NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, SAME

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu amesema uwekezaji kwenye eneo la viwanda uliofanywa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwenye mkoa huo umeleta faraja kubwa kwa wananchi.

Mkuu huyo wa Mkoa ameyasema hayo Desemba 14, 2022 wakati wa hafla ya uzinduzi wa ukarabati wa Kiwanda cha Kuchakata Tanagawizi cha Mamba Miamba Ginger Growers kilichoko wilayani.

Kiwanda hicho kinamilikiwa kwa ubia kati ya PSSSF na Ushirika wa wakulima wa Tangazwizi wa Mamba Miamba Ginger Growers ambapo PSSSF inamiliki asilimia 67% ya hisa na wanaushirika wanamiliki asilimia 33%.

PSSSF pia imewekeza kwenye kiwanda cha Kimataifa cha Biadha za Ngozi cha Kilimanjaro

“Mmetupa heshima kubwa na mmetupa maendeleo makubwa kwenye mkoa wetu wa Kilimanjaro” alisema Mhe. Babu.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwahimiza wakulima wa Tangawizi kutunza mioundombinu ya kiwanda ili kwa pamoja ilete faida kwa wananchi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini PSSSF, Dkt. Aggrey Mulimuka alisema, Bodi inaridhishwa na uwekezaji unaofanywa na Mfuko kwenye miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kiwanda cha Mamba Miamba.

“Wajibu wetu ni kuhakikisha mradi huu na uwekezaji mwingine unaofanywa na Mfuko unakuwa na manufaa kwa wananchama na bila mashaka yoyote tunaamini mradi huu utalipa.” Alisema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba alisema uwekezaji uliofanywa na Mfuko huo unafanyika kwa kufuata miongozo ya Benki Kuu pamoja na Sera ya Uwekezaji ya Mfuko.

“Lengo kuu likiwa ni kuwa na uendelevu wa kifedha ili kulinda thamani ya fedha za wanachama na lengo lingine ni kupata faida ya uwekezaji ili kukuza hazina na kuongea uwezo wa kulipa Mafao pale yanapohitajika na pia kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi.”

Akizungumzia ukarabati wa kiwanda hicho, CPA Kashimba alisema kiwanda hicho kilijengwa mwaka 2012 lengo likiwa ni kusindika tangawizi kiasi cha tani 9.8 kwa siku jambo ambalo halikuwezekana na kiwanda kilizalisha chini ya tani moja kwa siku kinyume na matarajio sababu kubwa ikiwa ni uwezo mdogo wa mitambo.

Kutokana na sababu hiyo wanaushirika kupitia Mbunge wa jimbo la Same, Mhe. Anne Kilango Malecela uliomba ubia na PSSSF na baada ya kufanyika uchambuzi Mfuko ulikubali kuingia ubia na kuanza ukarabati wa majengo na ufungaji wa mashine mpya za kisasa uliogharibu karibu shilingi Bilioni 2.

“Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha tani 10 kwa siku na kina maabara za kisasa zenye kukidhi viwango vya kimataifa kwa kupima ubora wa tangawizi inayozalishwa kiwandani.” Alifafanua CPA Kashimba.

Mbunge w ajimbo la Same Mashariki Mhe. Anne Kilango Malecela ambaye ndiye alitoa wazo la kuanzishwa kiwanda cha kuchakata Tangawizi katika eneo hilo aliishukuru PSSSF kwa kukubali kuwekeza kwenye kiwanda hicho kwani wakulima watanufaika na uwekezaji huo.

“Ninachoomba, kiwanda tayari tunacho na kina mitambo ya kisasa, tunahitaji tuwe na umeme wa uhakika, na mimi niombe Mkuu wa Mkoa Kiwanda kifungiwa transfoma yake ili kijitegemee na hivyo itapunguza adha ya upatikanaji wa uhakika wa umeme.” Aliomba Mhe. Anne Kilango Malecema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Edward Mpogolo alisema kabla ya uwekezaji huo soko la uhakika la Tangawizi lilikuwa na mashaka lakini mashaka hayo sasa yameondoka kupitia uwekezaji huo wa PSSSF kwani soko la uhakika la Tangawizi lipo.

“Ndugu zetu wa PSSSF wametusaidia kuboresha zao la Tangawizi kwa kutuletea kiwanda na na imani yetu kubwa sana wana Same na hususan sisi wakulima wa zao la Tangawizi watatusaidia kutengeneza soko na kuboresha bei ya Tangawizi katika maeneo yetu na Tanzania kwa ujumla.” Alisema Mhe. Mpogolo.

Naye  mkulima wa kwanza wa zao la Tangawizi katika kijiji cha Goha mahali ambapo kiwanda hicho kipo, Bw. Kilango Chikira Mfanga alisema kiwanda hicho kimeleta faraja kubwa kwa wakulima yeye akiwemo.

“Niliingiza mbegu ya Tangawizi kwenye eneo hili mwaka 1988 na niliweza kuuza maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo Arusha, Moshi na Dar es Salaam na Tangawizi ya hapa ni bora na inapendwa sana.” Alisema.

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu (katikati) akiwa akishuhudiwa na viongozi wa Mfuko w aHifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na wa Wilaya ya Same, wakati akikata utepe kuwashiria uzinduzi wa ukarabati wa kiwanda cha kuchakata tangawizi cha Mamba Miamba Desemba 14, 2022.
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu, akizungumza kwenye hafla hiyo.
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu akipatiwa maelezo na mtaalamu wa Maabara ya udhibiti ubora wa Tangawizi inayozalishwa na kiwanda hicho.
Uchakataji wa tangawizi ukiendelea
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu akisalimiana na mkulima wa kwanza wa zao la Tangawizi katika kijiji cha Goha mahali ambapo kiwanda hicho kipo, Bw. Kilango Chikira Mfanga
Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini PSSSF, Bi. Mazoea Mwera (kushoto) na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria PSSSF, Bi. Vupe Ligate wakiwa wamebeba tangawizi inayozalishwa na kiwanda hicho.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo.
Mhe. Babu akiongozana na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini PSSSF, Dkt. Aggrey Mulimuka (wakwanza kushoto), Mkurugenzi Mkuu PSSSF, CPA Hosea Kashimba (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Edward Mpogolo
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba akizungumza kuhusu uwekezaji wa Mfuko katika kiwanda hicho.
Makamu Mwenyekiti wa Bodhi ya Wadhamini PSSSF, Dkt. Aggrey Mulimuka, akizungumzia jinsi bodi yake ilivyoridhishwa na uwekezaji huo.
Mbunge wa jimbo la Same Mashariki, Mhe. Anne Kilango Malecela akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro, Mhe. Edward Mpogolo akizungumza kwenye hafla hiyo ambapo alionyesha furaha yake kutokana na uwekezaji uliofanywa na PSSSF kwenye kiwanda hicho.
Kiwanda cha kuchakata Tangawizi cha Mamba Miamba

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...