• waandaaji Waonya kuhusu umiliki wa nambari bandia; uuzaji tiketi kinyume cha taratibu za usajili

ZIKIWA zimesalia wiki chache kabla ya kufanyika mashindano ya Kilimanjaro International Marathon, wandaaji wa mbio wa mbio hizo maarufu kama Kilimanjaro Premium Lager Marathon wametangaza kufungwa kwa usajili wa washiriki kwa mwaka wa 2023 baada ya idadi iliyowekwa ya ushiriki kufikiwa tangu wiki iliyopita

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waandaaji hao, usajili kwa ajili ya ushiriki wa mbio za Kilimanjaro Premium lager za kilomita 42 na ule wa kilomita 21 Tigo Half Marathon umefungwa rasmi.

"Hata hivyo bado usajili kwa ajili ya mbio za kujifurahisha za Grand Malt 5km utaendelea, ila si kwa njia ya mtandao tena bali kupitia vituo vya kuchukulia namba jijini Dar es Salaam (Februari 18 na 19), Arusha (Februari 21 na 22) na Moshi (Februari 23, 24 na 25)," imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa tarehe ya mwisho ya kujiandikisha kwa mbio hizo za kilomita 42 na kilomita 21 ilikuwa ni Februari 6, 2023 lakini kwa mujibu wa waandaaji, nafasi za kujiandikisha zilijaa kabla ya tarehe hiyo jambo lililopelekea zoezi la usajili huo uliofanyika kupitia tovuti yawww.kilimanjaromarathon.com na kupitia Tigopesa, kufungwa.

"Tunawajibika kuchukua hatua hii ili kuakisi viwango vya kimataifa vilivyowekwa kuhusiana na usajili ili kuhakikisha maandalizi yanafanywa mapema ili kuepuka changamoto ambazo si za lazima wakati wa tukio husika”, imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo Imeongeza, "Hatua hii itatusaidia kama wandaaji wa mbio hizo kufanya maandalizi ya mapema, ikiwemo kuhakikisha uweko wa maji ya kutosha katika maeneo yatakayotumiwa na washiriki, medali za kutosha, vesti za kukimbilia pamoja na usalama wa uhakika kwa washiriki na eneo la Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi ambako tukio litafanyikia".

Huku hayo yakijiri, waandaji wa mbio hizo pia wametoa onyo kali kwa wale wanaotajwa kuhusika na uuzaji wa tiketi kwa njia ya mtandao kinyume cha taratibu ambapo umeonya watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Kuna taarifa zinazodai ya kuwa kuna baadhi ya watu ambao si waaminifu wanauza tiketi za Kilimanjaro Marathon mtandaoni, tunatoa rai kwa wananchi kutoa taarifa kwa wandaaji iwapo watawabaini wanaofanya mchezo huo mchafu ili hatua zichukuliwe dhidi yao kwani usajili ushafungwa”, imesema taarifa hiyo ya waandaji.

Waandaaji pia wameonya dhidi ya washiriki wanaokimbia kwa kutumia namba za ushiriki zisizo za kwao kwa mujibu wa usajili ambapo uongozi huo umesema hautawajibika na changamoto yoyote itakayotokana na hali hiyo, ambapo pia umesema kuwa, watakaobainika kufanya hivyo hawatapokea medali na majina yao hayatawekwa kwenye orohda ya walioshiriki mbio hizo mwaka huu.

"Pia tumekuwa na visa vya watu kukimbia na kwa kutumia nambari za zamani, hawa nao wakibainika watachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwafungiwa kabisa kushiriki mbio za Kilimanjaro Marathon,” iliendelea kusema taarifa hiyo ya waandaaji.

Wadhamini wa mbio za mwaka huu, ni pamoja na wadhamini wakuu Kilimanjaro Premium Lager-42km, Tigo- 21km Half Marathon, Grand Malt 5km Fun Run water table wadhamini TPC Sugar, Simba Cement, Kilimanjaro Water, TotalEnergies na wauzaji rasmi Kibo Palace Hotel, CMC Automobiles, KK Security na Keys Hotel.

Mbio hizi huandaliwa na kampuni ya Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa nchini na kampuni ya Executive Solutions Limited.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...