Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameagiza wafugaji wote ambao wameingiza mifugo yao kwenye maeneo wasiostahili warudi kwenye maeneo yao ya vitalu.

Ametoa agizo hilo kwenye mkutano wa hadhara wakati anasuluhisha mgogoro wa wakulima na wafugaji wa Kijiji cha Mkongo wilayani Namtumbo uliosababisha watu wanne kupoteza Maisha.

Mkuu wa Mkoa ameagiza wafugaji wote waliongiza mifugo yao bila vibali,wapeleke mifugo yao katika maeneo yenye vitalu vya wafugaji ambapo katika Mkoa wa Ruvuma wilaya ya Tunduru ina vitalu vya kutosha kwa ajili ya wafugaji.

“Mkoa wa Ruvuma ndiyo Mkoa pekee nchini ambao umetenga vitalu kwa ajili ya wafugaji,Katika wilaya ya Tunduru kitalu kimoja kina hekari 500,hadi sasa kuna vitalu 107 ambavyo vipo wazi kwa ajili ya wafugaji’’,alisisitiza.

RC Thomas ametoa mwezi mmoja kwa wakuu wa wilaya zote kusimamia zoezi la utambuzi wa mifugo yote iliyopo kwenye maeneo yao kama ina vibali na namna vibali vilivyotolewa.

“Utoaji wa vibali vya mifugo hivi sasa umekuwa ni holela na kuna mazingira ya rushwa,kila mtu amekuwa anatoa vibali hali inayosababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji’’,alisema Kanali Thomas.

Hata hivyo amesema kuanzia Novemba 10,2022 ni marufuku kuingiza mifugo mkoani Ruvuma hadi hapo uhakiki wa kubaini mifugo utakapokamilika.

Amesisitiza kuwa zoezi la utambuzi wa mifugo linaanza Novemba 10 na linatarajia kukamilika Desemba 9 mwaka huu na kwamba baada ya hapo oparesheni kabambe ya kuondoa mifugo iliyopo katika maeneo yasiyostahili itafanyika katika Mkoa mzima.

Mkuu wa Mkoa amewaagiza wakuu wa wilaya kuwachukulia hatua za kinidhamu wenyeviti wote wa vijiji na watendaji wanaohusika katika kuleta migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Amemwagiza Mkuu wa TAKUKURU kuchunguza tuhuma dhidi ya wenyeviti wa vijiji ambao wanatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji.

Kwa upande wake Awadhi Haji Kamishina wa Operasheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania akizungumza kwenye mkutano huo,amesema migogoro ya wakulima na wafugaji hivi sasa imeshamiri katika Kanda ya Kusini.

Amesema migogoro hiyo inasababishwa na watu wachache waliopewa dhamana kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa sababu mbalimbali zikiwemo rushwa hivyo kuruhusu wafugaji kuingia katika maeneo ambayo hawastahili.

Amewataka wafugaji walioingia kinyume na taratibu kuondoka na kwamba vitendo hivyo havitavumiliwa na matukio hayo yakijitokeza tena jeshi la polisi litachukua hatua kali.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt.Julius Ningu amesema serikali hairidhiki na mifugo inayoingia kwenye mashamba ya wakulima na imekuwa inachukua hatua kukabiliana na hali hiyo.
baadhi ya askari wa FFU Songea wakielekea eneo ambalo yalifanyika mauaji ya watu wanne katika Kata ya Mkongo gulioni wilayani Namtumbo kutokana na mgogoro wa wakulima na wafugaji
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mkongo wilayani Namtumbo baada ya kupata maelezo ya mgogoro wa wakulima na wafugaji katika kijiji hicho ulisababisha watu wanne kupoteza maisha


Kamishina wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania Awadhi Haji akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mkongo wilayani Namtumbo baada ya kusikiliza maelezo ya mgogoro wa wakulima na wafugaji katika kijiji hicho.



Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mkongo wilayani Namtumbo wakiwa katika mkutano wa hadhara wa utatuzi wa mgogoro wa wakulima na wafugaji ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...