Na. Vero Ignatus,Kilimanjaro
Wadau wa maendeleo kutoka Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Women Youth Empowerment CONSERVATION ya nchini Tanzania kwa kushirikiana na wafadhili kutoka Marekani wamejitokeza kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita za kumtua Mama Ndoo Kichwani kwa kuwachimbia kisima cha maji wakazi wa kijiji cha Majevu kilichopo Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.
Akizungumzia mradi huo Mwanzilishi wa Taasisi hiyo ambaye pia ni mhifadhi kutoka Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa Bwana Abel Mtui amesema wameamua kushirikiana na wadau hao kutoka Marekani kuwachimbia maji wakazi hao kutokana na uhaba wa maji katika eneo hilo.
Bwana Mtui amesema mradi huo umegharamiwa na Taasisi isyokuwa ya kiserikali ya KATIE ADAMSON CONSERVATION FUND ya nchini Marekani kwa kushirikiana na taaisi ya Women Youth Empowerment CONSERVATION ya nchini Tanzania ambapo mpaka kukamilika kwake unatarajia kugarimu zaidi shilingi milioni 27 za Kitanzania.
Amesema mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 60 kutokana na changamoto iliyojitokeza wakati wa uchimbaji na kwamba wataalamu wanaendelea kutafuta ufumbuzi;na pia matarajio yao ni jamii inufaike kwa kupata majisafi na salama. Aidha;Mkurugenzi wa Taasisi isyokuwa ya kiserikali ya KATIE ADAMSON CONSERVATION FUND Bwana Dave Johnson amesema, wamefadhili mradi huo wa maji kwa lengo la kwaondolea adha ya maji wananchi wa kijiji hicho kuepuka gharama kubwa ya ununuzi wa maji.
Bwana Johnson amesema hii Ni mara ya tatu anakuja nchini Tanzania kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii ambapo pamoja na kutekeleza mradi huo wa maji bado ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kusaidia jamii.
Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Bi Marry Allan Kanumba ambaye pia ni afisa mipango wa wilaya hiyo amesema mradi huo utakapokamilika utawahudumia wakazi zaidi ya mia moja wa kijiji hicho.
Pia Bi Kanumba amewashukuru wadau hao kuunga mkono juhudi za serikali kuchimba kisima cha maji katika kijiji hicho, hasa ikizingatiwa kwamba Wilaya ya Same inakabiliwa na changamoto ya ukame kutokana na mvua kuchelewa kunyesha hivyo uwepo wa kisima hicho ni ukombozi kwa wananchi hao kwa kuwa watapata majisafi na salama na kuboresha afya zao pamoja na kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji na badala yake watajikita zaidi katika shughuli za uzalishaji.
Akishukuru kwa niaba ya wakazi wa kijiji hicho Mwenyekiti wa kikundi cha Akina Mama cha Mkomazi Marandu conservation fund Women Group Bi Zera Mziray amesema kukamilika kwa mradi huo wa kisima cha maji itakuwa msaada mkubwa kwao, kwani walikuwa wakifuata huduma ya maji umbali wa kilomita mbili mpaka tatu, na kuuziwa maji dumu la lita ishirini kwa shilingi elfu moja.
Wilaya ya Same ni moja kati ya wilaya 7 za Mkoa wa Kilimanjaro;imepakana upande wa kaskazini na Wilaya ya Mwanga na nchi jirani ya Kenya, upande wa kusini na Mkoa wa Tanga na upande wa magharibi na Mkoa wa Manyara ambapo Makao makuu yapo Same Mjini.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...