Na Seif Mangwangi, Arusha
Tatizo la mabadiliko ya Tabia nchi inayosabaisha Njaa, Ukame na siasa chafu zimeelezwa kuwa ni sababu kuu za ongezeko la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi ya kisiasa duniani.
Kutokana na hali hiyo viongozi wa nchi za Afrika wametakiwa kujitafakari na kuja na suluhisho la kudumu kuhusu tatizo hilo la wakimbizi na wahamiaji ambalo limekuwa likiongezeka kila siku.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa majaji wa chama cha majaji wanaoshughulikia masuala ya wakimbizi na wahamiaji leo Jijini Arusha Rais wa Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za binaadamu (ACHPR), Jaji Imani Abdul amesema tatizo la wakimbizi limekuwa likiacha watu wengi katika simanzi.
Amesema maofisa wanaoshughulikia uhamiaji katika nchi mbalimbali Afrika na duniani wanapaswa kujua kuwa watu wamekuwa wakikimbia nchi zao kutokana na sababu mbalimbali na sio hiyari yao.
Jaji Imani amesema mbali ya siasa kuwa sababu mojawapo inayofanya watu wengi kukimbia nchi zao mara baada ya wanasiasa kutofautiana na kuibuka migogoro inayosababisha vita katika nchi nyingi za Afrika lakini sababu zingine ni mabadiliko ya hali ya hewa.
“Kuna tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa ambayo katika miaka ya karibuni limekuwa ni tatizo kubwa sana, watu wanahama nchi zao kutokana na ugumu wa maisha, wanakimbilia nchi zingine kutafuta chakula, sasa watu wa uhamiaji wanatakiwa kujua hili,”amesema.
Amesema watu wanaoshughulikia uhamiaji wanapaswa kujua kuwa hawa watu hawakimbilii katika nchi zao kwa kupenda, bali kuna mambo magumu nyuma yao ndio sababu wanakimbia kutafuta usalama wa chakula na maisha yao.
Jaji Imani amesema kupitia mkutano huo, majaji ambao kazi yao kubwa ni kutoa maamuzi ya haki katika mahakama zao, watajadili mambo mengi na kuja na tamko ambalo wataliwasilisha kwa watawala katika nchi za Afrika.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Majaji wanaoshughulikia wakimbizi na wahamiaji Duniani ambaye pia ni Jaji wa mahakama ya Upeo nchini Kenya, Jaji Isaack Lenaole amesema nchi za Afrika zinapaswa kujua sababu ya watu kuhama kabla ya kuzuia wasiingie katika nchi zao.
Amesema kutokana na ukame ambao umezikumba nchi za Somalia na Ethiopia, zaidi ya watu 3200 wamekimbilia katika nchi ya Kenya, ikiwemo wasomali 1800 na Waethiopia 1500 ambapo shida kubwa ni njaa katika maeneo yao.
“Leo hii ukizuia wakimbizi na wahamiaji wasiingie nchini kwako ni kwamba unataka wafariki jambo ambalo sio sawa kibinaadam, hivyo tunapaswa kujadili suala la mipaka yetu na haki za wakimbizi na wahamiaji na kuja na suluhisho la kudumu,”amesema.
Wakati huo huo Rais wa Chama cha Majaji wanaoshughulikia wakimbizi na wahamiaji Afrika, Jaji Dunstan Mlambo, amesema warsha hiyo inafanyika ikiwa ni kuzikumbusha nchi za Afrika kuwa kuhifadhi wakimbizi na watu wanaohitaji hifadhi za kisiasa ni haki za binaadam na zinapaswa kuheshimiwa.
Amesema malengo ya warsha ni pamoja na kuwajengea uwezo majaji kuhusu masuala ya wakimbizi na wahamiaji katika nchi zao na kuwakumbusha majukumu yao ya kutoa haki. Pia katika warsha hiyo majaji watajadili sheria za uhamiaji na kubainisha kasoro zilizopo ili ziweze kufanyiwa mabadiliko.
Rais wa Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binaadam, Jaji Imani Abood akitoa salamu za ukaribisho katika warsha hiyo
Majaji wakiwa kwenye mkutano
Majaji zaidi ya 200 ambao ni wanachama wa Chama cha Majaji wa Afrika wanaoshughulikia masuala ya wakimbizi na wahamiaji wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano wao unaofanyika jijini Arusha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...