Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WANANCHI na viongozi wa Vijiji vya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wameonywa kutouza ardhi kiholela kwa wageni kwani miaka ijayo watajuta kwa kukosa ardhi kwani ardhi haiongezeki ila watu wanaongezeka.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Ormemei Laizer ameyasema hayo kwenye tafrija iliyofanyika nyumbani kwake Kata ya Naisinyai baada ya kumshukuru Mungu katika Kanisa la KKKT kutokana na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo hivi karibuni.
Amesema hivi sasa Wilayani Simanjiro kumezuka wimbi la wananchi na viongozi wa baadhi ya vijiji kuuza ardhi kwa watu wanaotoka wilaya za jirani bila kutambua kuwa huo ndiyo urithi wao.
Amesema wananchi hao wakiuza ardhi yao miaka ijayo watakuja kuwa mizigo kwani watalalamika kwa viongozi kuwa hawana ardhi ili hali walishakuwa na ardhi kisha wakaiuza.
“Kila wakati nitakuwa ninakemea hili suala la uuzaji wa ardhi kwani watu wanakuja kutoka wilaya na mikoa jirani na kununua ardhi kwa bei chee Simanjiro ili hali huo ndiyo urithi wa wana Simanjiro,” amesema Kiria.
"Mtawaachia nini watoto wenu, ardhi inanunuliwa na wageni, hakuna siku utanunua ardhi tena hiyo ardhi kwa wageni, ardhi haiongezeki, kwa kiongozi wa serikali hakuna Mwenyekiti mwenye mamlaka ya kutoa ardhi bila idhini ya mkutano mkuu wa Kijiji," amesema Kiria.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dkt Suleiman Hassan Serera, akizungumza kwenye tafrija hiyo amewataka wananchi na viongozi wa Simanjiro kuwa na uzalendo na Simanjiro yao.
"Ninyi wenyeji ndiyo watoto wa chumbani hivyo mnapaswa kuwa na uzalendo na uchungu zaidi na maendeleo ya Simanjiro kuliko sisi viongozi wa kuteuliwa ambao ni watoto wa sebuleni," amesema Dkt Serera.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...