Mkurugenzi wa Takwimu, Mifumo, utafiti na ufuatiliaji wa Shirika linaloshughulikia Afya ya Jamii Tanzania Management Development for Health (MDH) Dkt Lameck Machumi akizungumza na waandishi wa habarui jijini Dar es Salaam leo wakati wa maandalizi ya mkutano mkuu wa Afya unaotarajia kufanyika Oktoba 11, 2022 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere Dar es Salaam.


Baadhi ya wataalamu Mbalimbali wa Afya wakiwa kwenye Mkutano leo jijini Dar es Salaam.

Na Karama Kenyunko
MKURUGENZI wa Takwimu, Mifumo, utafiti na ufuatiliaji wa Shirika linaloshughulikia Afya ya Jamii Tanzania (MDH) Dkt. Lameck Machumi 
amesema asilimia 79.2 ya wajawazito waliofanyiwa utafiti wamegundulika kuwa na usugu wa dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi.

Amesema, wamama wajawazito ambao walikuwa wanatumia dawa halafu wakapata ujauzito walikuwa na idadi kubwa sana ya usugu wa dawa kuliko wale ambao waligundulika kuwa na VVU baada ya kupata ujauzito.

Akizungumza katika kongamano la afya leo Oktoba 6, 2022 jijini Dar es Salaam, Dkt Machumi amesema asilimia 26.5 ya wajawazito ambao wamegundulika kuwa na VVU baada ya ujauzito, wana usugu wa dawa hizo.

Amesema katika utafiti waliofanya Aprili hadi Septemba 2019, na ripoti yake kutolewa mwezi Mei mwaka huu ilibaini uwepo wa tatizo hilo.

Dk Machumi amesema kuwa usugu wa dawa kwa mjamzito husababisha kujifungua mtoto mwenye VVU kwa sababu virusi vinakuwa havijafubaa kama inavyotakiwa hivyo kushusha kinga za mwili.

Amesema kwa Tanzania mtu mwenye virusi chini ya 1,000 anakadiriwa kuwa amefubaza virusi lakini mgonjwa mwenye virusi zaidi ya 1,000 anakuwa hajafubaza virusi hivyo.

Ameeleza kuwa dawa zikitumika sana vijidudu vinatabia ya kujibadilisha na vinapojibadilisha vinatengeneza usugu hivyo, kama mgonjwa hajapimwa ataendelea kutumia dawa na kupata magonjwa nyemelezi.

"Usugu wa dawa huweza kusababisha mjamzito kujifungua mtoto mwenye VVU kwa sababu virusi vinakuwa havijafubaa. Hivi sasa maambukizi toka kwa mama kwenda kwa mtoto yameshuka kiasi kwamba mjamzito mwenye VVU ana uhakika wa kujifungua mtoto asiye na maambukizi kwa sababu ya matumizi ya dawa za kufubaza virusi." amesema Dk Machumi.

Pia amesema usugu wa dawa ni moja wapo ya tishio kwenye matibabu ya VVU kwa sababu mtu anameza dawa lakini hawezi kufubaza virusi kutokana na kuwa sugu kwake,’’ ameongeza.

Amefafanua kuwa Tanzania imefanikiwa kupunguza maambukizi ya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa asilimia 11 na katika Mikoa ya Dar es Salaam, Kagera,Tabora na Geita maambukizi ni chini ya asilimia mbili huku lengo likiwa kufikia asilimia moja.

Amesema kipo kipimo cha usugu wa dawa ambacho kinaweza kufanyika kwa wajawazito na waathirika wengine wa VVU mara kwa mara licha ya gharama zake kuwa juu.

"MDH imeandaa mkutano huu kwa ajili ya kujadiliana na wanasanyansi kuangalia jinsi gani kipimo cha usugu wa dawa za ARVs kinaweza kutumika kwa wagonjwa kwa sababu si kila mtu anaweza kumudu gharama za vipimo hivi na ndio maana tumeishirikisha Wizara ya Afya kuona namna ya kusaidia katika hili." amesema

Ameeleza kuwa upimaji wa usugu wa dawa utasaidia kupata hali halisi ya wagonjwa na dawa mbadala kwa ambao hazifanyi kazi yake ya kufubaza virusi.

Ameongeza kuwa uelewa kuhusu usugu wa dawa za ARVs ni mdogo licha ya kwamba watanzania wengi wanafahamu kuhusu usugu wa dawa za Malaria ikiwemo ASP.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...