Naibu Waziri wa Kilimo, Mh. Anthony Mavunde ameitaka Bodi ya Kahawa Tanzania kuweka mfumo madhubuti wa ufuatiliaji kwa wakulima wote wanaopewa miche bora ili iweze kuongeza tija na uzalishaji.
Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo jana tarehe 20 Oktoba, 2022 Wilayani Kyerwa alipokuwa akizindua zoezi la ugawaji wa miche bora ya kahawa 800,000 iliyozalishwa na kampuni ya JJAD na kugawiwa bure kwa wakulima kupitia serikali.
"Sisi kama Wizara, tumewapa Bodi ya Kahawa malengo ya kuzalisha miche ya milioni 20 kwa mwaka. Lengo hilo tumeliweka ili kuendana na malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025 ambayo imetuelekeza kufikia uzalishaji wa tani 300,000 za kahawa ifikapo 2025. Hivyo, ni lazima Bodi ya Kahawa kufuatilia miche hii tunayogawa kwa wakulima ili iwe na tija na kuongeza uzalishaji.
Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya usimamizi mahiri wa Waziri Mkuu wetu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ni kuona Mkulima wa kahawa ananufaika na kilimo anachokifanya na kuchangia katika upatikanaji wa ajira na kuongeza pato la nchi. Mfano mzuri wa hili, ni manufaa ya mfumo mpya wa kuuza kahawa kwa njia ya mnada mkoani Kagera, ambao umeleta ufanisi mkubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza bei na pato kwa mkulima.
Ndugu zangu wakulima, hakuna jambo la muhimu sana kwenu ambalo litarahisisha sana kwa Serikali na wadau wote kutoa huduma kwenu kama tukiwatambua. Hivyo, ninawaomba mtoe ushirikiano ili muweze kusajiliwa, mtambulike mpo wangapi ili muweze kupewa huduma stahiki kulingana na mahitaji yenu.
Naiagiza Bodi ya Kahawa kwa kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa kuhakikisha mnaandaa Mwongozo wa ugawaji wa miche kwa wakulima ambao utaonesha vigezo vya nani atagawiwa miche na kuainisha majukumu ya wadau wote wanaohusika katika zoezi la uzalishaji, ugawaji na usambazaji wa miche”Alisema Mavunde
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Mhe. Rashid Mwaimu alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ambazo zimepelekea kahawa katika msimu huu wa kahawa kuuzwa kwa mfumo wa minada, mfumo ambao umeleta tija kubwa na mapato kwa wakulima kutokana na kuongezeka kwa bei tofauti na ilivyokuwa katika utaratibu wa awali.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya JJAD, **Ndg.Albert Katagire **alieleza kuwa ana mkataba wa kuzalisha miche milioni 3 kutoka kwa Bodi ya Kahawa Tanzania, hivyo miche hiyo 800,000 iliyo tayari ni sehemu tu ya miche hiyo milioni 3 ambayo inatarajiwa kukamilika kuzalishwa ifikapo mwezi Februari, 2023.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...