Na Rahima Mohamed Maelezo 31/10/2022
Mkurugenzi wa baraza la watu wenye ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe amewataka viongozi wa chama Cha Viziwi, kuhakikisha wanatoa mafunzo ya lugha ya alama kwa Viziwi na Jamii Ili kurahisisha Mawasiliano baina yao.
Debe alitoa wito huo wakati akifungua mkutano mkuu wa Uchaguzi chama cha Viziwi Zanzibar ( CHAVIZA) huko katika skuli ya Sekondari ya Dkt Ali Mohamed Shein Rahaleo Mjini Unguja.
Amesema watu wenye ulemavu wa uziwi wanakabiliwa na changamoto za kuwasiliana hivyo mafunzo yatakayotolewa yatarahisisha upatikanaji wa mahitaji yao ya kila siku.
Aidha amesema ni jukumu la viongozi hao kuhakikisha wanandaa mikakati madhubuti ambayo itawezesha upitikanaji wa mafunzo hayo ili jamii iwe na uelewa zaidi juu ya watu wenye ulemavu wa uziwi.
"Lengo la serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwahudumia wananchi wote ikiwemo watu wenye ulemavu nao wananufaika na fursa mbalimbali za kimaendeleo zinazotolewa na serikali yao" Amesema Mkurugenzi huyo.
Aidha amesema mabadiliko ya katiba ni jambo muhimu kwa sababu ndiyo maazimio ya wanachama na kuwataka viongozi wapya wajitahidi kukiendeleza Chama hicho kuhakikisha watu wenye ulemavu wa uziwi wanatambulika na kutetea haki za wanachama hao.
Mkurugenzi huyo amekipongeza Chama hicho kwa kukamilisha mchakato huo kwa kukutana kufanya mkutano mkuu ambao unatoa maamuzi makubwa katika jumuiya zao kutokana na jumuiya nyingi kushindwa kufikia hatua hiyo.
Akisoma ripoti ya Utekekelezaji Afua Nassour Hassan amesema Chaviza kimependekeza Wizara ya elimu itengeneze muongozo wa kufundishia lugha ya alama na jamii iendelee kuhamasishwa kujiendeleza kivitendo katika kujifunza lugha hiyo na kuifanyia kazi ipasavyo.
Aidha amelitaka Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu kushirikiana bega kwa bega na CHAVIZA pamoja na kuongeza wafanyakazi wa muda ili kurahisisha upatikanaji wa huduma endelevu kwa wanaofika ofisini hapo.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...