Na Pamela Mollel,Arusha
Kamati ya kudumu ya Bunge ya kilimo,mifugo na maji imefanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya maji ya kuboresha huduma ya maji safi na usafi wa mazingira katika jiji la Arusha na Wilaya ya Arumeru
Katika ziara hiyo wabunge hao walibaini kuwa changamoto kubwa ya kukatika kwa umeme inapelekea miradi mikubwa ya maendeleo kukwama hali inayopelekea wananchi kukosa huduma ya maji kwa wakati
Akizungumza katika ziara hiyo mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya kilimo,mifugo na maji Dkt.Christine Ishengoma alisema kuwa umeme ukikatika inapelekea msukumo wa maji kuwa chini
"Baadhi ya maeneo ambayo miradi inatekelezwa ni wilaya ya arumeru (ASUWSDP) na mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (AUWSA),ukiwemo mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya sh.Bilioni 520"alisema Dkt Ishengoma
Alisema Wilaya ya Monduli hawana maji kutosha na wanampango wa kupeleka maji hadi huko kupitia mradi huo ili kutatua changamoto ya maji katika eneo hilo.
"Tunamshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutenga fedha nyingi za miradi ya maji ili watu waweze kupata maji safi na salama kila wakati nchini,"Alisema.
Nae Waziri wa maji Jumaa Aweso alisema wao kama wizara yenye dhamana wanaendelea kusimamia na kufatilia kwa ukaribu ili kuhakikisha adhma ya Rais Samia ya kumtua mwanamama ndoo kichwani inakamilika.
"Utekelezaji wa miradi ya maji inategemea na utoaji wa fedha,mradi huu hatukupata changamoto yoyote na sasa upo asilimia 96.62 ya ukamilishaji.
Ikiwa mahitaji ya maji kwa jiji la Arusha ni lita milioni 109,mradi una uwezo wa kuzalisha lita milioni 200 kwa siku hivyo maji haya ni toshelevu na yawafikie na maeneo mengine pamoja na wilaya Monduli ili kutatua changamoto ya maji katika maeneo yao.
Alisema mikakati ya wizara ni kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili uweze kutimiza adhma ya ifikapo 2025 kwa Arusha iwe imefikia asilimia 100 ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi hiyo muhandisi Dkt.Richard Masika ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ulinzi kwa miundombinu ya maji na pale wanapoona pana uharibifu basi watoe taarifa mapema ili waweze kufanya matengenezo yanayotakiwa.
Mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira AUWSA Justine Rujomba ametoa shukrani zake juu ya utendaji wa utekelezaji wa miradi ya maji na kuahidi kupokea maelekezo yote yaliyotowa na kuyafanyia kazi hasa lile la kufikisha maji katika maeneo yote ya pembezoni mwa miji na maeneo jirani yaliyopitiwa na mradi huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...