Muandaaji wa filamu hiyo na mratibu wa taasisi ya Hope For Girls and Women kupitia mradi wa Nyumba Salama, Rhobi Samwelly (kulia,) akizungumza mara baada ya kutazamwa kwa filamu hiyo na kueleza kuwa  elimu zaidi inatakiwa kutolewa kwa jamii kuanzia ngazi ya familia ili kuweza kukomesha vitendo vya ukatili ikiwemo ukeketaji.
 
 

 Baadhi ya wadau wakifuatilia filamu ya In The Name of Your Daughter yenye maudhui ya kupinga ukeketaji kwa wasichana mkoani Mara.

 

KATIKA kuendelea kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia Ubalozi wa Ufaransa nchini kwa kushirikiana na Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa ‘Alliance Francaice’ wamekutanisha wadau na kujadili mustakabali wa watoto wa kike wanaopitia changamoto ya ukeketaji na vitendo vingine vya unyanyasaji wa kijinsia kupitia filamu maalum ya ‘In The Name of Your Daughter’ iliyobeba maudhui ya kupinga vitendo vya ukatili hasa ukeketaji katika Mkoa wa Mara.

Akizungumza  katika mjadala maalum mara baada ya filamu hiyo iliyotazamwa katika kituo cha utamaduuni cha ubalozi wa Ufaransa nchini ‘Alliance Francaise’ jijini Dares Salaam  muandaaji wa filamu hiyo na mratibu wa taasisi ya Hope For Girls and Women kupitia mradi wa Nyumba Salama, Rhobi Samwelly amesema katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia elimu zaidi inatakiwa kutolewa kwa jamii kuanzia ngazi ya familia ili kuweza kukomesha vitendo vya ukatili ikiwemo ukeketaji.

Amesema, katika mchakato wa kuwaokoa mabinti dhidi ya vitendo vya ukeketaji na kuwapeleka katika nyumba salama bado kuna changamoto kubwa hasa kwa jamii kutotaka kubadili mtazamo juu ya ukeketaji.

‘’Jamii bado imeshikilia tamaduni hii na haitaki kubadili mtazamo..viongozi wa kimila wamekuwa mstari wa mbele kupigia debe vitendo hivyo na kutangaza msimu ya ukeketaji na kubariki mchakato mzima lakini sheria haiwabani wanaobanwa ni wazazi na mangariba ni vyema hili likaangaziwa zaidi.’’ Amesema.

Pia amesema baadhi ya viongozi wa kisiasa wanashindwa kuchukua hatua stahiki kwa kuhofia kupoteza kura katika msimu wa uchaguzi.

‘’Baadhi ya viongozi wanashindwa kuchukua hatua stahiki kwa wapiga kura wao kwa kuhofia kupoteza nafasi zao..jamii pia inatuona sisi watetezi kama maadui licha ya kuwasaidia watoto wao dhidi ya ukeketaji ambao mathalani hufanywa ili kuwaandaa kuolewa hata kama ni wadogo.’’ Amesema.

Kupitia taasisi hiyo Bi. Rhobi Samwelly ameeleza kuwa wameweza kuwaokoa wasichana 4000 dhidi ya ukeketaji na ameushukuru ubalozi wa Ufaransa kwa kumpatia tuzo maalum ya utetezi wa haki za binadamu na kupata fursa ya kukutana na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron

Kwa upande wake Afisa Uhamasishaji kutoka Hope For Girls and Women Emmanuel Goodluck ameeleza kuwa  jamii ya Mkoa wa Mara hasa vijana bado wana mtazamo chanya katika suala la ukeketaji kwa kulichukulia kama fursa ya kujipatia kipato.

‘’Vijana katika jamii yangu bado wanachukulia suala la ukeketaji ni sehemu ya kazi ya kujipatia kipato hasa mafundi wa nguo na hata ndugu wa karibu hasa wa kiume hutegemea mali zinazotana na ukeketaji katika kuoa.’’ Amesema.

Aidha amesema licha ya kuonekana maadui katika jamii yao taasisi hiyo imeendelea kutoa elimu hasa katika msimu wa ukeketaji sambamba na kutoa elimu kwa wanafunzi kupitia filamu hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa imeokoa maisha ya mabinti wengi dhidi ya vitendo vya ukeketaji.

‘’Tunaendelea kutoa mafunzo haya kwa jamii ili kuweza kukomesha vitendo hivi na hii ni kwa kushirikiana na polisi kupitia dawati la jinsia, pia tunatoa elimu ya ujasiriamali na kuwahamasisha akina Mama kuwa na vikundi vya ujasiriamali na taasisi kutoa mikopo isiyo na riba ili kutoa nafasi ya kujitengenezea kipato.’’ Amesema.

Amina Ramadhani mwanafunzi wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye aliepuka vitendo hivyo na kusaidiwa na taasisi hiyo amewataka mabinti kuwa na misimamo na kutafuta suluhu pindi familia zao zinapotaka kuwafanyia vitendo hivyo.

‘’Dada zangu wawili walifanyiwa vitendo hivyo na mimi nikafanikiwa kuepukana navyo, mabinti tusimame imara, kwa nafasi yangu nitaendelea kupingana na tamaduni hizi ambazo si rafiki kwa mtoto wa kike.’’ Amesema.

Vilevile Askari wa polisi kutoka kituo cha polisi Mugumu wilayani Serengeti, Mara Sijali Kambuche ameshauri madawati ya jinsia kuwa na ushirikiano na wadau wa maendeleo na masuala ya jinsia na elimu pamoja na Wizara mbalimbali ili kuweza kukomesha vitendo hivyo na kuwataka wanaume wanaotendewa vitendo vya ukatili na wake zao kuripoti katika madawati ya jinsia kote nchini ili waweze kupata msaada wa kisheria.

Katika filamu hiyo ya In The Name Of Your Daughter imeonesha namna mabinti wa kuanzia miaka 6 wanavyoandamwa na suala la ukeketaji kwa gharama ya shilingi kumi na tatu elfu huku asilimia 30 ya mabinti kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania ikiwemo Mara ni wahanga wa tatizo hilo.Afisa Uhamasishaji kutoka Hope For Girls and Women Emmanuel Goodluck (kushoto,) akizungumza katika mjadala huo na  kueleza kuwa  jamii ya Mkoa wa Mara hasa vijana bado wana mtazamo chanya katika suala la ukeketaji kwa kulichukulia kama fursa ya kujipatia kipato.
Askari wa polisi kutoka kituo cha polisi Mugumu wilayani Serengeti, Mara Sijali Kambuche akizungumza wakati wa mjadala huo na kushauri madawati ya jinsia kuwa na ushirikiano na wadau wa maendeleo na masuala ya jinsia na elimu pamoja na Wizara mbalimbali ili kuweza kukomesha vitendo vya ukatili ikiwemo ukeketaji.
 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...