Na Muhidin Amri-Namtumbo
ASKARI wanyamapori wa vijiji (VGS)37,wamehitimu mafunzo maalum ya kozi namba 18/2022 katika chuo cha mafunzo ya Uhifadhi Maliasili kwa Jamii Likuyusekamaganga wilaya ya Namtumbo mkoni Ruvuma.
Akitoa taarifa ya mafunzo hayo,Mkuu wa chuo hicho Jane Nyau alisema,askari hao wamepata mafunzo maalum ya mbinu za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ikiwa ni utekelezaji wa mkakati huo.
Alisema,mafunzo hayo yametolewa kwa muda wa wiki mbili chini ya ufadhili wa Mamlaka ya usimamizi Wanyamapori Tanzania(Tawa)na wahitimu hao wametoka katika wilaya na mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
Nyau alisema,askari hao wamejifunza mbinu ambazo ni rahisi kuzitumia katika mazingira yao ya kawaida ambazo hazitumii gharama kubwa kiuendeshaji na zinawapatia faida nyingine mbadala.
Alitaja baadhi ya faida hizo ni kutumia mizinga ya nyuki ambayo mbali na kudhibiti wanyamapori hasa Tembo,lakini wananchi watanufaika kwenye kilimo kwani nyuki hao huhusika katika uchavushaji wa maua na hivyo kuongeza mazao kwa wakulima,wananchi kupata chakula ikiwamo asali na nta.
Alisema,matarajio ya chuo kwamba askari hao watakaporejea kwenye maeneo yao watakwenda kupunguza migogoro kati ya wanyamapori na binadamu kwa kushiriki moja kwa moja kuwadhibiti na kutoa elimu kwa jamii kuhusu mbinu walizofundishwa ili waweze kuzitumia kutatua changamoto hizo.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mamlaka ya udhibiti wa wanyamapori Tanzania(Tawa)Kamishina msaidizi Said Mshana alisema, kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Tawa imepanga kuchimba mabwawa 50 ya maji katika Hifadhi mbalimbali za Taifa.
Alisema,mpango wa kuchimba mabwawa hayo ni mkakati wa kudhibiti na kupunguza mtawanyiko wa wanyamapori wakali na waharibifu kwenda nje ya maeneo yao.
Alisema mkakati mwingine ni kuongeza doria za udhibiti wanyamapori pori wakali na waharibifu,ambapo jumla ya doria 64,724 zimefanyika katika kipindi cha Julai hadi Juni 2022 na kujenga vituo 16 vya kudumu vya askari wa kudhibiti matukio ya wanyamapori katika wilaya 16 hapa nchini.
Mshana alisema, hatua hizo na nyingine zilizopangwa kutekelezwa naTawa zitasaidia kupunguza changamoto ya mara kwa mara inayotokea ya wanyama hao kutoka kwenye hifadhi kwenda kwenye makazi ya watu na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazao mashambani.
Kwa mujibu wa Mshana,matukio ya migongano kati ya wanyamapori na wananchi yanayoongezeka kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na binadamu kuendesha shughuli zao kwenye mapito na mtawanyiko,na hivyo kupelekea ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Kamishina Mshana,amewakumbusha wananchi wanaokaa jirani na maeneo ya hifadhi,kutofanya shughuli zozote za kibinadamu katika maeneo hayo,ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Mkuu wa wilaya ya Nantumbo Dkt Julius Ningu,ameipongeza Tawa kwa kuchukua hatua madhubuti katika kudhibiti matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu ambao wanatishia maisha na mali za wananchi.
Alisema,hatua hizo pamoja na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mkakati wa Kitaifa wa kusimamia utatuzi wa migogoro baina ya watu na wanyamapori wa mwaka 2020-2024.
Alisema,mkakati huo unaohusisha wadau mbalimbali ikiwamo taasisi za uhifadhi,NGO’s na Halmashauri za wilaya utawezesha kupunguza migogoro na muingiliano kati ya wanyapori na binadamu.
Amewapongeza wahitimu kwa uvumilivu walioonyesha katika kipindi chote cha mafunzo na kueleza kuwa,mafunzo waliyoyapata yamewajengea utimamu wa mwili na kuwapatia mbinu za udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu.
Katika risala yao iliyosomwa na Nassoro Ndengwike wahitimu hao walisema, katika kipindi cha mafunzo wamefundishwa mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu,uhifadhi wa maliasili zilizopo katika hifadhi za Taifa,sheria za uhifadhi,fidia na vifuta jasho.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt
Julius Ningu akiangalia mtaro ambao unaweza kutumika kudhibiti
wanyamapori wakali na waharibifu kabla ya kufunga mafunzo maalum ya kozi
kwa askari wanyamapori 37 wa vijiji katika Chuo cha mafunzo ya ya
Uhifadhi wa Maliasili kwa jamii Likuyu Sekamaganga,kushoto kwake ni Mkuu
wa chuo hicho Jane Nyau.
Mhitimu wa mafunzo maalum kozi
namba 18/2022 ya Askari wanyamapori wa vijiji Nassoro
Ndengwike,akimuonesha Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt Julius Ningu
aliyevaa suti namna waya uliounganishwa na mizinga ya nyuki unavyoweza
kusaidia kufukuza wanyamapori wakali na waharibifu kuingia kwenye makazi
ya watu,katikati Mkuu wa chuo cha mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa
jamii Likuyu sekamaganga na kulia Kamishina msaidizi wa Tawa Said
Mshana.
Askari wanyapori(VGS) Sisemi
Kapimila kushoto akionesha tofali lililotengenezwa kwa pilipili na
kinyeshi cha Tembo linavyoweza kusaidia katika kudhibiti wanyamapori
wakali na waharibifu.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt
Julius Ningu kushoto,akimsikiliza Askari wa wanyampori wa vijiji
Jonathan Lweikiza akipiga ngoma ambayo inatumika kwa ajili ya kufukuza
wanyamapori wakali na waharibifu wanaovamia kwenye makazi ya watu na
kuharibu mazao mashambani.
Mkufunzi wa mafunzo maalum
namba 18/2022 ya Askari wanyamapori wa vijiji kutoka chuo cha mafunzo ya
Uhifadhi wa maliasili kwa jamii Likuyusekamaganga Kabadi Manyonyi
akieleza kuhusu mafunzo kwa vitendo yaliyofanywa na wahitimu wa mafunzo
hayo kwa mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt Julius Ningu aliyevaa suti,wa
kwanza kushoto Mkuu wa chuo hicho Jane Nyau.
Mhitimu wa mafunzo maalum kozi
namba 18/2022 Boniface Samson akipokea cheti cha kuhitimu mafunzo hayo
katika chuo cha mafunzo ya uhifadhi wa maliasili kwa jamii
Likuyusekamaganga kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt Julius
Ningu,katikati Mkuu wa chuo Jane Nyau.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...