-Mashirika ya MAIPAC na CILAO yabaini maarifa ya asili


Na Mwandishi wetu, Arusha

Mabadiliko ya tabia nchi, yameua mifugo na wanyamapori zaidi ya 38,72 kwa kukosa maji na malisho, Wilaya ya Longido mkoa wa Arusha.

Afisa mifugo na mabadiliko ya tabia nchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Nestory Daqarro ameoa taarifa hiyo, katika mkutano wa uhakiki wa taarifa (validation meeting) ulioandaliwa na taasisi ya wanahabari ya usaidizi wa jamii za pembezoni (Media Aid For Indigenous and Pastoralist Community-MAIPAC) kwa udhamini wa shirika la maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP) kupitia mfuko wa mazingira duniani (GEF) na kuratibiwa na jumuiko la maliasili Tanzania (TNRF) kujadili umuhimu maarifa ya asili katika utunzwaji vyanzo vya maji, misitu na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Daqqaro amesema katika kipindi cha miezi tisa, wanyama takribani 38,720 wamekufa wakiwepo twiga wanne, pundamilia 18, swala wawili na wengine ni ng'ombe, kondoo na mbuzi .

"Jitihada zinaendelea kufanywa hapa wilayani ikiwepo kuchimba visima na kupeleka maji maeneo ya wanyama, kutenga malisho ili kuokoa maisha ya wanyama na uchumi wa wilaya hiyo, ambapo asilimia 95 ya wananchi hutegemea mifugo," amesema.

Mkurugenzi wa jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF), Zakaria Faustine akizungumza katika mkutano huo, amesema kuna haja kuwa na mkakati shirikishi baina ya asasi za kiraia, serikali, mashirika ya kimataifa na wananchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Faustine amesema mradi wa kukusanya maarifa ya asili yanayoweza kutumika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, kutunza misitu na maji ambao unatekelezwa na MAIPAC ni sehemu ya mkakati wa kupata taarifa ili kusaidia maboresho ya sera na sheria nchini.

"Tunawapongeza MAIPAC na CILAO kwa mradi huu, ambao unatekelezwa pamoja na miradi mingine 12 ya mazingira ambayo inafadhiliwa na UNDP kupitia programu ya miradi midogomidogo kwa lengo na kushirikisha jamii za asili katika utunzwaji wa mazingira na vyanzo vya maji," amesema.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kimokowa, wilaya ya Longido, Kilei Mollel amesema licha ya wilaya hiyo, kukabiliana na ukame na kukosa maji pia imeibuka mimea vamizi ambayo hailiwi na mifugo na wanyamapori ambayo imeota katika maeneo mengi.

"Tumekuwa tukishirikiana na serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kama CORDs kung'oa mimea lakini ni mingi zaidi ya hekari 1,000 za malisho zimevamiwa," amesema.

Mkurugenzi MAIPAC Mussa Juma na Mkurugenzi wa shirika la CILAO, Odero charles Odero, wameeleza katika mradi huo wamefika katika wilaya tatu za Monduli, Longido na Ngorongoro na kukutana na makundi ya wazee maarufu, viongozi wa mila, wanawake, vijana na wanafunzi na kukusanya maarifa za asili katika masuala ya mazingira.

Juma amesema jamii za pembezoni zina utajiri mkubwa wa maarifa ya asili lakini, kama yasipohifadhiwa yanaendelea kutoweka na hivyo, jamii kutegemea elimu za kisasa pekee katika utunzwaji wa mazingira.

Kwa upande wake Odero amefafanua kuwa, maarifa ya asili ambayo yatakusanywa katika mradi huo, yatawekwa katika vitabu na kwenye vyombo vya habari ili kutumika katika utungaji wa sera lakini pia kuelimisha jamii umuhimu wa maarifa hayo.

Afisa misitu wa tarafa ya Makuyuni na Manyara, Hapiness Masaki na Afisa misitu wa wakala wa misitu (TFS) wilaya ya Ngorongoro, Major Ngoilenya wamesema ni muhimu maarifa ya asili kutumika katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi katika kutunza vyanzo vya maji na misitu.

Mkurugenzi wa shirika la MIMUTIE women Orgganization (MWO) Rose Njilo akizungumza katika mkutano huo, licha ya kupongeza mradi wa kukusanya taarifa za maarifa ya asili unaotekelezwa na shirika la MAIPAC, amesema hivi sasa wanaoathirika na mabadiliko ya tabia nchi ni wanawake na watoto.

"Mradi huu umekuja wakati muafaka sasa elimu ya asili itambulike na watunga sera ili iweze kuwasaidia wanawake na watoto jamii za pembezoni ambao ndiyo waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabia nchi," amesema.

Afisa habari wa shirika la PINGOs Forums, Elie Chansa alitaka taarifa za asili ambazo zitakusanywa katika mradi huo, zifikishwe serikalini na katika mashule na vyuo ili ziweze kutumika katika kutunza mazingira kama walivyofanya mababu.

Mradi wa kukusanya taarifa za uhifadhi mazingira, kutunza vyanzo vya maji, misitu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, unatekelezwa na shirika la MAIPAC kwa kushirikiana na shirika la CILAO katika wilaya tatu za mkoa Arusha ambazo ni Longido, Monduli na Ngorongoro.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...