesi umekamilika.....Mradi wa Kinyerezi 1 extension ambao utaingiza jumla ya megawati 185 katika gridi ya Taifa unatarajiwa kukamilika hivi karibuni na kuimarisha zaidi huduma ya upatikanaji wa umeme" Amesema.
Aidha amesema mradi wa umeme unaotokana na nguvu za jua mkoani Shinyanga na Kishapu unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka 2023 kwa kuanza na megawati 50 kati 150 hali itakayoboresha zaidi upatikanaji wa umeme kwa watanzania.
"Ni dhahiri kuwa mipango hii isingeanza kutekelezwa pengine hali ya upatikanaji wa umeme ingekuwa mbaya zaidi tofauti na ilivyo sasa... baadhi ya maeneo kadhaa tuu kwa baadhi ya mikoa yataathirika katika nyakati tofauti, kupitia maofisa mawasiliano wetu nchi nzima tutaendelea kuwataarifu wateja wetu kwa wakati kadiri miradi hii itakapoaanza kuingiza umeme katika gridi." Amesema.
Pia Mwambene amesema Shirika hilo linaendelea kuongeza vyanzo vingine vya uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati jadidifu na tayari wameingia makubaliano na Kampuni ya Madsar ya Abudhabi, Dubai na watashirikiana katika kuwezesha miradi mbalimbali ya umeme jadidifu utakaofikia megawati 2000.
Hivi karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA,) ilitoa taarifa juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi na kueleza uwepo wa upungufu wa vipindi vya mvua na ukame hali iliyopelekea Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO,) kueleza mikakati iliyofanywa na hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa watanzania.
Kaimu Mkurugenzi, Huduma kwa wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO,) Martin Mwambene akizungumza na waandishi wa habari (hawamo pichani,) juu ya mipango na mikakati ya Shirika hilo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi katika uzalishaji wa umeme na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa uhakika, Leo jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...