Na Said Mwishehe, Michuzi TV
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano kimataifa la Korea (KOICA) wameingia makubaliano ya kutiliana saini wa mkataba wa miaka minne wenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani milioni sita sawa na Sh bilioni 13 wenye lengo la kuongeza thamani ya kilimo cha wakulima wadogo na kuimarisha usalama wa chakula na lishe miongoni mwa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi Mkoa wa Kigoma.
Makubaliano hayo yamesainiwa lao katika Ofisi za KOICA jijini Dar es Salaam huku ikielezwa kwamba Mkoa wa Kigoma umekuwa ukiwahifadhi zaidi ya wakimbizi 200,000 kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi.
Mkurugenzi wa KOICA nchini Tanzania, Kyucheol Eo, amesema leo wakati wa utiaji saini mkataba huo ameeleza kwamba mbali na kuwasaidia wakimbizi waliopo Mkoa wa Kigoma lakini mkataba huo utawapa fursa wakulima wa mazao mbalimbali mkoani humo na mikoa ya jirani kujikita kwenye kilimo.
"Wakulima wadogo zaidi ya 20,000 watasaidiwa kwenye Kilimo chao na kuwainua kwa kipato pamoja na kujenga uwezo wa kitaasisi, kiufundi, kifedha na kilimo wa mashirika ya kijamii katika eneo hilo. Sina shaka kuwa mradi huu utaimarisha mnyororo wa thamani wa kilimo cha wakulima wadogo na kuboresha usawa wa kijinsia na amani katika wilaya zinazohifadhi wakimbizi Kigoma”, amefafanua
Ameongeza kwa ushirikiano huo mashirika hayo yataendesha mradi wa pamoja wa uliopewa jina la "Kilimo Tija Kigoma" ( KITIKI) ambao utawafanya wakulima wadogo nchini ambao wengi wao ni wanawake kupata mafunzo ya mbinu bora za kilimo, utunzaji wa mazao baada ya kuvuna na kupata masoko.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa WFP nchini Tanzania Sarah Gordon-Gibson alisema WFP itaunganisha wakulima na jamii za wakimbizi ili kuwapatia soko ambalo liko tayari kwa mazao yao na kwamba WFP inashukuru kwa msaada mkubwa kutoka Serikali ya watu wa Jamhuri ya Korea, kupitia ushirikiano na KOICA.
"Hatuwezeshi tu wakulima wadogo, bali pia tunachangia katika muunganiko wa vipengele vitatu vya misaada ya kibinadamu, maendeleo, na ujenzi wa amani mkoani Kigoma,"amesema Sarah na kuongeza Julai mwaka huu WFP ilianza utekelezaji mpango mkakati wake hapa nchini wa miaka mitano.
"Mpango huo utakaosaidia kuchangia maendeleo katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kimazingira ya usalama wa Chakula na lishe kwa wakimbizi na kusaidia wakulima wadogowadogo wa kitanzania na kujenga jamii inayostahimili hali ya hewa, kukuza mshikamano WA kijamii na usawa wa kjinsia".
Ameongeza WFP itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali na kwa kipekee imeishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wanaoutoa kufanikisha utendaji wa shughuli za WFP hapa nchini.
Kuhusu KOICA imeelezwa ni Wakala mashuhuri wa maendeleo wa Kimataifa inayosaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi nyingi na dhamira yake ni kuchangia ustawi wa pamoja na kukuza amani duniani kupitia maendeleo jumuishi ya pande zote bila kuacha mtu nyuma.Nchini Tanzania KOICA inafanya kazi kwa ajili ya watu ,amani ,ustawi ,sayari na ushirikiano.
Wakati Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani ni Shirika kubwa zaidi la kibinadamu duniani linalookoa maisha katika hali ya dharura na kutumia msaada wa chakula kutengeneza njia kuelekea amani, utulivu na ustawi kwa watu wanarejea katika hali ya kawaida kutoka katika hali ya migogoro,majanga na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
01:Mkurugenzi wa KOICA nchini Tanzania Kyucheol Eo(kushoto) na Mkurugunzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani(WFP) nchini Sarah Gordon-Gibson wakisaini mkataba wa kuungana kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wadogo wa wakimbizi Tanzania .Mkataba huo una thamani ya Sh.bilioni 13 na umesainiwa leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugunzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani(WFP) nchini Tanzania Sarah Gordon-Gibson(kulia) pamoja na Mkurugenzi wa KOICA nchini Tanzania Kyucheol Eo(kushoto) wakiwa wameshika mkataba wa kuungana kwa ajili ya kusaidia wakulima wadogo na wakimbizi nchini .Mkataba huo una thamani ya Sh.bilioni 13 na umesainiwa leo Novemba 3 mwaka 2022.
Mkurugenzi wa KOICA nchini Tanzania Kyucheol Eo(wa tatu kushoto) na Mkurugunzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani(WFP) nchini Sarah Gordon-Gibson(wan ne kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na maofisa wengine wa mashirika ya WFP na KOICA baada ya kusainiwa kwa mktaba wa ushirikiano wenye lengo la kuwasaidia wakulima wadogo na wakimbizi nchini Tanzania.
Mkurugunzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani(WFP) nchini Tanzania Sarah Gordon-Gibson(kulia) pamoja na Mkurugenzi wa KOICA nchini Tanzania Kyucheol Eo(kushoto) wakiwa wameshikana mikono baada ya kusaini mkataba wa ushirikiano wa kuwasaidia wakulima wadogo na wakimbizi mkoani Kigoma nchini Tanzania.
Mkurugunzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani(WFP) nchini Tanzania Sarah Gordon-Gibson(kulia) pamoja na Mkurugenzi wa KOICA nchini Tanzania Kyucheol Eo(kushoto) wakifurahia jambo baada ya kusaini mkataba wa ushirikiano wa kusaidia wakulima wadogo na wakimbizi nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...