Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Bao pekee lililofungwa na Mlinzi wa kati wa Simba SC, Henock Inonga Baka katika dakika ya 20’ ya mchezo dhidi ya Vipers SC ya Uganda, limefufua matumaini ya timu hiyo kusonga mbele katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL).
Katika mchezo huo wa Kundi C uliopigwa kwenye dimba la St. Mary’s Kitende, Entebbe nchini Uganda, wenyeji Vipers SC walilazimika kuacha alama tatu muhimu nyumbani baada ya Simba SC kuingia na mikakati imara ya kuondoka na alama hizo ambazo walizikosa katika michezo miwili mfululizo kwenye Michuano hiyo.
Kocha wa Simba SC, Robertinho ambaye aliwahi kuifundisha Vipers SC kabla ya kutua Simba SC, aliingia na mikakati hiyo na kufanikiwa kuwazuia Washambuliaji wa Cobra (Vipers) ambao waikuwa wanaongozwa na Nahodha wao, Milton Kalisa.
Baada ya kupata bao hilo kwenye dakika ya 20’, Simba SC walicheza kwa nidhamu ya hali ya juu kulinda bao hilo sanjari na kutafuta mabao mengine. Hata hivyo, Simba SC wakiwa na Washambuliaji wao, Moses Phiri, Kibu Dennis, Clatous Chama wakisaidiwa na Saido Ntibazonkiza waliendelea kuwanyima uhuru Walinzi wa Vipers kwenye dakika zote 90’.
Kwa matokeo hayo, Simba SC wanapata alama tatu muhimu na kusogea hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi hilo C, huku Vipers wakiburuza mkia wakiwa na alama moja pekee, Horoya AC wana alama nne ambao watacheza na Raja Casablanca wanaoongoza Kundi wakiwa na alama sita kibindoni.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...