Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu nchini (CVCPT), imeishauri serikali kuongeza wigo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ili kuwezesha wanafunzi wengi wanaohitaji kujiunga na vyuo vikuu kupata nafasi.
Ushauri huo ulitolewa leo Jumatano na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Yohana Mashalla, wakati wa mkutano wa 30 wa Kamati hiyo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Alisema idadi ya wanafunzi wanaomaliza shule za sekondari imekuwa kubwa hivyo kusababisha wanafunzi wengi kushindwa kujiunga na vyuo vikuu kutokana na hali ya umaskini kutoka kwenye familia zao.
Alisema miaka ya hivi karibuni serikali iliongeza idadi kubwa ya shule za msingi na sekondari na kutoa elimu bure hali inayosababisha ongezeko la wanafunzi wengi wanaomaliza shule ya msingi na kuhitaji kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali nchini.
“Vyuo vikuu navyo vitapata changamoto ya upungufu wa miundombinu hivyo kulazimika kuongeza idadi ya madarasa, maabara na maktaba ili kukidhi mahitaji ya idadi ya wanafunzi kwa hiyo bodi ya mikopo ipendekeze kwa serikali namna nzuri ya kuongeza wigo wa utoaji wa mikopo,” alisema Profesa Yohana.
Profesa Mashalla pia aliishauri serikali kuvisaidia kifedha vyuo vikuu nchini kupata uwezo wa kuweka miundombinu ya kuchukua idadi kubwa ya wanafunzi hali itakayosaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kwenye vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Naye Profesa Costa Mahalu ambaye ni Makamu Mkuu wa chuo cha Mtakatifu Augustine, alisema vyuo vikuu binafsi vinachangamoto nyingi kulinganisha na vyuo vya umma kwani vinajiendesha kwa kukusanya ada kutoka kwa wanafunzi.
Alisema idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo ya elimu ya juu ni ndogo na kwa wale wanaobahatika kupata wanapata asilimia ndogo hali inayovifanya vyuo hivyo kuishi maisha magumu kwani vinategemea zaidi ada katika kujiendesha kwake.
“Wanafunzi wanaopata mikopo wakiwa wachache sana inatusumbua sisi kwa kuwa inakuwa shida namna ya kuendesha vyuo bila wanafunzi na wanafunzi wengi wetu wanatoka kwenye familia ambazo haziko vizuri kifedha zinategemea zaidi mikopo ya bodi,” alisema Profesa Mahalu na kuongeza
“ Tusipopata wanafunzi wengi sisi wa vyuo binafsi huwa tunaathirika sana kwasababu hata mishahara ya kuwalipa watumishi inakuwa changamoto kubwa kwetu lakini wenzetu wa vyuo vya serikali hawana shida kwasababu mishahara yao yote inatoka serikalini,” alisema Profesa Mahalu.
Alisema kamati yao inahusisha vyuo binafsi na vya umma na lengo lao ni kuishauri serikali namna bora ya kuinua ubora wa elimu ya vyuo vikuu nchini.
Naye Profesa William Anangisye kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema lengo la vyuo vikuu ni kutoa wahitimu ambao watatatua changamoto mbalimbali kwenye jamii.
Alisema UDSM imekuwa ikipitia mitaala yake kila baada ya miaka mitano kuhakikisha chuo kinakuwa na mitaala bora ili kusaidia chuo hicho kupata wahitimu wenye ubora unaotakiwa na ambao watakidhi mahitaji ya soko.
“Mfano mwaka huu UDSM inapitia mitaala kwenye vitengo vyake vyote upitiaji wa mitaala ni muhimu na haukwepeki kwasababu mabadiliko katika jamii yetu yapo na kila jamii siyo jamii kwasababu kila siku inabadilika sasa ili iwe na lazima uwe na mitaala inayokwenda sanjari na mahitaji ya wakati huo,” alisema Profesa Anangisye
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu akizunumza wakati wa kikao cha Kamati ya Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu nchini (CVCPT), kilichofanyika jana katika ukumbi wa Tanzanite Milleinium.
Wajumbe wengine wa Kamati ya Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu nchini (CVCPT), wakisoma agenda za kikao hicho kilichofanyika jana katika ukumbi wa Tanzanite Milleinium jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu nchini (CVCPT), Profesa Yohana Mashalla, akizungumza wakati wa mkutano wa 30 wa Kamati hiyo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. Wengine ni wajumbe wa kamati hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...