· -Hatua hiyo inaipa uwezo benki kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wateja na kutekeleza mipango ya kukuza biashara.
Benki ya KCB Tanzania imeweka rekodi kwa kufikia mali zenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni moja hadi kufikia kipindi cha robo tatu ya mwaka 2022.
Rekodi hii imechangiwa zaidi na ongezeko la amana za wateja kwa asilimia 105 ndani ya kipindi cha miaka mitano huku faida ya benki ikiongezeka kwa asilimia 182 hadi bilioni 22.4 kwa kwa kipindi hicho.
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB, Bwana Cosmas Kimario alisema mafanikio hayo yametokana na mikakati ya benki kukuza huduma na kuimarika kwa mazingira ya biashara nchini.
Pia alisema sekta ya benki imeanza kuimarika tena baada ya kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na mlipuko wa Ugonjwa wa UVIKO-19 mwaka 2021.
“Biashara nyingi ziliweka mikakati ya kujipanua hasa baada ya adhari za UVIKO-19 na matunda yake yameanza kuonekana. Sisi pia imetusaidia kupata uzania imara zaidi (strong asset base) na kuwahudumia wateja wetu kwa karibu zaidi,”alisema.
Alisema sababu nyingine ni uwekezaji mkubwa ambao umefanyika katika kuimarisha uendeshaji wa benki hasa kutumia teknolojia ya kidigitali kufikisha huduma kwa wateja.
“Huduma kamaIntaneti Benki, Mobile Banking, na njia za malipo (POS) zimeendelea kuongeza ufanisi wa huduma kwa wateja wetu. Mpaka sasa asilimia kubwa ya miamala ya benki inafanyika nje ya matawi yetu jambo ambalo limeongeza ufanisi”.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni kuimarika kwa hali ya uchumi nchini kutokana na sera nzuri za serikali ya awamu ya sita na usimamizi na sera nzuri za Benki kuu ya Tanzania.
Aliongeza kuwa uwekezaji katika rasilimali watu ni chachu nyingine iliyosaidia kuleta mafanikio haya.
“Tumeendelea kuwekeza katika kuboresha na kukuza rasilimali watu ili kuongeza ufanisi lakini zaidi tumefanikiwa kupunguza gharama za uendeshaji hadi asilimia 49 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita,” alisema Bwana Kimario.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya KCB, Bwana John Ulanga alisema benki imeendelea kukua toka mwaka 1997 ilipoanzishwa.
“Benki ina mipango ya kujipanua zaidi ili kuweza kuwafikia watanzania wengi zaidi.Tuna mkakati wa kuongeza matawi matano ndani ya miaka miwili ijayo kwenye mikoa mbalimbali ambayo bado hatujaifikia,” alisema.
Aliongeza kuwa benki inaendelea kuangalia fursa ya kununua benki nyingine (acquisition) endapo zitajitokeza.
UKUAJI WA BENKI NDANI YA MIAKA MITANO
Akizungumzia ufanisi huo Mkurugenzi wa Fedha Bwana Willis Mbatia alisema:
· Utoaji wa mikopo umeongezeka kutoka bilioni 330 mwaka 2017 hadi Bilioni 623 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 88.
· Amana za Wateja zimeongezeka kutoka bilioni 318 mwaka 2017 hadi bilioni 646 mwaka huu sawa na ongezeko la asilimia 103
· Jumla ya Mali zimekua kutoka Bilioni 508 mwaka 2017 hadi kufikia trilioni 1.04 Septemba 2022 sawa na ongezeko la asilimia 105 na
· uwiano wa mikopo chechefu umeshuka kutoka asilimia 17.51 mwaka 2017 hadi asilimia 3.16 mwaka huu. Alisema banki inatarajia kupunguza mikopo chechefu hadi chini ya asilimia 3 kufikia mwisho wa mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB Tanzania, Cosmas Kimario akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutangaza mafanikio ya benki kufikia uzania wa mali wa trilioni moja.Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya KCB, John Ulanga na Willis Mbatia, Mkuu wa Fedha wa KCB (mwisho Kulia), Kaimu Mkuu wa Masoko, Uhusiano na Mawasiliano wa KCB, Shose Kombe (mwisho kushoto). Mafanikio hayo yanaipa benki hiyo nafasi ya kutanua wigo wa huduma hapa nchini
.Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya KCB, John Ulanga akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutangaza mafanikio ya benki kufikia uzania wa mali wa trilioni moja.Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa KCB, Cosmas Kimario na Mkuu wa Fedha, Willis Mbatia. Kaimu Mkuu wa Masoko, Uhusiano na Mawasiliano wa KCB, Shose Kombe (mwisho kushoto). Mafanikio hayo yanaipa benki hiyo nafasi ya kutanua wigo wa huduma hapa nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...