Na Janeth Raphael - Dodoma
SERIKALI imetoa maagizo tisa ya ugawaji na matumizi ya vishikwambi 293,400 vilivyogaiwa kwa walimu nchini huku ikionya matumizi yasiyosahihi ya vifaa hivyo.
Vishikwambi hivyo ni kati ya 300,000 vilivyotumika kwenye sensa ya watu na makazi 2022 ambapo Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza baada ya kukamilisha kazi ya sensa vigaiwe kwa walimu ili kuimarisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyasema hayo jana jijini hapa kwenye hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa vifaa hivyo kwa sekta ya elimu nchini.
Alisema serikali imedhamiria kuwekeza kwenye Tehama hivyo vishikwambi viwafikie walengwa waliokusudiwa ili kuleta mapinduzi ya elimu nchini ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Tehama ya mwaka 2016.
“Nataka vifaa hivi viwafikie walengwa wote kwa wakati ili waweze kufanya kazi,hapa ningependa kusisitiza kwamba vifaa hivi ni kwa walimu tu na kweli viwafikie na kutumika na walimu na si vinginevyo,”alisema.
Aliwataka viongozi wote watakaopewa majukumu ya kugawa vishikwambi hivyo Mikoani na Wilayani hakikisheni kuwa hakuna mwalimu atakayekosa kishikwambi.
“Vishikwambi na idadi ya walimu tunavijua nataka kuona vishikwambi vimewafikia vizuri, katika ngazi ya shule hakikisheni mnaweka utaratibu maalum wa kuhakikisha uwepo wa matumizi sahihi ya vishikwambi, kwa manufaa mapana ya elimu yetu hapa nchini,”alisema.
Majaliwa alisema kishikwambi hicho kitakuwa ni mali ya mwalimu husika na atakayekosa apelike taarifa kwa Wizara inayohusika ili ifuatilie.
“Tunaamini uwepo wa vifaa hivi utahamasisha sana matumizi ya teknolojia katika ufundishaji, kwa kutumia wataalamu wa ndani wa kila halmashauri uandaliwe utaratibu wa kutoa mafunzo ya msingi ya matumizi ya vifaa hivi, katika ngazi ya kata na wilaya,”alisema.
Alisisitiza walimu wote kutunza vifaa hivyo na kuvitumia kwa malengo kusudiwa ya elimu ikiwamo katika kufundishia somo la Tehama na kwa kurahisisha ufundishaji.
“Vitumike katika kuondoa changamoto ya zana mbalimbali za kufundishia na kujifundishia vifaa rejea kwa walimu, itumike kama nyenzo ya kuwezesha walimu kufikia zana mbalimbali za kuwezesha tendo la ufundishaji na ujifunzaji ikiwamo maktaba mtandao, maktaba ya Taasisi ya Elimu Tanzania(TIE), iliyo na vitabu mbalimbali vya kiada, ziada na miongozo mbalimbali ya kufundishia video na masomo yaliyoandaliwa kwa sauti,”alisema.
Waziri Mkuu alitaka walimu watumie mafunzo mbalimbali wanayoyaleta kwenye mtandao wa mafunzo endelevu kazini kwa walimu inayojulikana kwa jina la MEWAKA yawakute wakiwa shuleni.
“Wizara isimamie kuimarisha ufundishaji wa somo la Tehama katika ngazi zote za shule za msingi, sekondari hadi vyuo ambavyo tunavyo hapa nchini,”alisema.
Awali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda, alisema “Vishikwambi 300,000 vilinunuliwa kwa ajili ya sensa baadhi ya vishikwambi vilipelekwa Ofisi ya Takwimu kwa ajili ya zoezi la sensa ambapo Zanzibar vilipelekwa 6600 na 293,400 vilibaki Tanzania bara.”
Alifafanua mgawanyo wa vishikwambi hivyo kuwa ni walimu wa shule za msingi za umma 185,404, walimu wa shule za sekondari 89,805, Wathibiti Ubora wa shule ngazi ya Wilaya na Kanda 1,666, Wakufunzi wa vyuo vya ualimu vya umma 1393, Wakufunzi wa vyuo vya maendeleo ya wananchi 267, Maofisa Elimu Mikoa, Wilaya na Kata 5,772.
Pia alisema kwa Wakufunzi wa vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi(VETA) vishikwambi 996 na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) Vishikwambi 8,357.
Alitaja faida mbalimbali za matumizi ya vishikwambi hivyo kuwa ni kupunguza gharama na matumizi ya karatasi, kusafiri na kurahisisha upatikanaji wa vyenzo za kujifunzia na kufundishia na usahihishaji wa mitihani.
Pia alisema kwasasa mapitio ya sera ya elimu ya 2014 ambapo yapo mapendekezo ambayo hayatatoka hadharani kwasasa hadi mchakato wa ndani ukamilike.
“Baada ya hapo tutatoa white paper kwa ajili ya kujadiliana tena ili mwakani tufanye maamuzi, vile vile tutapitia Sheria ya elimu ya mwaka 1978 na mapitio ya mitaala yapo hatua za mwisho yanasubiri viongozi wa juu ndio maamuzi yatolewe,”alisema.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa hafla ya kugawa vishikwambi kwa walimu Nchini
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia akizungumza wakati wa hafla ya kugawa vishikwambi leo Mtumba Dodoma
Baadhi ya washiriki wa uzinduzi wa ugawaji wa vishikwambi katika sekta ya elimu wakiwa wamebeba vishikwambi walivyokabidhiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika uzinduzi huo kwenye ukumbi wa jiji Mtumba jijini Dodoma, Novemba 4, 2022. Kutoka kulia ni Mwalimu Hadikwa Chidumizi wa Shule ya Msingi Nkuhungu Dodoma, Mwalimu Victoria Kishiwa wa Shule ya Sekondari Dodoma, Mwalimu Mashaka Mnjalloh, Mdhibiti wa Ubora wa Elimu katika jiji la Dodoma, Mwalimu Robert Tesha, Afisa Elimu Kata ya Mnadani Dodoma na kulia ni Mwalimu Bernard Sinkamba ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Mnguru. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi kishikwambi Mwalimu Victoria Kishiwa wa Shule ya Sekondari Dodoma wakati alipozindua ugawaji wa vishikwambi katika sekta ya elimu kwenye ukumbi wa jiji Mtumba jijini Dodoma, Novemba 4, 2022.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi kishikwambi Mwalimu Bernard Sinkamba ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Munguri Dodoma wakati alipozindua ugawaji wa vishikwambi katika sekta ya elimu kwenye ukumbi wa jiji Mtumba jijini Dodoma, Novemba 4, 2022. Kushoto ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Adolf Mkenda. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...