JIJI la Dar es Salaam limefikia asilimia 85 ya malengo kwa kutoa chanjo kwa wananchi 2,820,821 kati ya 3,310,079 ambao walilengwa kufikiwa na chanjo hiyo ambayo ni salama na muhimu dhidi ya virusi vya Korona ambavyo vimeenea ulimwenguni kote.

Hayo yameelezwa leo na Afisa Afya wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Enezael Ayo wakati wa mkutano wa majadiliano kuhusu chanjo ya Korona na jukumu la waandishi wa habari katika kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa chanjo hiyo uliowakutanisha wataalam wa afya na Chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC,) chini ya mradi wa ‘Boresha Habari’ unaofadhiliwa na shirika la Internews.

Amesema kati ya watu milioni 6 (kwa mujibu wa sensa ya 2012,) watu 2,820,821 wenye umri wa kuanzia miaka 18 wanaoishi katika Jiji hilo wamekamilisha chanjo dhidi ya virusi vya UVIKO-19.

‘’Baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuzindua rasmi zoezi la chanjo Agosti 30 mwaka jana Dar es Salaam tuliweka nguvu katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu na kupata chanjo…Tulianza na vituo vitatu hadi kufikia vituo 318 kwa sasa na hiyo ni kutokana na mwamko wa wananchi wa kuona umuhimu wa kupata chanjo.’’ Amesema.

Dkt. Enezael amesema, Jiji la Dar es Salaam lililenga kuwafikia wananchi 3,310,079 na hadi sasa wamefikia asilimia 85 na wanaendelea kuhamasisha jamii kupitia kampeni mbalimbali ikiwemo  huduma ya Mkoba ambayo wananchi hufikiwa na huduma hiyo katika makazi yao na kampeni hiyo ni sehemu ya uhamasishaji wa kufikia asilimia 75 ya utoaji chanjo kwa Taifa.

Amesema, makundi yaliyopewa kipaumbele katika upataji wa chanjo ya UVIKO-19 ni wazee kuanzia miaka 50 na kuendelea, watoa huduma za afya, wenye magonjwa sugu pamoja na kundi la vijana ambalo huambukiza na kuambukizwa virusi hivyo.

‘’Wananchi wanatakiwa kuelimishwa zaidi ili waweze kupata chanjo hii tunashukuru wadau wa maendeleo wakiwemo MDH, Benjamini Mkapa, wanahabari, wahudumu wa afya ngazi ya jamii na wenyeviti wa mitaa kwa uhamasishaji tuendelee kumalizia asilimia zilizobaki ili kufikia lengo.’’ Amesema.

Kuhusiana na homa ya Ebola iliyoibuka Nchi  jirani ya Uganda Dkt. Enazael amesema  utoaji elimu kwa Umma ni endelevu na licha ya kushuka kwa tahadhari wa ya maambukizi ya UVIKO-19 wameanza kurudisha tahadhari kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola kwa kuelekeza shule, ofisi za Umma, kaya, vituo vya afya na sehemu zote za mikusanyiko kuwa na sehemu za kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni.

‘’Kwa utafiti mdogo tulioufanya tahadhari zilizochukuliwa dhidi ya UVIKO-19 kwa kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni magonjwa ya minyoo na ya aina hiyo yamepungua…Tunaendelea na kuelimisha Umma kwa kuwa jiji la Dar es Salaam ni jiji la biashara mwingiliano ni mkubwa kupitia kituo kikuu cha mabasi cha Magufuli na Uwanja wa ndege.’’ Amesema.

Kwa upande wake mtaalam wa masuala ya afya Dkt. Christina Mdingi amesema chanjo ya UVIKO-19 ni salama na muhimu dhidi ya virusi hivyo na kuvitaka vyombo vya habari kusimama katika nafasi yao ya kuelimisha na kutoa taarifa sahihi kwa Umma wa watanzania ili waweze kupata chanjo.

Vilevile Mwenyekiti wa Chama cha Waandshi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC,) Samson Kamalamo ameishukuru Internews kwa kuratibu mafunzo hayo yaliyogusa sekta nyeti ya afya na kuwataka waandishi wa habari kuzingatia weledi pindi wanapoandaa na kuchakata maudhui kabla ya kuyafikisha kwa jamii.

Awali mwanahabari na Mjumbe wa kamati tendaji ya Jukwaa la Waandishi wa Habari Tanzania (TEF,) Neville Meena amewataka waandishi wa habari kuandika habari bila kupotosha pamoja na kusoma, kutafiti na kuchambua ili kutoa habari sahihi kwa Umma.

Afisa Afya wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Enezael Ayo akizungumza wakati wa mkutano huo na kuwataka wanahabari kuendelea kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu na usalama wa chanjo ya UVIKO-19.
Mwanahabari na Mjumbe wa kamati tendaji ya Jukwaa la Waandishi wa Habari Tanzania (TEF,) Neville Meena.


Mtaalam wa masuala ya afya Dkt. Christina Mdingi akitoa mada katika mkutano huo na kueleza kuwa chanjo ya UVIKO-19 ni salama na muhimu dhidi ya virusi hivyo na kuvitaka vyombo vya habari kusimama katika nafasi yao ya kuelimisha na kutoa taarifa sahihi kwa Umma wa watanzania ili waweze kupata chanjo.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...