Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI imesema kuwa ipo pamoja na wadau mbalimbali wanaofanya shughuli za uokotaji wa Taka ili kufanikisha usafi na kupendezesha sehemu mbalimbali hususan kwenye majiji kama Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa na Afisa Tarafa, Tarafa ya Kariakoo, Dar es Salaam, Bi. Christina Kalekezi ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija katika hafla ya uzinduzi wa programu ya Waokota Taka kuelekea Siku ya Waokota Taka Duniani 2023.

Kalekezi amesema ni wajibu wa jamii kutambua umuhimu wa kuzalisha, kukusanya na kuokota Taka ili kuweka mazingira salama, amesema shughuli ya Uokotaji wa Taka ni Ajira hivyo ni wajibu kwa wadau hao kuchangamkia fursa hizo za ajira.

“Nimesikia kilichosemwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, amesema yupo mtu alikuwa anakota Taka, lakini baadae amekuwa Mwajiri, kwa hiyo utaona fursa zilizopo katika shughuli hii ya uokotaji wa Taka”, amesema Kalekezi.

Aidha, Kalekezi amesema Dar es Salaam itaendelea kumuunga mkono, Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla katika Kampeni ya Safisha, Pendezesha Dar es Salaam.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taka ni Ajira Foundation, Allen Kimambo amesema walianzisha Taasisi hiyo kutengeneza ajira zenye hadhi, kubuni mipango ya kubunifu kuondoa Taka na watu kupata ajira kupitia shughuli hizo za uokotaji Taka.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Nipe Fagio, Ana Rocha wameanza kuungana kuhakikisha wanafika malengo yao kwenye shughuli ya uokotaji Taka, amesema watahakikisha Waokota Taka wanakutana kujadiliana masuala mbalimbali yanayowahusu wao.

Siku ya Waokota Taka duniani huadhimishwa kila mwaka Machi 1 ikiwa na lengo la kutambua na kuthamini mchango wa kuokota Taka sehemu mbalimbali na kuhakikisha dunia inakuwa safi.
Afisa Tarafa, Tarafa ya Kariakoo, Dar es Salaam, Bi. Christina Kalekezi (aliyesimama) ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa programu ya Waokota Taka kuelekea Siku ya Waokota Taka Duniani 2023.
Mkurugenzi wa Taka ni Ajira Foundation, Allen Kimambo akizungumza katika hafla hiyo iliyowakutanisha wadau mbalimbali ambao wanahusika katika uokotaji wa Taka.
Wadau mbalimbali wa shughuli za uokotaji wa Taka wakiwasikiliza mazungumzo mbalimbali katika hafla ya uzinduzi wa programu ya Waokota Taka kuelekea Siku ya Waokota Taka Duniani 2023.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...