Na Baltazar Mashaka,Kahama
MWENYEKITI wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja amewapongeza viongozi wa ngazi mbalimbali nchini waliochaguliwa katika uchaguzi wa ndani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya wilaya.
Mgeja ambaye alikuwa mmoja wa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa CCM Wilaya ya Kahama,alitoa pongezi hizo jana katika eneo la Kinu cha Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (KACU) kilichopo Mhongolo,wilayani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotaka kupata maoni yake kuhusu mwenendo wa uchaguzi uliofanyika kote nchini kwa ngazi za wilaya, alisema binafsi kwa mtazamo wake ulikwenda vizuri,ameona umefanyika kwa haki,uhuru na kwa misingi ya demokrasia ndani ya Chama.
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wa Mkoa huo na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC),alisema viongozi waliochaguliwa na wajumbe wanastahili kupongezwa kwa ushindi.
“Binafsi nawapongeza viongozi mbalimbali nchini waliochaguliwa kuanzia nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa,Halmashauri Kuu ya Wilaya,Mkutano Mkuu wa Mkoa,Kamati za Siasa na Makatibu wa Itikadi na Uenezi, uchaguzi umekwisha kwa ngazi ya wilaya sasa wakafanye kazi kuhakikisha ilani ya uchaguzi ya CCM inatekelezwa ili kukirahisishia Chama uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025,”alisema Mgeja.
Aidha kwa heshima kubwa kwa viongozi wapya alisema baada ya uchaguzi ‘tugange yajayo’ hivyo kwa sasa wakaunganishe makundi ya wanachama waliowaunga mkono na ambao hawakuwaunga mkono na kuwa kitu kimoja kama ilivyokuwa awali kwa sababu CCM ni moja na ile ile.
“Kufanya hivyo wataonyesha ukomavu wa demokrasia na kisiasa, na kinachohitajika sasa baada ya uchaguzi ni umoja,upendo na mshikamano ndani ya Chama kwani waswahili wana usemi ‘Umoja ni nguvu na Utengano ni udhaifu’, hivyo tugange yajayo na yaliyopita si ndwele,”alisema.
Mgeja aliwatakia kheri viongozi wote walio chaguliwa nchini kwa nafasi mbalimbali kwa kipindi cha uongozi cha miaka mitano na kuahidi kuwa makada na wanachama wa CCM watawapa kila aina ya ushirikiano wanaouhitaji wenye
manufaa makubwa ya ujenzi wa Chama, KAZI IENDELEE.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...