WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula ameonya Wataalamu wa Taaluma ya Uthamini nchini kuacha na tabia zinazo dhalilisha taaluma ikiwemo ukosefu wa uadilifu katika suala zima la kuongeza ukadiliaji thamani usiozingatia uhalisia.

Dkt Mabula amesema kuna baadhi ya Wathamini kwa kushirikiana na wahusika kama vile walipa fidia, wananchi wenye mali, maafisa wa taasisi za fedha zinazotoa mikopo kwa uthamini wa mali za rehani, kuongeza au kupunguza thamani tofauti na uhalisia ili kutoa unafuu kwa upande husika jambo ambalo amesema lina athari kwa mapato ya serikali na kuitaka Bodi ya Wathamini kuwachukulia hatua pindi watakapobainika.

Aidha Dkt Mabula ameangazia pia suala la kuandikia na kujumuisha kwenye taarifa za fidia mali “hewa” yaani mali ambazo hazipo uwandani na wakati mwingine kuondoa na kutojumuisha kwenye taarifa ya fidia baadhi ya mali zilizopo uwandani katika taarifa ili kukidhi matakwa ya mteja wake anayetaka, hata kwa kutumia rushwa, unafuu wa fidia katika eneo husika.

Dkt. Mabula ameyasema hayo leo Oktoba 20, 2022 wakati akitoa hotuba ya ufunguzi kwa Wathamini mali katika Mkutano Mkuu wa tatu wa Wathamini unaoendelea kwa siku mbili jijini , Arusha.

‘’Vitendo vya aina hii vinaichafua taaluma hii, hivyo, naitaka Bodi kuchukua hatua kali zaidi kwa Wathamini watakaobainika na Makampuni yatakayojihusisha na vitendo vya aina hii, kwenye swala hili, naomba Bodi yako iwachukulie hatua wathamini wote bila kujali kama ni wa Serikali au wa kutoka sekta binafsi, kwa kuwa wote ni taaluma moja na sheria haingalii sekta binafsi wala mwajiliwa serikalini’’Aliongeza Dkt Angeline Mabula.

Dkt Mabula amemtaka Mwenyekili wa Bodi ya Wathamini kutoa taarifa kwa serikali ikiwa mthamini mhusika ni wa Serikali, ili Wizara iangalie namna ya kuchukua hatua stahiki kwa mtumishi kulingana na sheria za ajira ya Serikali.



Waziri Mabura ameiagiza Bodi ya taaluma hiyo kuwa, yale watakayoweza kuyafanyia kazi kupitia Mkutano huo, wayatekeleze kwa maarifa yao na juhudi zao zote, na yale ambayo yatahitaji muda waweke mikakati mipya ya kuyatekeleza.



Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi amewataka wathamini hao kuangalia namna bora ya kutoa maoni ili Wizara yake iweze kufanya maboresho katika sheria ya wathamini ili serikali iweze kukuza uchumi kutokana na taaluma hiyo.



Aidha Dkt. Kijazi amewataka wataalamu hao kuangalia kutoa mrejesho wa namna bora ya kuboresha mahusiano kiutendaji kazi kutokana na kuwepo mkanganyiko wa kimtizamo na kiutendaji unaotokana na tofauti zao katika ajira hususani kati ya waajiriwa serikalini na sekta binafsi.



‘’Tungependa kama Wizara kuona mkiboresha uhusiano kati ya sekta ya umma na sekta na kwamba mna mawasiliano ya mara kwa mara binafsi pia naelewa kumekuwepo na mitizamo binafsi nyingine chanya na nyingine hasi hivyo kuboresha uhusiano katika utendaji kazi kutasaidia kuwahudumia watanzania vizuri Zaidi kuliko ilivyo wakati huu’’. Alisema Dkt. Kijazi.



Mkutano wa tatu wa Mwaka wa taaluma ya Wathamini Pamoja na mambo mengine umepokea wanataaluma wapya 53 ambao wamesajiliwa na bodi ya taaluma ya wathamini baada ya kuwa wameshinda mitihani ya bodi hiyo na kusajiliwa na bodi hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...