Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba amepongeza juhudi zinazofanywa na sekta ya kibenki katika kuimarisha mwelekeo wa ujumuishaji wa fedha nchini.
Akizungumza
katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na wanachama wa Chama
cha Mabenki Tanzania (TBA) jijini Dar es salaam jana, Gavana Tutuba
alipongeza safari ya mabadiliko ya kidijitali ambayo benki ya biashara
imeanza katika kutoa urahisi na kufikia wigo mpana wa wateja. "Utendaji
imara wa benki katika mwaka uliopita ni ushuhuda wa mawazo ya kibunifu
yaliyowekwa na benki kuvutia wateja zaidi na kuwapa uzoefu bora.
Serikali
inatambua kazi nzuri ambayo benki hizo zimekuwa zikifanya katika
kupanua huduma za kifedha kwa watanzania walio wengi, wakiwamo katika
sekta rasmi ya fedha. Naipongeza TBA kwa jitihada zake mbalimbali kwa
miaka mingi na nazipongeza benki kwa utendaji wao mzuri wa kifedha. BOT
yaahidi mwendelezo wa mashirikiano, " alisema Gavana Mkuu.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Mabenki Tanzania (TBA),
Theobald Sabi, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya
Taifa (NBC), alitoa shukrani kwa niaba ya TBA kwa serikali na Benki Kuu
Tanzania (BOT) kwa ushirikiano na jitihada endelevu katika kukuza
mazingira mazuri ya kibiashara. "TBA inatambua ushirikiano na msaada
kutoka Serikalini na BOT ambao umesababisha sekta kupiga hatua kubwa.
Kwa
mfano, kufikia Desemba 2022, Benki za Tanzania zilipata faida ya zaidi
ya sh1.164 trilioni, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia kuzidi ile
alama ya faida ya trilioni. Tumeona pia ukuaji mkubwa katika maeneo
mengine, kama vile huduma za kibenki kupitia mawakala, kidijitali,
mikopo kwa sekta binafsi, na miongozo ya biashara yenye kujenga ambayo
imetufanya kustawi. Tunashukuru sana," alisema Sabi.
Aidha naye,
Mkurugenzi Mtendaji wa TBA, Tuse Joune alisema kuwa TBA kwa sasa
inatekeleza Mkakati wa Miaka Mitano (2023-2027) ambao utazinduliwa hivi
karibuni kwa umma. "Nina furaha kutangaza kwamba mpango wetu wa miaka
mitano (2023-2027) sasa uko tayari kwa uzinduzi, na hivi karibuni
tutaupeleka kwa umma," alisema.
Mbali na kumkaribisha Gavana
Tutuba, TBA pia ilitumia hafla hiyo kumuaga Gavana wa Benki Kuu
Tanzania(BOT) anayemaliza muda wake, Prof. Florence Luoga, ambaye
amestaafu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...