Na Mwandishi Maalum, Morogoro
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kutoka katika Kata zinazotaraji kufanya uchaguzi mdogo wa udiwani Desemba 17, 2022 kutofanya kazi ya uchaguzi kwa mazoea, badala yake wazingatie sheria, kanuni za uchaguzi pamoja na maelekezo ya Tume katika utendaji wao.
Tume pia imewataka wasimamizi wa nchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuhakikisha wanavishirikisha Vyama vyote vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi ili kurahisha utekelezaji wa majukumu yao.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Adv. Magdalena Rwebangira wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya wasimamizi wa Uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Kata yanayofanyika Mkoani Morogoro.
Adv. Rwebangira amesema Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha, hatua na taratibu mbalimbali za kufuatwa na kuzingatiwa kwani hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na hivyo kupunguza kama siyo kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
“Nachukua nafasi hii kuwaasa kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yenu mnao katika uendeshaji wa uchaguzi, ni vyema mhakikishe mnazingatia maelekezo mtakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea”,alisema Adv. Rwebangira.
Aidha amewataka kujiamini na kufanya kazi kwa weledi, na kwamba katika utendaji wa majukumu yao wanapaswa kuzingatia Katiba ya Nchi, Sheria za Uchaguzi na Kanuni zake, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume na kuongeza kua jambo hilo lisiishie katika mafunzo na nadharia bali ionekane kufuatiwa katika kutenda.
“Sanjari na hilo nawaasa kukumbuka kuvishirikisha Vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika maeneo yenu katika masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa kwani jambo hilo litawarahisishia sana utekelezaji wa majukumu yenu,”alisema Adv Rwebangira.
Wasimamizi hao wametakiwa kuhakikisha wanayatambua na kuyajua vizuri maeneo ambayo chaguzi utaendeshwa ikiwemo hali ya miundombinu ya kufika katika Kata na hasa Vituo vya kupigia kura.
“Mfanye utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani,”alisema Adv. Rwebangira.
Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Adv. Magdalena Rwebangira pia amewataka wasimamizi hao kuhakikisha kuwa wanaajiri watendaji wa vituo wenye weledi, wanaojitambua na kwa kadri inavyowezekana kuacha undugu au upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi.
Alisema jambo muhimu wanalotakiwa kuzingatia Wasimamizi hao wa uchaguzi ni kujiamini, kufanya kazi kwa weredi na kuzingatia Katiba ya nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, maadili ya uchaguzi pamoja na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume.
Aidha Mjumbe wa Tume hiyo ya uchaguzi, aliwasisitizia wasimamizi hao wa uchaguzi kuhakikisha wanafanya utambuzi wa vituo vya uchaguzi mapema kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Uchaguzi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Stephen Elisante, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uchaguzi alisema uchaguzi huo mdogo wa udiwani utafanyika katika Kata 12 za Tanzania Bara ila waliopo katika mafunzo hayo Mkoani Morogoro ni kutoka katika Kata sita za Vibaoni – Halmashauri ya Mji wa Handeni, Lukozi – Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Misugusugu – Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Majohe - Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mnyanjani - Halmashauri ya Jiji la Tanga na Dunda - Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.
Mapema kabla ya ufunguzi wa Mafunzo hayo watendaji w uchaguzi hao walikula kiapo cha kutunza siri na kiapo cha kujitoa uanachama wa vyama vyao vya siasa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro, Mhe. Japhet Bwire Manyama.
Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Adv. Magdalena Rwebangira akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya siku tatu ya wasimamizi Uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi pamoja na watendaji wengine wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mdogo wa udiwani unaotaraji kufanyika tarehe 17 Desemba, 2022. Mafunzo hayo yanayohusisha washiriki 42 kutoka Halmashauri sita za Jiji la Dar es Salaam, Bagamoyo mji, Kibaha Mji, Handeni Mji, Jiji la Tanga na Lushoto yanafanyika Mkoani Morogoro.
Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Adv. Magdalena Rwebangira akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya siku tatu ya wasimamizi Uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi pamoja na watendaji wengine wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo na Kata ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mdogo wa udiwani unaotaraji kufanyika tarehe 17 Desemba, 2022. Mafunzo hayo yanayohusisha washiriki 42 kutoka Halmashauri sita za Jiji la Dar es Salaam, Bagamoyo mji, Kibaha Mji, Handeni Mji, Jiji la Tanga na Lushoto yanafanyika Mkoani Morogoro. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Uchaguzi, Stephen Elisante na wengine kulia ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu wa Tume, Felister Ishuza na Mwenyekiti wa Mafunzo hayo ambaye pia ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Handeni, Maryam Ahmad Ukwaju.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Uchaguzi, Stephen Elisante akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mwenyekiti wa Mafunzo hayo ambaye pia ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Handeni, Maryam Ahmad Ukwaju akizungumza wakati wa mafunzo hayo.
Sehemu ya washiriki ambao ni Wasimimizi wa uchaguzi na Wasimamizi wasaidi wa Uchaguzi kutoka Halmashauri sita za Jiji la Dar es Salaam, Bagamoyo mji, Kibaha Mji, Handeni Mji, Jiji la Tanga na Lushoto yanafanyika Mkoani Morogoro wbakifuatilia mafunzo hayo.
Sehemu ya washiriki ambao ni Wasimimizi wa uchaguzi na Wasimamizi wasaidi wa Uchaguzi kutoka Halmashauri sita za Jiji la Dar es Salaam, Bagamoyo mji, Kibaha Mji, Handeni Mji, Jiji la Tanga na Lushoto yanafanyika Mkoani Morogoro wbakifuatilia mafunzo hayo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro, Japhet Bwire Manyama akiongoza kiapo cha kujitoa uanachama wa vyama vya siasa na kutunza siri kwa wazimamizi na wasimamizi wasaidi wa uchaguzi wakati wa mafunzo ya wasimamizi hao kutoka Halmashauri sita za Jiji la Dar es Salaam, Bagamoyo mji, Kibaha Mji, Handeni Mji, Tanga Jiji na Lushoto ambao wanataraji kufanya uchaguzi mdogo katika kata zao Desemba 17,2022.
Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi wakilakiapo cha kujitoa uanachama wa vyama vya siasa na kutunza siri mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro, Japhet Bwire Manyama wakati wa mafunzo ya wasimamizi hao kutoka Halmashauri sita za Jiji la Dar es Salaam, Bagamoyo mji, Kibaha Mji, Handeni Mji, Tanga Jiji na Lushoto ambao wanataraji kufanya uchaguzi mdogo katika kata zao Desemba 17,2022.
Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi wakilakiapo cha kujitoa uanachama wa vyama vya siasa na kutunza siri mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro, Japhet Bwire Manyama wakati wa mafunzo ya wasimamizi hao kutoka Halmashauri sita za Jiji la Dar es Salaam, Bagamoyo mji, Kibaha Mji, Handeni Mji, Tanga Jiji na Lushoto ambao wanataraji kufanya uchaguzi mdogo katika kata zao Desemba 17,2022.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...