Picha ya pamoja kwenye makabidhiano ya mkataba wa maridhiano,taasisi ya maji safi na taka ya Tanga-UWASA juu ya uanzilishwaji wa hati fungani za kukusanya fedha kwaajili ya kuboresha mfumo wa maji jijini Tanga,kuanzia kushoto ni Mkurugenzi Sera na Mipango-Tamisemi John Cheyo, Mkuu wa UNCDF-Tanzania Peter Malika,Mkurugenzi wa Idara ya Uwekezaji wa benki ya NBC, Bw. James Meitaroni James Meitaron na Mkurugenzi kutoka Tanga-UWASA Geofrey Hill.
– Leo Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji na Uwekezaji (UN Capital Development Fund -UNCDF) limetangaza rasmi uteuzi wa Benki ya NBC kuwa mtaalam mshauri atakayekamilisha hatua za msingi kuwezesha kuuzwa kwa Hati fungani ya Mamlaka ya Maji Tanga (Tanga UWASA) ambayo itakuwa ya kwanza kuwahi kutolewa na taasisi ya Serikali nchini.
Tangazo hilo la uteuzi limeambatana na utiaji saini wa makubaliano ya kimkakati baina ya UNCDF na Benki ya NBC ambayo itaongoza timu ya wataalamu washauri inayojumuisha taasisi tano zinazotoa huduma za ushauri wa kifedha na uwekezaji na kusajiliwa na Mamlaka ya soko la hisa na mitaji (Capital Market and Securities Authority-CMSA). Hatua hii ya uteuzi ni kwa mujibu wa matakwa na miongozo ya CMSA ambapo timu hiyo inatarajiwa kuhakikisha hati fungani ya Mamlaka ya Maji Tanga inaorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ifikapo robo ya kwanza ya mwaka 2023. Mkurugenzi wa Tanga UWASA, Bw. Geofrey Hill Akiongea katika hafla hiyo ya utiaji Saini, Mkurugenzi wa Tanga UWASA, Bw. Geofrey Hill, amesema, “Siku hii muhimu imefikiwa kutokana na ushirikiano wetu na UNCDF na kwa kuzingatia miongozo na maelekezo ya Serikali ya kutafuta vyanzo mbadala vya fedha ili kutekeleza miradi ya maendeleo. Tunatarajia kufanya kazi kwa ukaribu na NBC ili kuharakisha hatua zilizobaki kuwezesha upatikanaji wa fedha zitakazotumika kuboresha na kuongeza uwezo wetu wa kusambaza maji kwa wananchi na maeneo yasiyo na huduma hiyo”.
Kadhalika, akitoa salamu zake Mkuu wa Shirika la UNCDF Tanzania Bw. Peter Malika, alieleza kuwa “Tunajivunia kuwateua NBC ambayo ni taasisi ya kitanzania kukamilisha suala hili la kihistoria. Hii ni njia mojawapo ya kuimarisha na kujenga uwezo wa ndani (national capacities) kuibua na kutumia vyanzo bunifu vya fedha kugharamia maendeleo. UNCDF kama mdau wa maendeleo ina nafasi muhimu ya kusaidia kutatua changamoto za upatikanaji wa fedha hususani kwenye nchi zinazoendelea ambazo masoko ya fedha ni machanga.”
Mkurugenzi wa Idara ya Uwekezaji wa benki ya NBC, Bw. James Meitaroni alisema “Tukiwa kama Benki ya kizalendo, tunajivunia kuwa taasisi ya kifedha ya kwanza nchini kushiriki kama kiongozi wa mchakato na mtaalam mshauri, katika kuhakikisha ukamilifu na uuzwaji wa hati fungani hii ambayo itakuwa ni ya kwanza kutokea nchini Tanzania. Leo tumeshuhudia historia ikiandikwa ambapo kwa mara ya kwanza nchini, Mamlaka ya Umma imefungua milango mipya ya kupata fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Fedha zitakazopatikana kutoka kwenye mauzo ya hati fungani zitaenda moja kwa moja kurekebisha miundombinu ya maji ya mji wa Tanga na hivyo kuongeza tija ya upatikanaji na usambazaji maji jijini Tanga.
Tunajivunia kuwa Benki washauri na kutumia uzoefu wetu katika kuleta suluhu ya changamoto zinazokabili jamii. Kupitia hati fungani hizi tunaenda kupata suluhu kubwa ya tatizo la upungufu wa mji mkoani Tanga na vijiji vya jirani. Tunaishukuru sana serikali na wadau wengine kama UNCDF kwa kuendelea kuweka mazingira bora yanayofanya taasisi za kifedha kama sisi NBC kushiriki katika shughuli za kutatua changamoto za jamii inayotuzunguka”
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...