Watuhumiwa watatu wakitoka katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Novemba 10, 2022 mara baada ya Kusomewa mashtaka manne yanayowakabili. Washtakiwa wanadaiwa kukwepa kodi na kuisababishia mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya zaidi ya sh. Milioni 487. Mashtaka mengine ni Kuchepusha bidhaa kutoka njia yake iliyotengwa na kuwasilisha nyaraka za uongo.
Na Karama Kenyunko Michuzi TV
MKURUGENZI wa Dewa Trading Logistic Ltd , Erasto Dewa na wenzake wawili wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka manne ikiwemo la kukwepa kodi na kuisababishia mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya zaidi ya sh. Milioni 487.
Mashtaka mengine ni Kuchepusha bidhaa kutoka njia yake iliyotengwa na kuwasilisha nyaraka za uongo.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo leo Novemba 10, 2022 na wakili wa serikali Mwandamizi kutoka TRA, Medalakini Emmanuel akisaidiana wakili Neema Moshi imewataja washtakiwa wengine kuwa ni, Ramadhani Salum na Frank Mgata.
Mbele ya Hakimu Francis Mhina imedaiwa washtakiwa wametenda makosa hayo kati ya Septemba 21 na 28, 2022 huko Tabata, ndani ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Katika shtaka la kuchepusha bidhaa kutoka kwenye njia yake iljyotengwa inadaiwa, Septemba 28, 2022 huko katika eneo la Tabata, washtakiwa kwa pamoja walifanya ulaghai kwa kuchepusha bidhaa za vitenge kutoka njia iliyotengwa ya kutoka Dar es Salaam kwenda Malawi na kupakua bidhaa hizo katika eneo la Tabata jijini Dar es Salaam.
Katika shtaka la tatu linalomkabili mshtakiwa Dewa peke yake inadaiwa, Septemba 21,2022 kwa udanganyifu alitoa tamko la uongo la maelezo ya shehena ya marobota 290 kama mashuka badala ya vitenge.
Katika shtaka la mwisho inadaiwa Septemba 28, huko Tabata, washtakiwa wote kwa pamoja kutokana na matendo yao ya ukwepaji kodi, waliisababishia TRA hasara ya sh. 487,945,210.
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na imeahirishwa hadi Novemba 24, 2022.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...