Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Albert Chalamila amefungua mafunzo ya kukabiliana na maafa hususani kwenye eneo la uokoaji kwa vikundi vya wavuvi kutoka Manispaa ya Bukoba na Wilaya ya Missenyi yanayotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya Maafa.
Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo ametumia nafasi hiyo kufafanua baadhi ya mambo kuhusiana na ripoti ya ajali ya ndege ya Precision kuwa ipo ripoti ya siku 14, ripoti ya miezi mitatu na ripoti ya baada ya mwaka. Wachunguzi wachukua vifaa vyote vinavyohitajika ambavyo ni kisanduku cheusi (black box), wataangalia rekodi za sauti za mawasiliano ya marubani ambayo walifanya kabla ya ajali na ndipo watakuja na majibu ya kilichosababisha ajali.
“Nitoe ufafanuzi kuhusu mambo kadhaa juu ya ripoti iliyotolewa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, chini ya Waziri Profesa Mbalawa, alisema kuwa mlango wa ndege ulifunguliwa na wahudumu kwa kushirikiana na abiria mmoja. Kuna baadhi ya watu mmekuwa mnaipinga ripoti, ni kwamba taarifa za baada ya uchunguzi uwa hazipaswi kubezwa kwasababu ni baada ya uchunguzi. Mtakumbuka kwamba sisi tulitoa ripoti ya awali kwamba majeruhi walikuwa 26 lakini baada ya uchunguzi majeruhi walikuwa 24 na wawili walikuwa ni majeruhi ambao hawakuwa wasafiri,”ameeleza Mhe. Chalamila
Ameendelea kueleza kuwa ripoti iliyotolewa na Profesa Mbalawa ni ripoti sahihi kwasababu waliokuwa nje waliona juhudi na jitihada zilizofanywa na wavuvi na watu wengine wakiwa karibu na milango, wameizunguka ndege na wengine wakiwa majini. Lakini ripoti imeonyesha na waliokuwa ndani nao walikuwa wanafanya jitihada za kufungua mlango ili watu waweze kutoka. Kama mlango ulifunguliwa kwa jitihada za aliye nje na aliye ndani ichukuliwe zote zilikuwa ni jitihada za kuokoa. Na baada ya watu kutoka ndani ya ndege walifika nchi kavu kwa msaada wa vyombo vya wavuvi wa Mkoa wa Kagera kwasababu ndio waliokuwa eneo la karibu na tukio.
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Moses Machali ameeleza kuwa ujio wa mafunzo haya ni jambo jema na la kupongezwa kwasababu yatawajengea uwezo wa namna gani wataweza kukabiliana na majanga pale yanapojitokeza katika maeneo yao. Kupitia wadau mbalimbali walioalikwa, wanaofanya kazi zao ndani ya ziwa na kandokando ya ziwa anaamini yapo mambo watakayojifunza na kupata ujuzi na maarifa sahihi ya namna watakavyokabiliana na majanga hayo. Amewapongeza wavuvi kwa kuonesha ushirikiano mzuri na kwa kazi kubwa waliyoifanya wakati wa uokoaji kwenye ajali ya ndege.
Aidha amewasihi watu kuacha maneno ya upotoshaji ya kuwagawa wavuvi kutokana na kitendo cha kijana Majaliwa kuonekana kuwa amefanya kazi kubwa kuliko wenzake, hii haina maana kuwa wengine hawakufanya kazi bali kwa ushirikiano wa pamoja wote wamefanya kazi kubwa kuwezesha suala zima la uokoaji. Hivyo kupitia kwa kijana Majaliwa ambae ameonekana kwa niaba ya wengine, miongoni mwa kundi la wavuvi ni jambo la kujivunia kuonekana kwake na imekuwa ni heshima kwao. Na kuwataka wavuvi wawaepuke watu wanaotoa maneno ya kuwagawa.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Luteni Kanali Selestine Masalamado ameeleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya maafa inajukumu la kusimamia masuala ya maafa Nchini kwa kuzingatia mipango na miongozo kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Menejimenti ya Maafa Sura namba 6 ya mwaka 2022. Idara imeendelea kupambana kupunguza maafa kwa kusimamia na kuratibu huduma za dharura pale majanga yanapotokea kwa kushirikiana na Wizara, Taasisi, Idara na Mashirika.
Kutokana na ajali ya ndege ya shirika la precision iliyotokea hivi karibuni na kusababisha vifo vya watu 19 na majeruhi 26 waliokolewa amewapongeza wavuvi walioshiriki katika zoezi zima la uokoaji. Ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa alielekeza kujengewa uwezo kwa vikundi vya wavuvi katika ziwa Viktoria hasa eneo la Mkoa wa Kagera lakini pia katika ukanda wa maziwa makuu yote Nchini, hivyo wameanza na Mkoa Kagera baada ya hapo watapeleka elimu hiyo maeneo mengine ya ukanda wa maziwa makuu.
Sambamba na mafunzo, vikundi na wadau wengine wamekuwa na changamoto ya vifaa vya uokoaji ambavyo vinahitajika ili kurahisisha zoezi la uokoaji wa maisha na mali hivyo idara imeona ni muhimu kutekeleza mpango wa kuwajengea uwezo na kuwapatia vifaa vya kisasa kama Waziri Mkuu alivyoelekeza.
Mafunzo haya yatasaidia kutoa huduma kwa haraka na kuongeza idadi ya wataalamu watakaosaidia uokozi baharini na maziwa makuu hivyo kuanzisha vikundi vya uokoaji. Pia yatatolewa kwa vikundi vya wavuvi kutoka Wilaya ya Bukoba na Wilaya ya Muleba.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...