Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Wawakilishi wa Tanzania katika Michuano ya Kimataifa, Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL) na Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC), Simba na Yanga wameanza vibaya Michuano hiyo baada ya wote kupoteza kwenye michezo yao ya kwanza wakiwa ugenini.

Walianza Wekundu wa Msimbazi, Simba SC ambao wanawakilisha taifa kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa katika hatua ya makundi, ambao Februari 11, 2023 kwenye dimba la General Lansana Conté nchini Guinea walipoteza mchezo wao dhidi ya wenyeji Horoya AC baada ya kupata kipigo cha bao 1-0, bao hili lilifungwa na Pape Ndiaye 18’.

Katika mchezo huo wa Kundi C la Michuano hiyo ya CAF CL, Simba SC wapo na timu za Raja Casablanca ya Morocco, Vipers SC ya Uganda na Horoya AC ambao wameanza nao kwenye mchezo wa kwanza kwenye dimba hilo lililopewa jina la Rais wa zamani wa Guinea, Lansana Conté.

Wakiwa katika nafasi ya tatu hadi sasa bila alama yoyote, Wekundu wa Msimbazi watacheza mchezo wao wa pili wa Kundi hilo dhidi ya Raja AC kwenye uwanja wa nyumbani Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Februari 18, 2023. Katika mchezo mwingine wa Kundi hilo, Vipers SC kutoka Uganda walipata kichapo kibaya cha mabao 5-0 nchini Morocco dhidi ya wenyeji Raja AC. 

Kwa upande wa Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC), Young Africans SC nao wamepokea kichapo cha mabao 2-0 nchini Tunisia dhidi ya wenyeji Union Sportive Monastirienne kwenye dimba la Olympique Hammadi Agrebi mjini Tunis.

Katika mchezo huo wa Kundi D la Michuano hiyo, mabao ya wenyeji US Monastir yalifungwa na Mlinzi wa kati wa timu hiyo, Mohamed Saghraoui kwenye dakika ya 10’ ya mchezo huku bao la pili likifungwa na Mshambuliaji Boubacar Traorè katika dakika ya 16’. Hadi kipyenga cha mwisho Wananchi walitoka kwenye dimba hilo wakiwa wamelowa mabao 2-0.

Mapema, kwenye mchezo wa Kundi hilo la D, TP Mazembe ya DR Congo walipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wageni katika dimba la Stade de TP Mazembe, AS Real Bamako kutoka nchini Mali, mabao ya Mazembe yalifungwa na Jephté Bola 24’, Alex Ngonga 38’ na Patient Mwamba 94’ huku bao la Real Bamako likifungwa na Souleymane Coulibaly 32’.

Februari 19, mwaka huu, Wananchi watakuwa na kibarua dhidi ya TP Mazembe kwenye mchezo wa pili wa Michuano hiyo katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, huku US Monastir wakiwafuata Real Bamako nchini Mali.

Kiungo Mshambuliaji wa Young Africans SC, Stephane Aziz Ki (wa mbele) akimiliki mpira mbele ya Mchezaji wa US Monastir ya Tunisia kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika, mchezo huo ulichezwa kwenye dimba la Olympique Hammadi Agrebi mjini Tunis. Yanga SC walipoteza kwa mabao 2-0.

Kiungo Mkabaji wa Simba SC, Ismael Hamed Sawadogo akiondoka na mpira mbele ya Mchezaji wa Horoya AC katika mchezo wa kwanza wa Michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika kwenye dimba la General Lansana Conté. Simba SC walipoteza mchezo huo kwa bao 1-0.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...