Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma, John Mwanja akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa chuo hicho kwa Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Neema Mwakalyelye (kushoto), wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kukagua ujenzi wa chuocha VETA wilayani Ikungi mkoani hapa juzi. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro.



Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Neema Mwakalyelye (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Ikungi. Kutoka kulia waliosimama mbele ni ni Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Ikungi, Erick Nyoni, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida,Widege Mzalendo, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,Jerry Muro, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Mika Likapakapa na Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma, John Mwanja. Waliosimama nyuma kutoka kushoto ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ikungi (OCD) Suzana Kidiku na kushoto kwake ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Winfrida Funto.



Na Dotto Mwaibale, Singida


MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi nchini na kutoa fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyuo vipya na uboreshaji wa vyuo vya zamani.

Pongezi hizo zimetolewa juzi na Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma, John Mwanja mbele ya Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Neema Mwakalyelye kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa VETA wakati wa kikao na viongozi mbalimbali wa wilaya ya Ikungi cha kupata taarifa ya ujenzi wa chuo cha ufundi VETA kilichojengwa wilayani humo na VETA Kanda ya Kati-Dodoma kwa usimamizi wa TAKUKURU.

Aidha Mwanja alitoa shukurani hizo za dhati kwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Neema Mwakalyelye kwa usimamizi thabiti katika shughuli za serikali hivyo kuifanya serikali ya Awamu ya sita ing’are katika kuwaletea wananchi maendeleo yao.

Katika hatua nyingine Mwanja alitoa shukrani kwa uongozi wa chama na serikali wa Mkoa wa Singida na Wilaya ya Ikungi kwa ushirikiano wao mkubwa wanaowapa katika kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ikungi.

Akizungumzia faida ya chuo hicho mara kitakapokamilika alisema kinatarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 343,985 wa Wilaya ya Ikungi na wakazi wapatao 1,754,370 wa Mkoa wa Singida. Pia, wakazi wa mikoa jirani watanufaika na huduma za chuo.

Alisema katika utaoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwenye kozi za muda mrefu na kozi za muda mfupi, chuo hicho kitajielekeza katika kutoa mafunzo kwenye maeneo ya kimkakati kulingana na mahitaji ya shughuli za kiuchumi wanazofanya wananchi wa Wilaya ya Ikungi na Mkoa wa Singida kwa ujumla.

Alisema katika kutekeleza mradi huo VETA imekumbana na changamoto mbali mbali kama

kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi wakati wakiendelea na utekelezaji wa mradi, hali iliyopelekea pesa iliyotengwa kutokidhi mahitaji halisi ya mradi kutokana na bei za vifaa kupanda zaidi ya matarajio ya awali.

Alitaja changamoto nyingine waliyokumbana nayo ni uwezo mdogo wa kiuchumi wa mafundi waliowatumia hivyo kupelekea kushindwa kuwalipa vibarua wao kwa wakati na kupelekea baadhi yao kuacha kazi, hivyo kupelekea kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...