WAZIRI wa Ofisi ya Rais ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amevitaka vipaji vya wachezaji wa michezo mbalimbali kwenye michezo ya Sjhirkisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali, (SHIMIWI), viendelezwe na kutumika kwenye timu za taifa nchini.

Mhe. Mhagama ametoa kauli hiyo katika ufunguzi rasmi wa michezo ya SHIMIWI inayofanyika Jijini Tanga akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ambapo amesema watumishi wa umma wanaoshiriki kwenye michezo hii wameonesha vipaji vya juu ambavyo vitaweza kusaidia taifa na timu mbalimbali za hapa nchini. SHIMIWI inashirikisha michezo ya soka, netiboli, kuvuta kamba, mbio za baiskeli, raidha, karata, bao, draft na vishale (darts).

“Hakuna sababu ya kwenda nje ya nchi kutafuta wachezaji kwani hata kina Mayele na Leta Mzungu unaweza kuwakuta ndani ya Ofisi ya Rais Ikulu na Madini, na wamo wengi sana humu humu kwenye timu zetu zinazoshiriki SHIMIWI, hivyo vipaji vyao viendelezwe zaidi,” amesema Mhe. Mhagama

Amesema SHIMIWI inaendelea kukua kwa kushirikisha timu nyingi kutoka kwenye wizara, Idara, Wakala za serikali na Ofisi za Wakuu wa mikoa na atahakikisha anapeleka salamu serikalini ili mikoa yote ishiriki kwenye michezo hii, tofauti na mwaka huu imeshiriki mikoa 18 pekee.

Halikadhalika Mhe. Mhagama amesema baada ya timu za SHIMIWI kuendelea kuwa bora na wabobezi zitaweza kushindana na timu za serikali za nchi nyingine kwenye michezo makubwa ya umoja wa Afrika Mashariki, ili kujenga urafiki.

Pia amelitaka shirikisho hilo kuhakikisha watumishi wenye mahitaji maalumu wanashiriki kikamilifu kwenye michezo ijayo.

"Napenda kuwahamasisha Watumishi wa Umma wenye mahitaji maalum kushiriki michezo hii, mwakani na idadi ya Watumishi iongezeke zaidi na kuongeza baadhi ya michezo ambayo haipo kwa sasa kama kabadi ili washiriki kikamilifu haki hii ya msingi," amesema Mhe. Mhagama.

Mhe. Mhagama amewagiza waajiri wote nchini kuhakikisha wanamichezo wanawezeshwa vyema kushiriki michezo hiyo, huku akitaka wanamichezo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za michezo pamoja na Utumishi wa Umma.

Katika Hatua nyingine Mhe.Mhagama amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma, ikiwemo upandaji wa madaraja, ubadilishaji wa kada na kufuta tozo ya thamani ya Mkopo wa Elimu ya Juu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa SHIMIWI, Daniel Mwalusamba amesema shirikisho linakabiliwa na changamoto la kukosa utaratibu wa kushiriki kwenye mazoezi, ambapo ameomba uwekwe utaratibu ili waweze kushiriki kwa wingi.

Amesema malengo ya SHIMIWI ni kujenga umoja wa kitaifa, kujenga ushindani wa kimichezo kati ya watumishi na taasisi zake, kujenga afya ya kimwili na akili na kujenga ukakamavu na moyo wa ushindani na kuwafanya watumishi kuwa na mahusiano mazuri na kufahamiana.

Mwalusamba amesema michezo ya mwaka huu imeshirikisha wanamichezo 2510 wanashiriki kwenye michezo hiyo, kutoka kwenye timu timu 63 kutoka Wizara 27, Mikoa 18, Idara za Serikali 18 zinashiriki michezo hiyo iliyobeba Kauli mbiu "Michezo hupunguza magonjwa yasiyoambukiza na kuongeza tija mahala pa kazi, Kazi Iendelee".


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...