.jpg)

.jpg)
MAKAMU
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa
wito kwa watoaji wa huduma za kifedha nchini kutazama
upya masharti ya mikopo, ikiwemo dhamana ya mali zisizohamishika kwa kuwa ni
kikwazo kwa wajasiriamali pamoja na kutafuta njia
za kibunifu katika kuwafikia vijana hapa
nchini ili waweze kupata mikopo itakayoinua maisha yao na uchumi wa taifa kwa
ujumla.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 24 Novemba 2022
wakati akifungua Maadhimisho ya Pili ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayofanyika
katika viwanja vya Rock City Mall Jijini Mwanza. Aidha amesema Riba ya mikopo ya wastani wa asilimia 16 bado ni mzigo
kwa Watanzania walio wengi hivyo amesisitiza kila benki kupitia umoja wao (TBA)
kuchambua mizizi ya changamoto hiyo na kupunguza zaidi riba kwa wakopaji.
Halikadhalika, Makamu wa Rais ametoa wito kwa watoaji wa
huduma za kifedha nchini kupunguza gharama za kutuma na kupokea pesa kimataifa kwa
kuwa zimekua zikisababisha wageni pamoja na diaspora kutumia njia zisizo rasmi
wanapowatumia pesa jamaa zao hapa nchini. Ameongeza kwamba kwa upande wa credit cards, tozo za benki na mawakala
wao zimekuwa mzigo na hivyo kukwamisha
watalii kununua vitu kwa wingi na kuikosesha mapato Serikali na watoa huduma
mbalimbali.
Pia
ameutaka Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) kusaidia
kuhamasisha wanachama wao kutanua wigo wa huduma za kifedha katika maeneo ya vijijini pamoja na mkopeshe zaidi na kukuza
akiba ili kupunguza utamaduni wa wananchi kutunza pesa katika mfumo usio rasmi.
Makamu wa Rais
ametoa wito kwa Benki Kuu ya Tanzania kutoa elimu
na mwongozo kuhusu fursa na hatari zinazoambatana na maendeleo ya wimbi la fedha za kidigitali (Central Bank Digital Currency, cryptocurrencies,
bitcoins n.k.)ambayo yanaigusa jamii hususan vijana na baadhi ya wastaafu wenye
kiu ya kuwekeza huko. Pia amewasisitiza
Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha
watoa huduma wanaheshimu Sheria ya kumlinda mtumiaji wa huduma
jumuishi za fedha kwa njia ya simu za mkononi. Amesema riba zinazotozwa na baadhi ya watoa huduma kutokana na mikopo
ya muda mfupi ya fedha na muda wa maongezi ni kubwa hivyo wananchi waelezwe
makato yao kabla hawajaamua kuchukua mikopo hiyo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Hamad
Chande amesema kupitia maboresho yaliofanyika katika sekta ya fedha nchini
jumla ya shilingi Trilioni 3.99 imekopeshwa kwa sekta binafsi ikiwa ni ukuaji
wa asilimia 19.4, kuchangia ukuaji wa pato la taifa kwa asilimia 4.9 kwa mwaka
2021 pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya huduma za fedha kwa njia ya simu
kufikia akaunti milioni 33.14.
Chande amesema sekta ya fedha inakabiliwa na changamoto mbalimbali
nchini ikiwemo wananchi kutumia huduma za fedha zisizo rasmi kama vile biashara
haramu ya upatu , biashara zisizo rasmi kwa njia ya mtandao pamoja na idadi
kubwa ya wananchi kutokuwa na uelewa wan kutosha kuhusu teknolojia ya masuala
ya fedha.
Awali akitoa taarifa ya Maadhimisho ya Pili ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa , Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Lawrence Mafuru amesema maadhimisho hayo ni utekelezaji wa mpango mkuu wa maendeleo ya sekta ya fedha wa mwaka 2020/2021-2029/2030 ambao umelenga kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha , mitaji ya muda mrefu kulinda watumiaji wa huduma za fedha, kuimarisha sekta ya fedha, kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya sheria , kanuni , taratibu na miongozo katika sekta ya fedha nchini.
Ameongeza kwamba wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa inalenga kuwafikia
wadau mbalimbali wakiwemo watumishi wa umma, wanafunzi, wanawake , vijana wajasiriamali
wadogo na wa kati,asasi za kiraia pamoja na zile za kidini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...