Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka ameshiriki mazishi ya marehemu Adam Halenga, Afisa Misitu wa Wilaya ya Uvinza aliyeuwawa Januari 31, 2023 pamoja na wenzake wawili kwa kuvamiwa na kundi la wafugaji wakati akitekeleza majukumu yake katika Hifadhi ya Msitu wa Kijiji cha Chakulu wilayani Uvinza mkoani Kigoma.

Akitoa salamu za pole za Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ndugu, jamaa, familiia na wafanyakazi wenzake na wahifadhi wote nchini wakati wa mazishi hayo yaliyofanyika katika Kata ya Nguruka wilayani Uvinza Prof. Sedoyeka ameeleza kuwa Serikali imepata pigo kufuatia kifo cha mtumishi huyo kutokana na moyo wake wa kupenda uhifadhi, maisha ambayo aliyaishi hapa duniani akifanya kazi ya kutunza mazingira ya misitu kazi ambayo imekua na faida kubwa kwa wananchi wote ikiwemo kuleta mvua.

“ Kama Serikali kitendo kilichofanyika cha kuvamia, kuwapiga na kuwauwa ndugu hawa waliokuwa wakitekeleza majukumu yao kisheria hakikubaliki, kitendo hiki ni cha kikatili hakikubalik. Sisi kama Serikali hatutakivumilia, tutahakikisha waliohusika wote wanakamatwa. Nashukuru Jeshi la Polisi limeshachukua hatua na linaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha wale wote waliohusika wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria” Amesisitiza Prof. Sedoyeka.

Amewaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi au viongozi wao wa Serikali za mtaa kutokana na taarifa zozote watakazozisikia au kuzipata kuhusu kitendo kilichofanyika ili wote walioshiriki katika kutenda kitendo hicho cha kinyama waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Prof. Sedoyeka amesisitiza kuwa Tanzania inaongozwa kwa misingi ya Sheria huku akiwataka wananchi waendelee kuungana pale wanapoona baadhi ya watu wachachache wanaharibu misingi ya amani na utulivu iliyojengwa ndani ya Taifa la Tanzania pia waendelee kukemea na kupiga vita vitendo vya baadhi ya watu wachache wanaojichukulia sheria mkononi kwa manufaa yao binafsi.

Aidha, amewashukuru wananchi wote waliojitokeza kushiiriki katika msiba, michango mbalimbali na mazishi ya mtumishi huyo ambaye enzi za uhai wake alijitolea kulinda rasilimali za Misitu katika eneo lake la Wilaya ya Uvinza kwa manufaa ya Watanzania wote.

Marehemu Adamu Halenga aliuwawa Januari 31, 2023 akiwa kwenye doria katika Hifadhi ya Msitu wa Kijiji cha Chakulu mara baada ya kikosi cha doria cha Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza alichokuwa akikiongoza kilipovamiwa na wafugaji waliokuwa na lengo la kupora mifugo yao iliyokuwa imekamatwa Hifadhini.
Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...