Miongoni mwa maswali ambayo nimekuwa nikijiuliza mara nyingi ni namna ambavyo sekta ya TEHAMA inaathirika kutokana na kutokuwepo kwa muunganiko wa kutosha kati ya taasisi za elimu ya juu pamoja na makampuni hapa nchini. Lakini pia, ni zipi hasa sababu zinazosababisha uwepo hafifu wa muunganiko huo? Pamoja na hayo, katika kupata ufumbuzi swali sahihi la kujiuliza ni kwa namna gani changamoto iyo inaweza kutatuliwa kwa maslahi ya maendeleo ya sekta ya TEHAMA hapa nchini.

Katika mfumo wa jadi wa kukuza vipaji, taasisi za elimu ya juu huweka kipaumbele zaidi katika nadharia na dhana lakini hutoa nafasi kidogo kwa mafunzo kwa vitendo. Si sahihi kusema kuwa hakuna muunganiko wa uleaji na usambazaji wa vipaji kati ya taasisi za elimu ya juu na mahitaji ya makampuni, lakini ni ukweli kuwa mfumo wa sasa wa ukuzaji vipaji una changamoto kubwa.

Katika muktadha huu, mkakati wa muda mrefu unaojumuisha kuchangia rasilimali, faida za ziada, na maendeleo ya pamoja kati ya vyuo vikuu na makampuni inahitajika ili kukidhi usambazaji wa vipaji na mahitaji ya vipaji hivyo; kufikia faida za pamoja kati ya vyuo vikuu, makampuni, na vipaji; na kusaidia maendeleo ya sekta ya TEHAMA.

Katika nadharia, ushirikiano kati ya vyuo vikuu na makampuni unaweza kuwa muhimu katika kukuza suluhisho la shida ya vipaji vinavyokidhi soko la ajira. Hata hivyo, ushirikiano kati ya vyuo vikuu na makampuni unaweza kuwa mgumu kutekelezeka. Ugumu wa utekelezaji wa jambo hilo pamoja na mambo mengi, unasababishwa na mambo yafuatayo:

Kwanza, ushirikiano wa kukuza vipaji kati ya taasisi za elimu ya juu na makampuni haujaendelezwa kikamilifu. Kwa ujumla, ushirikiano huo ni wa hiari na si wa kina.

Pili, baadhi ya makampuni hayaupi kipaumbele mchakato wa mafunzo kwa vitendo, na hayaendani na malengo ya uzalishaji na ukuzaji wa vipaji ya vyuo vikuu.

Kama wadau wa sekta ya TEHAMA, pasi na shaka jambo lililo mbele yetu ni namna bora ya kuufikia muunganiko thabiti kati ya taasisi za elimu ya juu na makampuni kwa lengo la kutatua tatizo la uhaba wa ujuzi unaohitajika katika soko la ajira ili kusaidia ukuaji na ustawi wa sekta ya TEHAMA nchini.


Kituo cha pamoja cha mafunzo ya vitendo kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Huawei

Mnamo 2017, Huawei ilisaini makubaliano ya ushirikiano na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloji katika utekelezaji wa ukuzaji wa vipaji Tanzania. Kupita makubaliano hayo , Huawei ilianzisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Ndaki ya Teknolojia za Habari na mwasailiano (TEHAMA), ukiwa na lengo la ushiriki wa pamoja kwa pande zote mbili katika kuwajengea uwezo na ujuzi wanafunzi katika kada ya TEHAMA.

Kupitia ushirkiano huo, Huawei imejenga mfumo mzuri wa ukuzaji wa vipaji unaoakisi mchakato mzima wa kujifunza, pia imetengeneza daraja la ajira kwa kuimarisha utaratibu wa ushirikiano kati ya vyuo vikuu na makampuni, kwa lengo la kukuza maendeleo ya sekta ya TEHAMA na kubuni mifumo ya maendeleo ya vipaji kulingana na mahitaji ya soko la ajira. Kwa pamoja, Huawei imekuwa ikishirikiana na vyuo vikuu, ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kukuza vipaji vya TEHAMA ambavyo vinakidhi mahitaji ya sekta ya TEHAMA, kutoa vipaji vya hali ya juu kwa maendeleo ya sekta ya TEHAMA nchini na nje ya nchi.

Huawei kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa pamoja wamezindua kituo cha Mafunzo kwa Vitendo. Uzinduzi wa kituo hicho ni muendelezo wa ushirikiano kati ya taasisi hizi mbili katika ukuzaj wa vipaji.

Uanzishwaji wa kituo hiki cha pamoja cha mafunzo kwa vitendo katika chuo kikuu cha Dar es Salaam kitatoa fursa kwa wanafunzi pamoja na wahitimu kupata mafunzo ya vitendo moja kwa moja kutoka kwa wataalum wabobezi katika kada ya TEHAMA kutoka katika kampuni ya Huawei kwa kushirikiana na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa uchache wanafunzi na wahitimu watanufaika na mambo yafuatayo;

1.    Kupata mafunzo ya kada ya mawasiliano kwa vitendo kutoka kwa wataalamu wabobezi, hivyo kuwafanya wanafunzi na wahitimu kuwa na ujuzi wa vitendo sahihi ambao unahitajika katika soko la ajira.

2.    Itaboresha mazingira ya kupata bunifu nzuri zaidi kutoka kwa wanafunzi na wahitimu

3.    Kuelewa kwa kina mfumo mzima wa teknolojia ya mawasiliano na kupata uzoefu utakaowawezesha kufanya shughuli zote zitakazohitajika katika makampuni.

4.    Kukuza vipaji vya vijana walioko shuleni pamoja na wale ambao wamemaliza elimu ya ngazi za juu.

Pamoja na faida hizo chache, jambo kubwa zaidi ni kuwa kituo hiki kitaboresha upatikanaji wa wahitimu wenye ujuzi wa kiufundi ambao watalisaidia taifa katika kufikia utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Mwaka 2025.

 

Imeandaliwa na:

Dkt. Moses Ismail

Mratibu Ubunifu, Ndaki ya Teknolojia za Habari na Mawasiliano,

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...