Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
Winga wa timu ya taifa ya Wales, na Nahodha wa timu hiyo, Gareth Bale amewakatalia Marekani kuondoka na ushindi katika mchezo wao wa Kundi B katika Michuano ya Kombe la Dunia, 2022 nchini Qatar baada ya kulazimishana sare ya bao 1-1.
Mchezo huo uliopigwa kwenye dimba la Al Rayyan mjini Doha, timu ya taifa ya Marekani ilanza kupata bao la kuongoza dakika ya 36 kupitia kwa Mshambuliaji wa Klabu ya Lille, Timothy Weah ambaye pia ni Mtoto wa Mchezaji wa zamani wa Soka na Rais wa sasa wa Liberia, George Weah.
Hadi kipindi cha kwanza kinahitimishwa, Marekani walikuwa wanaongoza kwa bao hilo lililofungwa na Mtoto huyo aliyefuata nyayo za Baba yake kulisaka kabumbu. Kijana Timothy alitumbukiza wavuni Mpira safi baada ya kupokea ‘Pasi’ safi kutoka eneo la katikati ya uwanja.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu hizo kutafutana, wote wakicheza soka la ufundi ili kupata alama tatu na kujiweka pazuri katika msimamo wa Kundi lao, dakika ya 80, Wales walipata mkwaju wa Penalti, baada ya Bale kufanyiwa ‘Faulo’ eneo la hatari. Penalti hiyo, iliwekwa wavuni kwa ustadi mkubwa na yeye mwenyewe, Gareth Bale dakika ya 82.
Kundi B la Michuano hiyo, Uingereza anaongoza kwenye msimamo akiwa na alama zake tatu, baada ya kupata ushindi wa mabao 6-2 dhidi ya Iran huku nafasi ya pili akiwa Wales mwenye alama moja sawa na Marekani mwenye alama kama hiyo huku Iran akiburuza mkia bila alama yoyote.
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...