Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru ameridhishwa na maandalizi na utayari wa wanafunzi kuelekea kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne na kusema kuwa halmashauri yake inategemea matokeo bora zaidi ya msimu uliopita.
Mkurugenzi Mafuru aliseme hayo alipofany ziara ya kutembelea na kukagua maadalizi ya wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani yao ya taifa ya kidato cha Nne katika shule ya sekondari Miyuji iliyopo jijini Dodoma.
Mafuru alisema “leo nimetembelea shule ya sekondari Miyuji. Nimekuja kukagua maandalizi ya wanafunzi wa kidato cha Nne na program maalum ya kuwapa wanafunzi muda wa kutosha wa kusoma ili kujiandaa na mtihani wa taifa. Nimejionea kuwa wanafunzi wanajiamini na wapo tayari kuanza mitihani wiki ijayo. Sisi halmashauri tuliamua kuwatengenezea mazingira mazuri ya kusoma. Tukasema kwa miezi miwili hii tukae na wanafunzi hapa shuleni ili wapate muda wa kutosha moja musoma na mbili kupumzika”.
Mkurugenzi wa Jiji alisema kuwa taarifa ya awali wanafunzi hao walikuwa na uwezo wa chini sana. Kutokana na program hiyo maalum wanafunzi wanauwezo mzuri. “Nimejionea, nimeenda nimekutana na wanafunzi wana ari kubwa ya ufaulu. Kwa kweli nimshukuru Afisa Elimu Sekondari, Madam Upendo Rweyemamu ambae kimsingi ndiye aliyeleta hii program kwa Jiji la Dodoma. Iliwasilishwa katika Baraza la Madiwani wakaridhia na tumeona kujiamini kwa watoto, ogopa mtoto anayekwambia lete mtihani hata leo, maana yake wapo tayari. Matarajio ya Jiji ni matokeo bora zaidi ya msimu uliopita” alisema Mafuru.
Aidha, alimshukuru Mkuu wa Shule ya sekondari Miyuji, Mwalimu Greyson Maige kwa kusimamia program hiyo maalum katika shule yake. “Mwalimu Maige anajiamini kwamba wanafunzi watafaulu vizuri. Na walimu wake ambao wamesimamia program hii wanahakikisha kuwa wanafunzi wapo tayari kuanza mitihani wiki ijayo wakiwa katika mazingira rafiki ukilinganisha na miaka ya nyuma” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Kwa upande wa Afisa Elimu Sekondari Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alisema kuwa maandalizi ya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne yamekamilika. Watahiniwa wote wapo tayari kwa ajili ya mtihani. “Tutakuwa na jumla ya watahiniwa 6,647 ambao watafanya mtihani. Kati yao wavulana ni 3,019 na wasichana ni 3,628. Tulianza kuwaandaa wanafunzi hawa muda mrefu. Tumekuwa na program mbalimbali kama program za shule kwa shule na program za ndani ya wilaya.
Akiongelea program maalum kwa wanafunzi walioonekana kuwa ufaulu hafifu alisema kuwa wamefundishwa kupitia program maalum ili waweze kuongeza ufaulu wao. “Tunaprogram maalum kwa wanafunzi walioonekana wana ufaulu hafifu. Tuliwatengenezea mazingira ya kuwaweka pamoja na kikosi kazi cha walimu 56 wamekuwa nao kwa zaidi ya miezi miwili. Hivi karibuni tuliwapa mtihani wa jaribio na wanafunzi wengi walipata daraja A na B katika masomo yao. Wanafunzi hawa tumewaandaa vizuri na hata kisaikolojia wapo tayari kukabiliana na mtihani” alisema Mwalimu Rweyemamu.
Akiongelea matarajio ya ufaulu kwa ngazi ya halmashauri, alisema kuwa matarajio ni kuongeza ufaulu zaidi. “Unapowekeza mahali unategemea kupata mabadiliko ama mavuno mazuri. Mwaka jana tulikuwa na daraja la I (652) kati ya wanafunzi 55,326. II (524), III (1,012) IV (2,735) na O (403). Tulipata ufaulu wa asilimia 93 na GPA ya 3.1. Kwa mikakati tuliyoweka na program tunazofanya tutapunguza sana Daraja 0. Lakini daraja la I-III litaongezeka sana” alisema Mwalimu Rweyemamu.
Afisa Elimu huyo alilishukuru Baraza la Madiwani kwa kuwa msaada kwa idara yake. “Matunda haya ninayopata siyo kwamba napigana mwenyewe nina nguvu kubwa ya viongozi wangu wakiwemo madiwani, Mstahiki Meya, Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Uchumi na Afya, maafisa elimu kata na wakuu wa shule. Shukrani za kipekee kwa Mkurgenzi wa Jiji kwa ‘support’ kubwa aliyoifanya kwenye idara yangu. Kama Mkuu wa Idara unaweza kuwa na mawazo mazuri ya jinsi ya kuboresha taaluma kama usipopata ‘support’ yake huwezi kutoboa” alisema Mwalimu Rweyemamu.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma lina vituo 54 vitakavyofanya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne mwaka 2022.
Home
ELIMU
MKURUGENZI HALMASHAURI YA JIJI LA DODOMA ARIDHISHWA MAANDALIZI MTIHANI WA TAIFA KIDATO CHA NNE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...