WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua visima vya dharura vinavyosafishwa, kufufuliwa na kuunganishwa katika mfumo wa usambazaji maji kwa wananchi na kuagiza zoezi hilo pamoja na uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali liwe endelevu.

Mheshimiwa Majaliwa amekagua visima katika eneo la Tabata Relini na Mwananyamala Komakoma jijini Dar es Salaam leo (Alhamisi, Novemba 10, 2022), ambapo ameshuhudia usafishwaji wa kisima pamoja na zoezi la usambazaji maji.

Visima hivyo ni miongozi mwa visima 197 vilivyochimbwa na Serikali mkoani Dar es Salaam ambapo kwa sasa 160 vimefufuliwa na kutoa lita milioni 29.4 kwa siku, Maji hayo yameunganishwa katika mfumo na hivyo kupunguza changamoto ya maji.

Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Bonde la Wami Ruvu pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) waendelee kufanya tafiti kubaini maeneo yenye maji mengi na kuchimba visima na kuyaingiza katika mfumo.

Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kuendelea kulinda maeneo yote yenye vyanzo vya maji pamoja na kuyatumia vizuri maji yanayopatikana ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa maji hususani katika kipindi hiki cha ukame.

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika mikoa yote nchini likiwemo jiji la Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatekeleza kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani ili kuhakikisha wananchi wote nchini wanapata huduma hiyo karibu na maeneo yao ya makazi. Amewataka waendelee kuiamini Serikali yao kwa sababu imedhamiria kuwatumikia.

Awali, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali nchini wizara imejipanga kuchimba mabwawa kwa ajili ya uvunaji wa maji ya mvua na kuyaingiza katika mfumo.

Waziri huyo ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kupata mitambo ya kuchimba visima na hivyo kukabiliana na upungufu wa maji. “Tutashinda site kuhakikisha maji yanapatikana kwa wananchi.”

Mahitaji ya maji katika mkoa wa Dar Es Salaam ni lita milioni 544 kwa siku na uzalishaji maji kwa siku ni lita milioni 520 katika kipindi ambacho kiwango cha maji katika Mto Ruvu kinakuwa katika hali ya kawaida, hivyo kuwa na upungufu wa lita zaidi ya milioni 24.

Hata hivyo katika kipindi hiki ambacho kiwango cha maji kimepungua katika Mto Ruvu uzalishaji wa maji nao umepungua na kufikia lita milioni 300 kwa siku, hivyo kusababisha upungufu wa lita milioni 244.

Hivyo baada ya kuingiza lita milioni 70 kutoka katika mradi wa visima vya Kigamboni na lita milioni 29.4 kutoka katika mradi wa visima vingine 160 vya jijini Dar es Salaam sasa upungufu wa maji ni lita milioni 145 kwa siku, hivyo kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo jijini humo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa akishuhudia usafishaji wa visima vya dharura vinavyosafishwa, kufufuliwa na kuunganishwa kwenye mfumo wa huduma maji Tabata Kisiwani wakati wa ziara yake ya kukagua upatikanaji wa maji kwenye visima mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam ili kuona ni kwanamna ga DAWASA pamoja na Wizara ya Maji wameweza kushughurikia changamoto ya upatikani wa maji katika Jiji hilo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso kuhusu namna walivyofanikisha kusimama pamoja na DAWASA kuchimba visima na kufufua visima 197 ambapo mpaka sasa visima vipatavyo 160 vinatoa maji mpaka sasa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu ya kukagua visima katika Jiji la Dar es Salaam.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa Wizara ya Maji, DAWASA pamoja na Wananchi wa Tabata Kisiwani alipofanya ziara ya kukagua visima vitakavyoweza kupunguza makali ya upatikanaji wa maji kwenye Jiji la Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa pamoja na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso wakipata maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja kuhusu uzalishaji wa maji kwenye Kisima cha Tabata Kisiwani ikiwa ni utekelezaji wa kufufua na kuchimba visima vitakavyoweza kupunguza ukali wa mgao wa maji katika Jiji la Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa pamoja na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso wakipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu Mhandisi Elibariki Mmasi kuhusu hali ya upatikanaji wa maji kwenye mto Ruvu, Wami pamoja na kwenye visima wakati wa ziara ya Waziri Mkuu ya kukagua visima vitakavyoweza kupunguza ukali wa mgao wa maji katika Jiji la Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam,Jenerali Mstaafu, Davis Mwamunyange.
i Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Cyprian Luhemeja (kushoto) wakati alipokagua visima vya dharura vinavyosafishwa na kufufuliwa na kuunganishwa kwenye mfumo wa huduma ya maji kwa wananchi katika eneo la Mwananyamala Kwa Makoma jijini Dar es salaam , Novemba 10, 2022. Wa nne kulia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya DAWASA, Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange na wa tatu kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es salaam, Kate Kamba.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa Wizara ya Maji, DAWASA pamoja na Wananchi wa Mwananyamala kwa Makoma alipofanya ziara ya kukagua visima vitakavyoweza kupunguza makali ya upatikanaji wa maji kwenye Jiji la Dar es Salaam
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso akizungumza na wananchi wa Mwananyamala kwa Makoma wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokagua utekelezaji wa kufufua na kuchimba visima vitakavyoweza kupunguza ukali wa mgao wa maji katika Jiji la Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa pamoja na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso wakipata maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja kuhusu uzalishaji wa maji kwenye Kisima kilichopo Mwananyamala kwa Makoma ikiwa ni utekelezaji wa kufufua na kuchimba visima vitakavyoweza kupunguza ukali wa mgao wa maji katika Jiji la Dar es Salaam
Kisima kilichopo Mwananyamala kwa Makoma



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...