BADO kuna changamoto kubwa kwa wasichana ya  kutembea umbali mrefu kwenda shule,hali inayochangia kupata  hatari ya matukio ya ukatili wa kijinsia katika kundi hilo na kupelekea kupoteza ndoto zao.




Asilimia kubwa ya changamoto hiyo inawasababisha wasichana wengi kushindwa kufikia ndoto zao na kuongeza  mimba za utotoni kutokana na wasichana kutembea umbali mrefu kurudi na kwenda shuleni kurubuniwa na wanaume.


Wasichana wamekuwa wakikubwa na madhira mbalimbali ikiwemo Mimba za utotoni,uchelewaji wa masomo shuleni kutokana na umbali kati ya shule na nyumbani hivyo kusababisha kukosa masoma kwa wakati.


Watoto wa kike ndio wahanga wakubwa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali katika kupata elimu bora, changamoto hizo muda mwingine huvuruga mfumo mzima wa maisha ya watoto wa kike na kusababisha  kushindwa kutimiza zao.

 

Licha ya vikwazo wanavyopitia katika kupata elimu bora, wasichana wamekua wakipitia matukio ya  ukatili wa kijinsia kama vile kubakwa,kuozeshwa katika umri mdogo, mimba za utotoni ambazo baadhi zimekua zikisababishwa  na kutembea umbali wakati wa kuelekea na kurudi kutoka  shule hasa kwa wasichana wanaosoma shule za umma za Msingi na Sekondari. 


Ripoti mbalimbali zinaonyesha shule nyingi za sekondari zilizopo maeneo ya Vijijini huwaladhimu wasichana kutembea umbali kuanzia  km nne hadi 10 kwenda na kurudi kutoka shule ambapo husababisha wasichana kukutana na matukio hayo ya ukatili wanapokuwa njiani.


Kwa Mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi),kuna ongezeko la asilimia 57 la  wanafunzi wa Sekondari walioacha shule mwaka 2019 hadi kufikia wasichana 5,398 ukilinganisha na 3,439 kwa mwaka 2015.


Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu,ustawi wa jamii na mashirika ya kitaifa na kimataifa yamekuwa yakipiga kelele juu ya kutafuta njia ya kupunguza hali ya wasichana kutopata unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo kupata mimba za utotoni.


Kupitia changamoto hizo wanazokutana nazo wasichana, Shirika la Msichana Initiative kupitia mradi wake wa Baiskeli Moja kwa Msichana Mmoja limeendelea kugusa wasichana wenye changamoto hizo na wameweza kuwafikia wasichana 100 kwa shule ya Sekondari Sejeli na Banyibanyi zilizopo Wilaya ya Kongwa Dodoma pamoja na Shule ya Sekondari Zinga  na Mapinga.



 

Katika zoezi la ugawaji Baiskeli lilofanyika katika mikoa ya Dodoma na Mkoa wa Pwani (Bagamoyo),Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi ameendelea kuwasisitiza wanafunzi kujiamini na kujitambua.


Anasema pamoja na kuwapatia baskeli  lazima msichana mwenyewe uwe na ndoto na uwe thabiti katika kuhakikisha unafikia ndoto zako.

''Unataka kuwa nani kwasababu tunaweza tukakupa kifaa lakini kama haujiamini, haujitambui utarubuniwa tu bado yaani lazima ujitambue mimi ni nani nataka nini na haya maisha ili hata ukikutana na bodaboda una baiskeli hauna baiskeli utamwangalia tu machoni utamwambia mimi nasoma niache nisome’’ Anasema  Gyumi.


Gyumi anasema Msichana Initiative imekua ikitekeleza mradi wa “BAISKELI MOJA, MSICHANA MMOJA’’(ONE GIRL ONE BIKE) toka mwaka 2017, wenye lengo la kusaidia wasichana wanaotembea umbali zaidi ya kilomita 10 kwenda na kurudi kutoka shule.


Anasema mradi huu unalengo la kusaidia kutatua changamoto hii ukilenga kupunguza hatari ya matukio ya ukatili kwa wasichana. ''Kama Shirika mpaka sasa tumefanikiwa kugawa jumla ya Baiskeli 448 tangu kuanza kwa mradi huu mwaka 2017,  tunawashukuru sana washirika wetu (Karimjee Jivanjee Foundation, Partners For Equity, MY ILAVA, InfoBip na Watanzania wa kawaida ambao wamekua wakijitoa kwa hali na mali katika kuwasaidia wasichana wa Tanzania kwenye kufikia ndoto zao za kielimu,''anasema 


Aidha anasema mradi huo wa Baiskeli Moja kwa Msichana Mmoja unaendelee kuwainua wasichana wanaotembea umbali zaidi ya km 10 kwenda na kurudi kutoka shule ili waweze kuepukana na  matukio ya ukatili na  wafike shule kwa wakati.


* Wakizungumzia Mafanikio ya mradi huo.


Mwalimu kutoka  Shule ya  Zinga,Sofia Msefu anasema kutokana na mradi huo umeweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa  wasichana hao kutoka kwenye hatari za kukutwa na matukio ya ukatili yanayotokea barabarani wakati wanapoenda au kurudi kutoka shule.


“Napenda kuwashukuru Shirika la Msichana Initiative kwa msaada huu wa Baiskeli, unatija kubwa kwa wanafunzi wetu kutokana na  asilimia kubwa ya wanafunzi wanatoka mbali, kupitia hizi baiskeli tunaamini utoro utapungua na wanafunzi wengi watafaulu,''anasema.


Anasema  katika shule yao  kitu hiki hakijawahi kutokea isipokuwa kupitia mradi huo wa Baiskeli Moja kwa Msichana Mmoja umeweza kuwasaidia kutimiza ndoto za wasichana wengi.

 

Naye Mzazi wa mnufaika wa mradi huu kutokaJosin Salum ,anaishukuru taasisi hiyo ya msichana initiative kupitia mradi wake huo kwa kumsaidia mtoto wake pindi anapoenda shule na kurudi nyumbani. 


‘’Binafsi kama mzazi nimefurahi sana kwa ajili ya hili shirika kuweza kwa ajili ya kuweza kutuwezeshea watoto wetu kupata usafiri wa Baiskeli maana walikuwa wanapitia  na changamoto nyingi sana kwa kutoka mbali kwasababu hata mwanzo mtoto wangu hakupendezewa kuja kusoma shule hii kwa sababu ya umbali lakini kuanzia leo hii naanza kuona nuru kwa binti yangu, Mungu awabariki sana, ’’ anasema 


Vivian Milonge Mwanafunzi  kutoka Shule ya Sekondari Zinga-Bagamoyo,anasema kabla hajapokea baiskeli hiyo alikua akipata lifti kutoka kwa madereva pikipiki''bodaboda'' mbalimbali ambapo ilikua ni ngumu kukataa kwasababu alikuwa akihitaji kufika shule mapema. 


''Nina furaha kwasababu nitawahi shuleni na kurudi nyumbani shule kwa wakati hivyo nawashukuru sana Msichana Inititiative na wafadhili wote kwa kutuwezesha kupitia mradi huu,pia tunawashukuru watanzania wote ambao mmekua mkijitoa kupitia mradi huu, kwenye kutuwezesha sisi wasichana kufikia ndoto zetu  za kielimu kwa kuchangia baiskeli moja  au zaidi,''anasema 


Mwanafunzi Amina Suleiman  anasema awali alikuwa akichelewa  vipindi vya asubuhi kila siku lakini tangu sasa apatiwe baskeli ataweza kuwahi  vipindi vya asubuhi na kuongeza  juhudi katika masomo yangu.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...