NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deo Ndejembi amekemea tabia ya baadhi ya waajiri katika Taasisi za Umma kuficha barua za uhamisho wa watumishi wa umma ambao Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ameridhia na kutoa kibali cha uhamisho ili wakautumikie umma katika maeneo mengine ya nchi ambayo mamlaka imeona kuna uhitaji.
Akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Mhe. Ndejembi amesema, waajiri na Maafisa Utumishi wanapaswa kutenda haki kwa watumishi wa umma ambao wanastahili kuhama baada ya kupatiwa kibali cha uhamisho na mwenye mamlaka ambaye ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, na si kufichiwa barua zao za uhamisho kwa lengo la kukwamisha mchakato wa uhamisho.
“Waajiri na Maafisa Utumishi tendeni haki kwa watumishi wa umma ambao wanastahili kuhama baada ya uhamisho wao kuridhiwa na mamlaka, tusifiche barua zao kwani kitendo hicho kinakwenda kinyume na mamlaka na ni kinyume cha Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo,” Ndejembi amesisitiza.
Ndejembi ameongeza kuwa, wapo watumishi wa umma ambao wamefanya kazi kwa muda mrefu katika kituo kimoja cha kazi, hivyo mamlaka kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu-UTUMISHI ikaamua kumpeleka mtumishi huyo katika eneo lingine la kazi ili abadili mazingira ya kazi ambayo yatamuongezea ufanisi kiutendaji, lakini baadhi ya waajiri hukwamisha uhamisho huo wakati mamlaka iliridhia baada ya kufanya uchambuzi yakinifu.
Aidha, Naibu Waziri Ndejembi amewataka waajiri katika Taasisi za Umma kutopitisha barua za kuomba uhamisho za watumishi ambao ni ajira mpya, kwani ajira zao hazina muda mrefu na baadhi yao wanakuwa hawajathibitishwa kazini, hivyo kutotimiza kigezo cha kutumikia miaka mitatu tangu waajiriwe.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...