Na Lusajo Mwakabuku - WKS

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Haki na Sheria, amefungua na kushiriki kikao wa Mawaziri wa Sheria na Haki kilichofanyika Jijini Accra-Ghana kuanzia Tarehe 21 hadi 22 Januari,2023.

Akitoa hotuba ya utangulizi kabla kuanza kwa kikao hicho, Waziri Ndumbaro aliwashukuru wataalamu wa Kisheria wa Serikali kwa kujadili na kuzichanganua kisheria hati zilizoletwa kwao ili waweze kuzipitia na kuwashauri wakuu wa nchi zao.

“Kwa namna ya pekee nitoe shukrani kwa wataalamu wa Kisheria wa Serikali kutoka nchi washiriki waliokutana kujadili na kuchakata kisheria hati hizi tunazokwenda kuzipitia” Alisema Ndumbaro.

Kamati ya wataalam inajumuisha Wataalam kutoka Nchi Wanachama wanaohusika na sekta zinazohusiana na masuala ya Haki na Sheria, ambayo mikutano yake hutangulia kabla ya mkutano wa ngazi ya Mawaziri.

Aidha Waziri Ndumbaro alielezea kufurahishwa kwake na namna kamati hiyo ya wataalamu ilivyoweza kufanya kazi kwa uweledi licha ya kuzuka kwa mjadala juu ya baadhi ya vipengele vilivyowasilishwa katika itifaki zilizokuwa zinajadiliwa huku wengine wakitaka baadhi ya sehemu za itifaki hizo zifutwe.

“Nimefahamishwa kuwa kulikuwa na mjadala mkali wakati wa kikao cha Wataalam wa Sheria wa Serikali uliotokana na kutokukubaliana kwa baadhi ya mambo ambayo baadhi yao waliyapa kipaumbele. Hali hiyo ilipelekea mapendekezo ya kufutwa kwa baadhi ya maandishi. Lakini kwa kuzingatia maagizo yetu kwao hilo haikuwezekana”. Aliongeza Ndumbaro

Waziri Ndumbaro alisema licha ya majadiliano hayo, alitaarifiwa kwamba mazungumzo yao yalikuwa mazuri na yenye kujenga na yalifanyika katika hali ya utulivu, na kwamba mvutano huo ulipelekea kupatikana kwa maoni mengi mazuri yaliyoboresha rasimu wanayoijadili katika kikao chao.

Katika Mkutano huo Kamati ya Mawaziri wa Sheria na Haki umepitia, kuchambua na kuhakiki itifaki zitakazowasilishwa kwenye Kikao cha Wakuu wa Nchi za Afrika Februari, 2023. Itifaki hizo ni pamoja na Itifaki ya Sera za Ushindani Afrika, Itifaki ya Haki za Miliki Ubunifu Afrika na Itifaki ya Uwekezaji Afrika baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Kamati ya Wataalamu iliyoongozwa na Bi.Mary Makondo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria.

Itifaki zilizojadiliwa zitawezesha kuwa na Afrika inayoondoa vikwazo katika Soko huru, ushirikiano wa kiuchumi katika maeneo ya biashara na ukuaji wa viwanda ili kufikia malengo ya Afrika ya Ajenda ya Mwaka 2063.

 Dkt. Damas Ndumbaro (katikati) akiongoza kikao cha Saba cha Kamati ya Mawaziri wa Sheria na Haki kilichofanyika Accra – Ghana.

Dkt. Damas Ndumbaro Waziri wa Katiba na Sheria (wa Tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya Pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo (wa Tatu kutoka kushoto) na wataalamu wengine mara baada ya kuhitimishwa kwa kikao hicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...