Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Tanzania, Eric Sambu (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Manunuzi wa Benki ya CRDB Pendason Philemon wakifurahia jambo wakati wa hafla ya kuwapa tuzo watoa hudum bora ijulikanayo kama Consumer Choice Award Africa 2022 iliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
KAMPUNI ya ulinzi ya kibinafsi ya SGA Security imeshinda tuzo ya mtoa huduma bora na salama anayekubalika na wateja na mwenye kutumia vifaa bora na vya uhakika katika kutoa huduma ukanda wa Afrika Mashariki.
SGA ilishinda tuzo hiyo kwenye hafla ya kutoa tuzo kwa watoa huduma bora ijulikanayo kama Consumer Choice Award Africa 2022, iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Tanzania, Eric Sambu, alielezea furaha yake kufuatia ushindi huo ambapo amesema kuwa tuzo hiyo ni ushahidi tosha kuwa wateja wana Imani na kampuni hiyo kongwe ya ulinzi hapa nchini.
“Tumejikita katika kutoa huduma zetu kwa weledi mkubwa huku tukitumia vifaa vyenye ubora na hili ndilo limepelekea wateja wetu kupiga kura ya ubora wa huduma kwa kampuni yetu na kushinda tuzo hii kwa mwaka wa tatu sasa,” alisema.
Aliongeza, “Huu ni ushahidi tosha unaoonyesha ya kuwa tumefanya maboresho makubwa katika kutoa huduma zetu lengo kuu likiwa ni kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma zinazoendana na thamani ya fedha wanazotoa ili kupata huduma tunazotoa”.
Aliendelea kusema kuwa tuzo hiyo ni maalum kwa zaidi ya wafanyakazi 18,000 wa kampuni hiyo walioko katika mkoa huo wa Dar es Salaam ambao alisema wamejitolea kwa hali na mali katika kuhudumia wateja wa kampuni hiyo.
“Tayari tuna Vyeti vinne vyenye hadhi ya kimataifa na vinavyotambuliwa na taasisi ya viwango ya kimataifa ya ISO kwa miaka kadhaa ambavyo vinaonyesha udumishaji wa mifumo thabiti ya usimamizi vinavyoakisi ubora wa huduma zetu kwa manufaa ya wateja wetu na umma kwa ujumla", Bw Sambu aliongeza.
Alisema kuwa siri ya mafanikio katika huduma za ulinzi na usalama ni kuwajengea uwezo wafanyakazi katika kuwahudumia wateja vizuri na ambapo aliongeza kwa kusema kuwa SGA imewekeza sana katika kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa ngazi zote.
Hivi karibuni, SGA ilitunukiwa tuzo ya mwajiri anayekidhi vigezo zaidi Zanzibar, tuzo iliyotolewa na chama cha wafanyakazi (ZAFICOWU), chama cha waajiri Zanzibar (ZANEMA) kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi Zanzibar.
Bw. Sambu aliendelea kusema kutambulika kwake kampuni hiyo kiasi cha kupata tuzo mbalimbali ni ishara ya wazi kuwa imejikita katika kutoa huduma bora na kwamba kampuni hiyo sasa ni mfano bora wa kuigwa na taasisi zingine hapa nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...