Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akipanda mti aina ya Mdodoma kandokando ya barabara ya Dodoma – Morogoro eneo la Ihumwa Jijini Dodoma wakati akiongoza zoezi la upandaji miti kusheherekea Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar leo tarehe 12 Januari 2022.MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amesema kwa sasa suala la upandaji miti linapaswa kuwa la lazima na kuziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafikia lengo la upandaji miti milioni moja na laki tano kwa mwaka kama ilivyopangwa.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akiongoza zoezi la upandaji miti katika Jiji la Dodoma maeneo ya Ihumwa na Msalato leo tarehe 12 Januari 2023 ikiwa ni katika kusheherekea maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Amesema Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yanapaswa kutumika kama chachu ya kuifanya Tanzania kuwa ya kijani na kurekebisha yale yote yaliofanyika katika kuharibu mazingira.

Aidha Makamu wa Rais amesisitiza ushirikishwaji wa sekta binafsi na wafanyabiashara katika upandaji na utunzaji miti pamoja na kuzisihi familia kuongeza juhudi katika upandaji miti na usafi wa mazingira. Pia amezitaka taasisi za serikali kupanda miti katika maeneo yao na kuhakikisha miti hiyo inaishi.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka viongozi kuwa mfano katika zoezi la upandaji na utunzaji miti kwa kuonesha kwa vitendo. Ameagiza Jiji la Dodoma kuratibu zoezi la usimamiaji miti iliopandwa ili kuhakikisha inaishi na kupendezesha jiji. Aidha amewataka kudhibiti masuala yote ya uchomaji moto maeneo yaliopandwa miti pamoja kukabiliana na changamoto ya uingizaji au upitishaji mifugo katika maeneo hayo. Amesema kila mwananchi anapaswa kuimwagilia miti iliopandwa mbele yake hususani wale wanaomiliki vituo vya mafuta na wanaozalisha tofali.

Dkt. Mpango ametoa wito kwa Waandishi wa Habari hapa nchini kutoa kipaumbele katika kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya upandaji miti na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla. Amesema ni muhimu kwa waandishi wa Habari kutoa habari za mifano ya wale walioweza kutunza mazingira ili wawe hamasa kwa watanzania wengine.

Pia Makamu wa Rais ameagiza Wakala wa Misitu Nchini kupitia upya utaratibu wa leseni za ukataji miti kwaajili ya mkaa ili kuokoa maeneo ambayo yana uoto na vyanzo vya maji.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amesema tayari mipango mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira imeanza kutekelezwa ikiwemo kugawa maeneo yaliopandwa miti kwa taasisi za serikali na binafsi ili waweze kusimamia na kuhakikisha miti hiyo inaishi.

Waziri Jafo amemuhakikishia Makamu wa Rais zoezi la upandaji miti na kuitunza miti hiyo litakua endelevu wakati wote.

Kwa Upande wake mdau wa Mazingira na Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Pinda ametoa wito kwa wananchi kuzingatia utaratibu wakati wa upandaji wa miti ikiwemo kuandaa mazingira ya upandaji na kufuata maelekezo ya wataalamu ili kufahamu aina ya mti na mahali unapopaswa kupandwa. Mheshimiwa Pinda amesema Jiji la Dodoma linakabiliwa na upungufu wa mvua hivyo ni vyema uchimbaji wa mashimo pamoja na nafasi baina ya mti na mti ukawa wa kitaalamu zaidi ili kuepusha miti hiyo kutofikia lengo.

Pia Pinda amesema Jamii inao wajibu mkubwa wa kusimamia na kutekeleza kwa makini yale yote yanayopelekea Maisha ya binadamu kuwa salama ikiwemo upandaji wa miti na kuhakikisha inafikia lengo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema upandaji miti katika vyanzo vya maji umepewa kipaumbele mkoani Dodoma kwa kuanza na Bonde la Mzakwe ambalo limekua na changamoto ya ukuaji wa miti. Amesema tayari wataalamu wamewezesha aina ya miti inayopaswa kupanda pamoja na kuweka mazingira yatakayookoa miti hiyo dhidi ya hatari ya moto.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...