Na Mwandishi wetu- Tabora

Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili MO iko mbioni  kusogeza huduma zake za kibingwa kwa wakazi wa mkoa wa Tabora na mikoa jirani katika  Hospitali ya Rufaa ya Nkinga ili kuwaondolea wananchi  usumbufu na gharama kubwa kufuata huduma hizo Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema imekua azma ya Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha huduma za kibingwa zinasogezwa karibu na wananchi na kuwaondolea usumbufu wananchi wa kuzifuata huduma hizo umbali mrefu.

Tulipokea wito wa wenzetu wa Hospitali ya Rufaa Nkinga kuja kutembelea hospitali yao, kuona miundombinu na vifaa vilivyopo ili tuone namna bora ya kusogeza huduma zetu kwa wakazi wa mkoa wa Tabora na mikoa jirani, leo tumetembelea hospitali hii na tumeona mazingira yao kwakweli wanafanya kazi kubwa na nzuri na sisi tunawaahidi kusogeza huduma zetu hapa kama ambavyo Serikali inaelekeza.

Aidha, Dkt. Boniface amesema kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Afya na sekta nyingine ipo kwenye mchakato wa bima ya afya kwa wote ambayo itawapa wananchi uhakika wa matibabu ya kibingwa wakati wote. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya rufaa ya Nkinga Bw. Victor Ntundwe amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface kwa kuitikia wito na ombi la kufika katika hospitali ya Nkinga ili kuona namna bora ya kuanzisha ushirikiano ili kusogeza huduma za kibingwa za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kwa wakazi wa Tabora na mikoa jirani.

“Leo imekua siku ya pekee kwetu kwani tumempokea Mkurugenzi Mtendaji wa MOI na timu yake ambao pamoja na mambo mengine wametembelea hospitali yetu ili kuona ni namna gani tunaweza kuanzisha huduma za MOI hapa, kwaweli tumefarijika sana na tunaamini matunda ya ziara hii yataonekana siku si nyingi. Alisema Bw. Ntundwe

Mganga Mkuu wa Hospitali ya rufaa Nkinga Dkt. Tito Chaula amesema ushirikiano kati ya MOI na Nkinga utaleta tija kwani kwa kipindi kirefu wananchi wamekua wakipata usumbufu wa kufuata huduma mbali na kwa gharama kubwa hivyo kuanza kwa huduma za MOI katika hospitali hiyo kutamaliza changamoto hiyo.
Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...